Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wazee Yanga waendeleza `bifu`

2nd May 2012
Print
Comments
Lloyd Nchunga

Katika kile kinachoonekana kuwa ni kuendeleza malumbano, wazee wanaojitambulisha kuwa ni wa Yanga wamemjia juu mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga na kudai kwamba hawakukurupuka wakati walipoutangazia umma kuwa wameachiwa majukumu ya kuisimamia timu hiyo kuelekea mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya watani zao wa jadi, Simba.

Kauli ya wazee hao imekuja siku chache baada ya Nchunga kupinga madai ya awali kuwa wazee hao wamekabidhiwa timu kwa ajili ya kuiandaa kwa mechi dhidi ya Simba itakayochwezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari, Nchunga alisema kuwa timu bado iko mikononi mwa uongozi na kwamba, walishindwa kuwapa wazee hao kama walivyokubaliana awali kutokana na kundi hilo kushindwa kueleza vyanzo vyao vya mapato ambavyo vitawasaidia kuihudumia timu.

Hata hivyo, akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ibrahim Akilimali aliyejitaja kuwa ni katibu wa wazee hao, alisema kuwa wao hawakuwa na nia ya kuwapokonya viongozi madaraka bali lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanaiandaa vyema timu hiyo ili iifunge Simba na pia kufanya usajili kabambe utakaowapa nguvu ya kutetea taji la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na pia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Akilimali alisema kuwa wamesikitishwa na kauli iliyotolewa na Nchunga kwamba hawaamini kuwapa timu wakati tayari walishamweleza nia yao; kwamba hawako tayari kuona wanafungwa na Simba na pia kuwashuhudia mahasimu wao hao wa jadi wakitwaa ubingwa kupitia mgongoni mwao.

Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Jabir Katundu, alisema kuwa wamesikitishwa na kitendo cha uongozi kuwakatalia wazee hao kuingia kwenye jengo la makao makuu lililopo katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.

"Sisi tulishamweleza yeye (Nchunga) abaki na uenyekiti wake, lakini atupe timu ili tuisimamie katika mechi dhidi ya Simba… hatutaki Simba wawe fahari kwa mambo mawili ya kutufunga na kubeba ubingwa," aliongeza Katundu.

Wakati huo huo, timu ya Yanga iliondoka jana asubuhi kuelekea Bagamoyo ili kujiandaa na mechi yao dhidi ya Simba, ikiwa chini ya kocha msaidizi Fred Felix Minziro.

Mahasimu wao Simba ambao watahitaji sare tu katika mechi hiyo ya Jumamosi iliwajihakikishie ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara, wako Zanzibar tangu juzi wakiendelea kujifua dhidi ya Yanga.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles