Tuesday Jun 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanatuhumiwa, wanatimuliwa, hawashitakiwi

10th June 2012
Print
Comments

Wimbi la ‘timua timua’ watendaji wabovu wanaodaiwa kuliingia taifa hasara hususani ya mabilioni ya Shilingi kwa ujumla wa hesabu zake, inaendelea.

Tangu Rais Jakaya Kikwete alipolitangaza Baraza la Mawaziri kutokana na mabadiliko madogo yaliyofanywa baada ya shinikizo la wabunge, huku akiwatimua kazi mawaziri sita na naibu mawaziri wawili, hali hiyo imehamia ngazi za wizara.

Tayari mawaziri Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasli na Utalii) na Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) wamefikia uamuzi mgumu, kuwatimua baadhi ya watendaji waliobanika kuhusika na ‘madudu’ ya kiutendaji.

Sababu kubwa zaidi iliyoshinikiza uhalali kwa mawaziri hao kuwatimua watendaji waliopo chini ya wizara zao, ni ubadhirifu wa mali, fedha na matumizi mabaya ya ofisi za umma, walipokuwa wanazishikilia kwa niaba ya umma.

Hali hiyo ndio iliyojitokeza hata wakati Rais Kikwete akitangaza kuwatimua kazi mawaziri sita na naibu mawaziri wawili. Ni ubadhirifu wa mali, fedha na matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Matukio hayo yanayofanyika kwa sababu zinazofanana, yanatoa ‘picha’ moja kwamba ndani ya serikali iliyopo madarakani, wapo baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema kwa nchi na watu wake.

Wamekabidhiwa dhamana ya kuzitunza, kuzilinda na kuweka mikakati thabiti ya kuzitunza rasilimali za umma, wakizitumia ofisi za umma kwa maslahi ya umma, inakuwa kinyume chake.

Ni sawa na kusema neno ‘maslahi ya umma’ halipo kwenye kamusi ya vichwa vyao! Ndio maana kila kukicha wanabuni na kutekeleza mipango ya ‘kuitafuna nchi’. Wanakula, wanakula, wanakula hadi kuvimbiwa, lakini hawasazi.

Rais Kikwete na mawaziri Dk Kigoda, Balozi Kagasheki na Dk Mwakyembe, wameonyesha dalili na ishara kuwa nchi inaliwa. Kinachotakiwa sasa ni mkakati wa kuziokoa rasilimali na fedha za umma zilizosalia, zisiendelee kumalizwa na ‘mchwa’.

Kwa maana katika moja ya hotuba zake, Rais Kikwete aliwahi kuthibitisha kwamba ‘mchwa’ wamejaa kwenye ngazi ya halmashauri ya wilaya na manispaa, lakini si huko tu.

Sasa wamebainika kwenye serikali kuu yaani wizarani, wameingia hadi kwenye idara za serikali. Ni wazi kwamba serikali imejaa wasiokuwa na utashi mwema katika utumishi wa umma, ndio maana wanabainika kila ngazi, wanatajwa kwa majina na nyadhifa, wengine wanatolewa kafara, wanatimuliwa kazi.

Lakini kuwatuhumu na kuwatimua kazi wahusika katika kadhia ya wizi na ubadhirifu wa mali ama matumizi mabaya ya ofisi za umma, kunatosha kuwa kigezo kinachouaminisha umma, kwamba serikali imedhamiria kuutokomeza ufisadi?

Kwamba watajwe kwa tuhuma nzito, wafukuzwe kazi ili waende kujipanga vizuri, wakitumia vizuri kiasi cha fedha walichokichota kujiimarisha kiuchumi! Haiwezekani.

Ikiwa hali hiyo itajikita mioyoni mwa wenye kukabidhiwa dhamana ya utumishi wa umma, nchi itaendelea ‘kuliwa’, itafilisiwa, itapigika na wananchi wake wataendelea kuwa masikini wa kutupwa.

Hali hiyo ikiendelea, kwamba ‘ushujaa’ uonekane katika kuwataja washukiwa, kuwatuhumu na kuwatimua kazi peke yake, itakuwa sawa na kutwanga maji kwenye kinu, hakuna mabadiliko chanya yatakayopatikana.

Watajitokeza wenye kukabidhiwa dhamana za uongozi, watahujumu uchumi na rasilimali za umma, watazitumiavibaya ofisi za umma wakitarajia kwamba, kubainika kwao kutawafikisha katika kutimuliwa kazi tu, basi!

Lakini serikali katika ngazi tofauti, ikizitumia taasisi zenye mamlaka ya kufanikisha michakato wa kisheria, inapaswa kwenda mbele zaidi ya kushutumu na kufukuza.

Inakuwaje kijana ama yeyote aliye katika ngazi za msingi, akikamatwa (hata) na kuku peke yake, anakuwa mteja wa mahabusu, kisha ndani ya siku chache anaianza safari ‘nenda rudi’ mahakamani. Inawakuwaje iwe heri kwa ‘mijizi mikubwa’ inayoliathiri taifa na watu wake kwa ujumla?

Kucheza na mafisadi ni kulichezea taifa, ni kuchezea uchumi wa nchi, ni kuchezea maendelea na ustawi wa jamii. Kwa nini iwe hivyo.

Kwa maana umma unapovitazama vielelzo kama ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Kamati ya Bunge ya Mazingira, Ardhi na Maliasili…nini kinahitajika zaidi ya hivyo ili uchunguzi ukamilike na wahusike wachukuliwe hatua za kisheria?

Hata mawaziri Dk Kigoda, Balozi Kageshi na Dk Mwakyembe, walipowatimua watendaji walio chini ya wizara zao, haikufanyika hivyo kwa sababu ya ugomvi binafsi.

Walifikia uamuzi huo baada ya wahusika kubainika (pasipo shaka), kwamba walitenda isivyostahili hivyo adhabu peke yake ni kutimuliwa, hata kama ni kwa njia ya kusimamishwa, ili hatua nyingine zifuatwe.

Ukimya unapojitokeza katika kuchukua hatua zaidi za kisheria, umma unavishwa blanketi jeusi usijue kinachoendelea na kubaini ikiwa serikali ina dhamira ya kweli ya kushughulikia ufisadi ndani ya taifa hilo lililojaliwa rasilimali za kutupwa.

Ifike wakati watawala watambue kwamba kufumbia macho waovu na uovu wao kunachochea hasira za wananchi, wanawachukia, wanakosa imani nao, wanazidi kuwapinga na ikibidi kushiriki mikakati ya kuwaondoa madarakani.

Tukiwa taifa huru, watawala wanapaswa kupata ujasiri wa kuchukua hatua kali na za haraka dhidi ya waovu na uovu wao.

Haiwezekani mashauri kama yanayowahusu mafisadi yachukue ‘miaka alfu lela ulela’ wakati yanayohusu kupinga matokeo ya chaguzi za wabunge yanaendeshwa kwa kasi na kufikia suluhu.

Kuna nini?

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +25 754691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment