Friday Feb 12, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wasira apanda kizimbani

24th May 2012
Print
Comments
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, amepanda kizimbani kutoa ushahidi kwa tuhuma katika kesi ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa Igunga, Dk. Peter Kafumu (CCM), katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Uchaguzi huo ulifanyika kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo baada ya Rostam Aziz kujiuzuku Julai 13, 2011 akidai kuwa amechoshwa na siasa uchwara, fitima na kuandamwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiwa shahidi wa 20 kwa upande wa walalamikiwa, Waziri Wasira alikanusha tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake, ikiwa ni pamoja na kutoa ahadi ya kugawa mahindi kwa baadhi ya sehemu jimboni humo wakati wa kampeni ili wananchi wakichague CCM.

Akihojiwa na wakili wa upande wa walalamikiwa, Kayaga Kamaliza, kuwa alishiriki vipi katika uchaguzi huo mdogo wa Igunga, Waziri Wasira aliiambia Mahakama kuwa alishiriki kama mpiga kampeni wa chama hicho huku akitaja baadhi ya viongozi alioshiriki nao kuwa ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Mchemba na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde.

Alipoulizwa kwa nini alitumia usafiri wa serikali, Wasira alidai kuwa katika kampeni hizo alikwenda kichama na kwamba kila kifaa alichokitumia Igunga kilikuwa cha chama.

Wakili wa upande wa mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari, alimtaka Waziri Wasira kuieleza Mahakama alikwenda katika kampeni za Igunga kwa cheo gani na alikuwa anajitambulisha kama nani.

Akijibu swali hilo Waziri Wasira alidai kuwa alikwenda Igunga kama kiongozi wa chama akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM na kwamba nafasi yake ya uwaziri hakukabidhiwi kwa mtu yeyote na kwamba alipata ruhusa ya kwenda katika kampeni.

“Uwaziri huwa haukabidhiwi, niriondoka nao, lakini niliomba ruhusa ngazi ya juu na nikapewa ruhusa,” alidai na kuongeza: “Nilikuwa nikitambulishwa kama mjumbe wa Kamati Kuu.”

Waziri Wasira akijibu madai ya kutoa ahadi ya kugawa mahindi katika baadhi ya kata na ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu, aliiambia Mahakama kuwa hakutoa ahadi hizo na kuongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulikuwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya  mwaka 2010.

“Mimi siwezi kugawa mahindi huo ni uongo na ni uzushi kabisa. Pia Chama Cha Mapinduzi hakina mahindi, ni chama cha kisiasa waliotoa ushahidi huo ni waongo sijatoa ahadi yeyote inayohusiana na mahindi,” alidai Wasira.

Profesa Safari alimuuliza Waziri Wasira kama alikutana na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Adeni Rage, katika uchaguzi huo, lakini Wasira alidai kuwa Rage alikuwa akikutana naye katika vikao vya ndani vya tathmini, lakini hakuwahi kukutana naye katika mikutano ya kampeni.

Baada ya kutoa majibu hayo, Profesa Safari alimuuliza Wasira kuwa mbona Rage wakati anatoa ushahidi katika kesi hiyo wiki iliyopita aliiambia Mahakama kuwa 26 Septemba 26, mwaka jana katika kata ya Igulubi walimpokea yeye (Wasira) na kufanya naye mkutano.

Badala yake Wasira alidai kuwa inawezekana mwezekana Rage na wanachama wengine wa CCM walimpokea na wakafanya mkutano.

Kabla ya Wasira kutoa ushahidi wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Igunga ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Protace Magayane, alitoa ushahidi kuhusiana na suala la ahadi ya msaada wa mahindi na suala zima la maadili akiwa mwenyekiti wa maadili ya uchaguzi.

Akijibu kuhusu za ahadi za msaada wa mahindi, Magayane alidai kuwa mahindi hayo yaliyokuwa yakidaiwa kugawiwa yalikuwa ni ya msaada wa serikali.

Aliiambia Mahakama kuwa mahindi hayo yalianza kutolewa katika maeneo yaliyokuwa na njaa tangu Aprili, mwaka jana kabla ya uchaguzi huo.

Kuhusu hoja ya maadili, Magayane alidai kuwa alipokea malalamiko kadhaa kutoka katika vyama vya siasa na kwamba wakati huo huo alikuwa akifanya mikutano ya mara kwa mara na vyama ili kutatua kero hizo.

Profesa Safari alipomhoji Magayane kuhusiana na ujio wa mawaziri katika kampeni hizo, alikana kupata taarifa hizo na kudai kuwa alikuwa akisikia kuwa watu hao wapo, lakini hakuwahi kuwaona.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mary Shangali, imeahirishwa hadi Juni 13, mwaka huu huku mashahidi 20 wa upande wa walalamikiwa wakiwa tayari wametoa ushahidi wao.

Shahidi muhimu wa upande wa walalamikiwa, Dk. John Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi,  bado hajatoa ushahidi huku upande wa mlalamikaji ukiwa umeandaa mashahidi 20, wakiwemo kumi wa serikali.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, akilalamika kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki kwa kuwa taratibu nyingi zilikiukwa. Anawalalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa Uchaguzi na Dk. Kafumu.

Katika uchaguzi huo, Dk. Kafumu alipata kura 26,434 dhidi ya mpinzani  Kashindye aliyepata kura 23,260.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment