Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga kuivaa APR bila Berko, Sunzu

26th July 2012
Print
Comments
Mabingwa watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga

Mabingwa  watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga leo watashuka dimbani kuwavaa 'maafande ' wa Rwanda, APR katika mechi yao ya nusu fainali ya pili ya michuano hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Leo itakuwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye mashindano hayo ambapo Ijumaa iliyopita, zilikutana katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C ambapo Saidi Bahanuzi aliifungia Yanga magoli yote katika ushindi wa 'Wanajangwani' wa mabao 2-0.

Katika mechi ya leo, Yanga inayonolewa na Mbelgiji Tom Saintfiet, itamkosa kipa wake chaguo la kwanza, Mghana Yaw Berko ambaye aliumia katika mechi ya robo fainali waliyoshinda kwa penati 5-3 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar. Kipa Ally Mustapha 'Barthez' aliyetua Yanga msimu huu akitokea Simba ndiye anayetarajiwa kusimama langoni.

Kiungo Nizar Khalfan ambaye pia alitua Yanga hivi karibuni baada ya kuachwa na klabu ya Philadephia Union ya Marekani atakosekana vilevile leo kwa vile badfo anasumbuliwa na maumivu ya nyonga.

Saintfiet alisema kwamba wachezaji wake wanafahamu kuwa mechi hiyo dhidi ya APR itakuwa ngumu na hivyo wataingia uwanjani kwa lengo la kupambana ili kuhakikisha kuwa wanafika fainali na hatimaye kutetea ubingwa wao.

Kocha huyo alisema kuwa ataingiza kikosi kitakachocheza tofauti na walivyokutana katika mechi ya hatua ya makundi ambayo kuna wakati walikuwa wakizidiwa sana katika kumiliki mpira.

Saintfiet aliongeza kwamba 'presha' ya APR kutokubali kufungwa kwa mara ya pili mfululizo inaweza kuwasaidia kuifunga tena.

Kocha wa APR ambaye anamaliza mkataba wake mwisho wa mwezi huu, Ernie Brandts, aliliambia gazeti hili kwamba kikosi chake kina njaa ya ushindi na hivyo ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Brandts alisema kuwa mechi hiyo itakuwa ni yenye ushindani mkali na kwamba wao wamejipanga kushinda kwa nia ya kusonga mbele na pia kulipiza kisasi kwa wenyeji.

"Tulikuja kushindana na tutaendelea kushindana, hatutakubali kuona tunapoteza tena kwa Yanga, tutajituma zaidi na hatutawaangusha wale wanaoipenda APR," alisema mshambuliaji wa APR, Suleiman Ndikumana, ambaye aliwahi kuichezea Simba.

APR ambao mwaka 2010 walitwaa ubingwa wa mashindano hayo, leo watamkosa beki wao wa kati, Kabange Twite, ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Kabla ya mechi ya Yanga dhidi ya APR, mchezo mwingine wa nusu fainali utachezwa saa 7:00 mchana kati ya wawakilishi wengine wa Tanzania Bara, Azam dhidi waalikwa, klabu ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Simba magoli 3-1 wakati Vita iliwaondoa Atletico ya Burundi juzi baada ya kuifunga mabao 2-1.

Timu zitakazoshinda leo zitakutana katika fainali itakayochezwa keshokutwa huku  watakaopoteza wakitarajiwa kusaka nafasi ya mshindi wa tatu ambayo zawadi yake ni dola za Marekani 10,000 (Sh. Milioni 15).

Wakati huo huo, jana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa kiingilio cha juu leo ni Sh. 20,000 na kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 5,000.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment