Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wagombea Yanga wamwaga sera

12th July 2012
Print
Comments

Wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mdogo wa Klabu ya Yanga unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, 'wamejinadi' kwa wapiga kura kwa nyakati tofauti na kila mmoja amesema kwamba anataka kuona klabu hiyo inajiendesha kwa kujitegemea badala ya kugetemea ufadhili wa mtu mmoja.

Justin Baruti, mgombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, alisema jana wakati akifanya kampeni kwenye uzinduzi wa tawi la Ubungo Terminal, jijini kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa katika cheo hicho atahakikisha klabu inajiendesha kwa kutumia vitega uchumi vyake na kuacha utegemezi.

Baruti alisema kuwa anataka kuona idadi ya wanachama inaongezeka na kufikia 200,000 ambao ndio watakuwa mtaji 'mkubwa' wa kuipa klabu mapato huku pia atahakikisha umoja na ushirikiano unakuwepo ndani ya Yanga jambo ambalo litachangia mafanikio.

Baruti ambaye aliwahi kuichezea Yanga Kids wakati baba yake akiwa ni Mweka Hazina wa klabu hiyo (Steve Baruti), aliwataka wanachama wa Yanga wasifanye makosa na wamchague yeye kwenye nafasi hiyo.

Mgombea mwingine wa nafasi ya Mwenyekiti, Edgar Chibura, alisema kwamba mbali na kutumia vitega uchumi vyao kama jengo lililopo mtaa wa Mafia, Kariakoo, atahakikisha ubinafsi unakwisha na utawala wa kuheshimu katiba unakuwapo.

"Yanga ina miaka 77 lakini hali ilivyo haiendani na umri huo, nataka uongozi wa uwazi na sio wa kumtegemea mtu mmoja," aliongeza Chibura.

Clement Sanga, ambaye anawania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, alisema amejitosa kuwania nafasi hiyo kwa nia ya kutoa mchango wake kwa klabu anayoipenda tangu utotoni.

"Kwa sasa Yanga haina dira wala mwelekeo. Tunahitaji kuwa na dira na mwelekeo, bila hivyo hatutafika popote," alisema.

Alisema akiingia madarakani kwa kushirikiana na viongozi wenzake mtazamo wake utakuwa ni katika kujenga mfumo wa kudumu katika masuala ya soka la vijana, kuanzisha SACCOS kwa wanachama, kujitegemea na kuleta umoja kwa kuondoa makundi ambapo viongozi wa matawi Tanzania nzima, wazee, vijana na hata vikundi vya ushangiliaji vinatambuliwa kikatiba ili viweze kuendelea kuisaidia klabu kwa utaratibu ulio rasmi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment