Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Vitambulisho vya Taifa vyaibua kashfa JWTZ, Polisi

15th May 2012
Print
Comments
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu

Kashfa kubwa ya udanganyifu wa elimu imelikumba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na lile la Polisi nchini, baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kubaini cheti kimoja cha elimu kutumiwa na askari zaidi ya mmoja wa majeshi hayo kama kiambatanisho, kwa ajili ya kuomba kupatiwa Kitambulisho cha Taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya askari wanaotuhumiwa na ufisadi huo wa elimu, 248 ni wa JWTZ na 700 wa Jeshi la Polisi.

Alisema kashfa hiyo ilibainika kwa askari hao katika uhakiki wa fomu za kukusanyia taarifa za waombaji wa kitambulisho hicho.

Maimu alisema zoezi la ujazaji wa fomu hizo, lilianza Januari, mwaka huu, kwa majaribio kwa wafanyakazi wa serikali waliopo jijini Dar es Salaam, visiwani Zanzibar pamoja na majeshi yote, ikiwamo JWTZ, Magereza, Uhamiaji na Polisi nchini kote.

Alisema katika ujazaji wa fomu hizo, hakukuwa na matatizo.

Hata hivyo, alisema zipo changamoto kadhaa zilizojitokeza katika zoezi hilo; ya kwanza ikiwa ni kubaini kasoro katika ujazaji wa fomu hizo na baadhi ya fomu kujazwa mara mbili.

“Ya tatu, vyeti vya elimu kutumiwa na mtu zaidi ya mmoja,” alisema Maimu.

Akijibu swali ni watumishi wa taasisi gani za serikali waliobainika kutumia cheti kimoja cha elimu kwa mtu zaidi ya mmoja, Maimu alijibu “Jeshi la Wananchi watu 248 na polisi watu 700.”

Alisema changamoto ya nne iliyobainika katika zoezi hilo, ni kutokutimia kwa kumbukumbu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukamilisha anuani za makazi na uwezekano wa vitambulisho hivyo kutumiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Nida alisema wamekamilisha hatua zote na wako tayari kuzindua mradi huo na kutoa kitambulisho.

Hata hivyo, alisema zimejitokeza changamoto na mahitaji ya msingi kutoka kwa wadau muhimu wa vitambulisho vya taifa, ambayo hawana budi kuyafanyia kazi ili kitambulisho kikidhi mahitaji yote ya msingi.

Alisema baada ya kushauriana na serikali, wameona ni vyema kusitisha kwa muda uzinduzi huo uliokuwa ufanyike mwezi huu ili mapendekezo ya wadau yaweze kuingia katika mfumo wao.

Maimu alisema hitaji kubwa lililojitokeza ni mfumo wa vitambulisho kutambua na kuingia anuani za makazi na postikodi, kufanya usajili wa pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuwezesha rasimu ya ukusanyaji maoni ya katiba mpya chini ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi ya Mabadiliko ya Katiba.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles