Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Waziri Magufuli aagiza RFB kuchunguze matumizi ya fedha

31st July 2012
Print
Comments
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema fedha za Mfuko  wa Bodi ya Barabara (RFB) zimekuwa zikitumika vibaya kama kulipia malipo ya shughuli za Mbio za Mwenge, mtihani wa kidato cha nne na na posho za vikao na ametaka Bodi hiyo, kuchunguza matumizi hayo na kuwachukulia hatua haraka watumishi waliohusika.

“Bodi ya Mfuko wa Barabara iendelee kuchunguza matumizi ya fedha hizi pamoja na kupitia ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua haraka ikiwa ni pamoja na kuleta taarifa za wahusika mapema ili serikali ichukue hatua,” alisema Dk. Magufuli wakati akifungua mkutano wa wadau wakuu wa Mfuko wa Barabara uliofanyika jijini hapa jana.

Aidha, aliwataka makatibu wakuu wa Wizara ya Ujenzi, Tamisemi, makatibu tawala wa mikoa, mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na  taasisi zote zinazohusiana na barabara kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote wanaohusika na matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Barabara kinyume na sheria iliyoanzisha mfumo huo.

Alitaja baadhi ya mifano mibaya ya matumizi ya fedha za Mfuko wa Barabara katika halmashauri nchini kama matumizi nje ya utaratibu na yenye mashaka kama vile ulipwaji mara mbili kwa mkandarasi kwa kazi moja uliofanywa katika Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma.

Nyingine alisema ni malipo yasiyostahili yaliyofanywa na halmashauri za Morogoro, Chato, Kishapu, Mtwara, Kigoma, Biharamulo, Bukoba, Muleba na Misenyi ambazo zilitumia fedha katika kulipana posho, malipo ya mafuta kwa magari yasiyohusiana na shughuli za barabara, malipo ya ujenzi wa nyumba ya kuishi mkurugenzi (Kishapu), posho za kuhudhuria
mafunzo na semina, malipo  zaidi ya stahiki ya mkandarasi na  malipo ya matengenezo ya magari.

Alitaja mifano mingine kuwa ni Manispaa za Morogoro, Musoma, Halmashauri za Wilaya ya Mafia, Mwanga, Geita, Chato, Kibondo, Bariadi, Tarime kuwa zilitumia fedha za mfuko huo kwa malipo ya shughuli za Mbio za Mwenge, kulipia malipo ya mitihani wa kidato cha nne, malipo ya ununuzi wa vifaa kwa miradi isiyohusiana na barabara, malipo kwa ajili ya kuchimba shimo la takataka (Chato), malipo kwa mkandarasi bila kutangaza tenda na malipo kwa posho za kujikimu.

Pia alisema kumekuwa na utendaji kazi ulio chini ya viwango hali ambayo inachangia matumizi mabaya ya fedha kama ambavyo imetokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ambapo ujenzi wa daraja eneo la Kigwe-Ngulugano na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuzidisha stahiki kwa mkandarasi.

Alisema kutokana na umuhimu wa barabara katika kujenga uchumi endelevu na kupunguza umaskini nchini, Bodi ya Mfuko wa Barabara kama sehemu ya serikali ina jukumu kubwa la kuzimamia kikamilifu taasisi zinazotumia fedha za Mfuko bila woga.





 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment