Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Majumba ufukweni Dar kubomolewa

16th May 2012
Print
Comments
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka

Serikali imetangaza kwamba nyumba zote zilizojengwa kandokando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992, 1995 na 2004.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, walipozungumza na waandishi wa habari kuelezea migogoro ya ardhi inayotokea nchini na mikakati ya wizara zao kutatua migogoro hiyo.

Prof. Tibaijuka, alisema zoezi la kuwahamisha wakazi waliojenga kandokando ya fukwe za bahari litahusisha mikoa yote iliyopakana na Bahari ya Hindi ambayo ni Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ambazo zinakataza ujenzi wa nyumba kandokando ya fukwe za bahari ndani ya mita 60 pamoja na mita 30 kandokando ya mto.

“Ni lazima tufuate sheria zinazotukataza kujenga kandokando ya fukwe za bahari, kwani hizo ni sehemu maalum kwa watu wote kuzitumia, ingawa kuna nchi zingine zinazoruhusu ujenzi ndani ya bahari, kama vile Dubai,” alisema Prof. Tibaijuka

Aliongeza kuwa kujenga kandokando ya fukwe za bahari na mito ni hatari kwa maisha. “Tumeshuhudia athari zilizotokea pindi tsunami ilipoikumba nchi yetu, pamoja na mafuriko, tunafanya hivyo kwa kuokoa maisha ya watu,” alisema bila kueleza kama nyumba zitakazobomolewa ni za makazi peke yake.

Hata hivyo, alisema nyumba zilizojengwa katika fukwe na kando ya mito kabla ya sheria ya hizo kupitishwa hawataondolewa kwa nguvu badala yake watapewa muda wa kuishi maeneo hayo hadi hati miliki zao zutakapomalizika muda wake.

“Wapo wakazi wenye hati halali wanaofikia 300 ambao walikuwepo kabla ya sheria ya kuwataka watu kutokujenga pembezoni mwa bahari umbali wa mita 60 ya mwaka 1992 ambao watapewa fidia kwa kuwahamisha taratibu na hawatarudishiwa tena hati zao,” alisema Prof. Tibaijuka.

Akizungumzia nyumba zilizojengwa kiholela, alitolea mfano nyumba inayotakiwa kubomolewa eneo la Msomali Mbezi Kawe, jijini Dar es Salaam kwamba imejengwa barabarani na inapaswa kuondoka na wapimaji wa ardhi wamethibitisha hilo.

“Maagizo ya Waziri wa Ardhi ni kwamba eneo lililojengwa nyuma na fensi zivunjwe na upana wa barabara ubakie kwenye hali ya awali ya 10m kama ilivyo kwenye mchoro wa mipango miji,” alisema Prof. Tibaijuka.

Prof. Tibaijuka alisema kwa kushirikiana wizara yake, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mazingira zimeamua kukaa pamoja na kuyatafutia ufumbuzi matatizo na migogoro ya ardhi kwa kuwa matatizo hayo yanazihusu wizara hizo kwa pamoja.

Tibaijuka alionya kuwa kuanzia sasa tabia ya uchakachuaji na utoaji holela wa ujanja ujanja wa viwanja umefikia mwisho wake na nyumba zote ambazo zimejengwa kinyume cha sheria popote pale zitavunjwa.

Aidha, Waziri huyo aliwaasa wananchi wote ambao viwanja vyao vina migogoro kwenda kuripoti polisi mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe, badala ya kuwahusisha maofisa ardhi kwa kuwa wao siyo mahakimu, na kuwaonya maofisa hao kuacha mara moja tabia ya kuingilia migogoro ya ardhi.

“Kama kiwanja chako kimevamiwa, ni vizuri uende polisi na siyo ardhi, na maofisa ardhi waache kuingilia migogoro kwani wao siyo mahakimu,” alisema.

Aidha, Prof. Tibaijuka alieleza kuwa wizara yake ina nia ya dhati ya kutatua na kuipatia ufumbuzi migogoro yote ya ardhi inayotokea nchini, na kuitaja baadhi ya migogoro ambayo wizara yake imeshaitatua.

Aidha, Prof. Tibaijuka aliipatia wiki mbili Shirika la Masoko la Kariakoo kuliendeleza eneo la wazi  linalomiliki lililopo Mbezi Beach, vingenevyo atawanyang’anya na kuwapatia watu wengine waiendeleze sehemu hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, alisema kuwa zoezi la kuwahamisha wakazi waliovamia mito linatarajiwa kuanza hivi karibuni na wataanza na wakazi waliovamia mto Mbezi na Nduwe.

“Setelaiti ya mwaka 2005 inaonyesha mto Ndumbwi ulikuwa unaonekana wazi, lakini sasa wakazi wameuvamia na kujenga kandokando ya mto huo, hata Mto Mbezi Beach pia,” alisema Huvisa.

Alisema kuwa ukaguzi kwa wakazi waliojenga ndani ya mita 30 kutoka kandokando ya mito utafanyika hivi karibuni sambamba na zoezi la kuwabomolea nyumba zao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles