



Fainali za Mataifa ya Ulaya (Euro) 2012 zilianza Ijumaa katika nchi za Poland na Ukraine ambapo maelfu ya mashabiki wa soka nchini na kwingineko duniani wamekuwa wakifuatilia kupitia matangazo ya vituo mbalimbali vya televisheni.
Ni michuano inayohusisha mataifa ya Ulaya yaliyofuzu katika fainali hizo zinazofanyika kila baada ya miaka minne na kuhusisha nyota wanaocheza katika ligi kuu mbalimbali; wakiwemo wanaotoka katika ligi kuu maarufu za England, Hispania, Ujerumani na Italia.
Sisi tunadhani kwamba huu ni wakati mzuri kwa wachezaji, makocha, viongozi, mashabiki na wadau wengine wa soka kufuatilia kwa umakini zaidi michuano hiyo ili wapate cha kujifunza.
Kuanzia ndani ya uwanja, makocha na wachezaji wao wanaweza kujifunza mbinu mbalimbali za kucheza dhidi ya timu inayoonekana kuwa na kiwango kikubwa na kushambulia zaidi kuliko wao.
Washambuliaji wanapata mbinu mbalimbali pia za kupenya kwenye ukuta wa mabeki wa timu inayocheza kwa kujihami zaidi na kusubiri mashambulizi ya ghafla, mtindo unaofahamika zaidi katika mchezo wa soka kama ‘kupaki basi’.
Kwa mfano, tunaona kwamba kupitia fainali za Euro 2012, wachezaji wetu wanaweza kujifunza pia namna ya kukabiliana na mechi inayoambatana na shinikizo kali, ikiwa ni pamoja na kuhimili kelele za mashabiki wenye kawaida ya kuwabeza wapinzani wao kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho.
Mathalan, tunadhani kwamba miongoni mwa mbinu za kiufundi ambazo hadi sasa wachezaji wetu wamezipata ni zile zilizoonekana katika mechi ya ufunguzi ya Kundi B kati ya Uholanzi na Denmark.
Katika mechi hiyo, wafuatiliaji wengi wa soka walitarajia kuona kuwa Uholanzi yenye kikosi kilichojaa wachezaji nyota kama Van Persie wa klabu ya Arsenal ya England, Roben wa Bayern Munich ya Ujerumani, Ibrahim Affelay wa Barcelona ya Hispania na Rafael Van DerVaart wa Tottenham Hotspur watapata ushindi mnono dhidi ya Denmark isiyokuwa na wachezaji wengi wenye majina makubwa kulinganisha na wao.
Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti. Wachezaji wa Denmark wakaonekana wakicheza kwa malengo zaidi na kujituma katika kila idara.
Wakajazana wengi langoni kwao kila mara waliposhambuliwa na badala ya kubutua mipira mbele wakati wakiokoa, wakatulia na kupeana pasi ndefu, lakini zilizojaa umakini na kusababisha hatari nyingi langoni mwa wapinzani wao kuliko ilivyotarajiwa.
Mwisho wa mechi hiyo, ni Denmark ndio walioibuka kidedea baada ya kupata ushindi wa bao 1-0. Uholanzi wakatoka uwanjani na sifa ya kucheza pasi nyingi na kupiga mashuti mengi pia, lakini karibu yote yakienda nje ya lango kutokana na ulinzi ‘ngangari’ wa Denmark.
Ni wazi kwamba mechi hiyo imetoa somo kuwa hakuna timu ya kubezwa kwani lolote huweza kutokea. Kocha wa Denmark na benchi lake la ufundi walijua kwamba Uholanzi wana wachezaji wenye vipaji zaidi kuliko wao na hivyo wakabuni mbinu sahihi za kuwazuia na kucheza kitimu zaidi kabla ya kuibuka na ushindi.
Hata hivyo, baada ya mechi kumalizika na kujikuta wamelala katika mechi waliyotarajia kushinda, wachezaji wa Uholanzi walikubaliana na matokeo na kuwapongeza wenzao wa Denmark.
Hata mashabiki wao waliojikuta wakiumizwa na matokeo hayo, kamwe hawakufanya tukio lolote baya na badala yake wakajipa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zitakazofuata.
Kuna baadhi ya makocha wametoa nafasi ya kutosha kwa wachezaji chipukizi na hivyo kuunda vikosi vikali vyenye mchanganyiko mzuri wa umri.
Kupitia fainali za Euro, viongozi wa mamlaka za soka nchini wanayo fursa nzuri pia ya kujifunza namna nzuri ya kuandaa mashindano kwa namna bora zaidi na kutimiza malengo waliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na kuzingatia malazi, usafiri, miundombinu ya uwanja na hata ratiba ya michuano husika.
Kwa ujumla, fainali za Euro 2012 zinatoa nafasi nzuri ya kujifunza kwa wadau wa soka watakaoamua kufuatilia michuano hiyo kwa umakini zaidi badala ya kugombania timu za kushangilia.