Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Mabomu Yarindima Mtwara
Polisi mkoani Mtwara leo wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kudhibiti wanainchi wanaoandamana kupinga uamuzi wa serikali wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara.

Wassira anapowadhalilisha binti wa uzao wake!

7th October 2012
Print
Comments
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira

Septemba 30 mwaka huu, siasa za Tanzania zilishuhudia wasichana kutoka familia ya akina Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wakijiunga katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wasichana hao wasomi, Esther Wassira na Lilian Wassira, walifikia hatua hiyo inayotambulika kwa mujibu wa haki za binadamu na misingi ya demokrasia, na kukabidhiwa kadi na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa.

Sijadili tofauti zilizojitokeza, iliporipotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, wakiwataja Esther na Lilian kuwa watoto wa Stephen Wassira, mwanasiasa aliyewahi kujulikana kwa jina la Tyson, ingawa hakutaka na hataki kuitwa hivyo. Na mimi simuiti hivyo!

Sitaki nijadili kwa kulihusisha tukio hilo na mambo ya kifamilia ndani ya uko wa akina Wassira, kwa maana kila mtu ana haki isiyoathiriwa na matamanio ya watangulizi wao katika nyanja ya siasa.

Lakini lipo jambo moja ambalo ninalazimika kulizungumzia, ili kuweka kumbukumbu na kutoa mwelekeo stahili kwa wazazi ambao upande mwingine, wana dhamana za uongozi kama Stephen Wassira.

Kwa vile tangu kuripotiwa kwa taarifa za Esther na Lilian, Stephen Wassira hajalikanusha, kwamba katika kujenga hoja baada ya wasichana hao kujiunga Chadema, akasema:-

"Kwani ukiwa baba mdogo unafuatilia vyama, sina habari zao kama wamejiunga na Chadema kuna tatizo gani, wameshasomeshwa ni wakubwa ... siwezi kujua labda wanaume zao wapo Chadema sasa nitawazuiaje wasijiunge nao," alisema Wassira.

Hapo ndipo hoja yangu ya msingi inaposimama, kwamba Stephen Wassira, alifikiria nini hata kufikia hatua ya kuwadhalilisha Esther na Lilian, kwa kuwahusisha na ‘kuwafuata wanaume zao Chadema’ hata pale wanapotimiza matamanio yanayogusa haki zao za msingi?

Nilipofuatilia mjadala kuhusu tukio hilo, sikuona maana ya kuzungumzia zaidi kuhusu Esther na Lilian kutokuwa ‘watoto wa kuzaa’ wa Stephen Wassira.

Badala yake mwanasiasa huyo alipaswa kujisafisha kwa `kauli chafu’ yenye kudhalilisha, dhidi Esther na Lilian ambao ni watoto wa kaka yake, George Wassira.

Kutamka kwamba wasichana hao ‘huenda’ wamewafuata wanaume zao, hakutoi taswira chanya kwa Stephen Wassira kuwa baba, mlezi na kiongozi mwema, bali Yule asiyejua vizuri majukumu yake na namna bora ya kuyatekeleza.

Kumhusisha mtoto wa kike na ‘mambo ya wanaume’ kwa tafsiri rahisi ni kuitaka jamii iamini kwamba msichana mhusika ni kihelehele, hana adabu, hayaishi maadili mema, hafai mbele ya umma wa wastaarabu.

Kumhusisha mtoto wa kike na ‘mambo ya wanaume’ kunatoa maana na kumfanya msichana mhusika aonekana kuwa miongoni mwa ambao hawakupata malezi bora.

Kwamba tangu kwenye familia ya baba, mama, kaka, dada na ndugu wengine, msichana mhusika ‘hakufundwa’, hivyo wanaume kwake ni jambo lenye maana pana kuliko kitu chochote!

Inapotolewa kauli kama alivyokaririwa Stephen Wassira, ninapata wasiwasi kuhusu mahali walipojificha wanaharakati wa haki za jinsia hususani wanaowatetea wasichana na wanawake. Wako wapi?

Pamoja na ukweli kwamba kwa kuwadhalilisha Esther na Lilian, Stephen Wassira amejionyesha mbele ya umma kuwa miongoni mwa wasiodhibiti ndimi zao dhidi ya kuwachafua watu wasiokuwa na hatia, lakini ‘mbaya’ zaidi wakitokana na uzao wake!

Watoto ni watu wa kuheshimiwa sana ndani ya familia, ukoo na taifa. Watoto wanajifunza kutoka kwa wazazi, walezi na wakubwa zao, ingawa inawezekana pia kuwa miongoni mwao.

Anapotokea kiongozi kama Stephen Wassira kuwahusisha Esther na Lilian na ‘mambo ya wanaume’, kizazi kilicho chini ya umri wake (Wassira), kijifunze nini?

Tena pale ambapo anaweka wazi na kuthibitisha kuwa Esther na Lilian ni watoto wa kaka yake, wakiwa na haki zote za kumuita baba, tena baba mwema wa familia, lakini yeye anawahusisha na ‘mambo ya wanaume’. Fedheha isiyovumilika!

Hivi Esther na Lilian, wangezungumza wakati Stephen Wassira akitoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiunga NCCR-Mageuzi, wakasema ‘amefuata mabibi zake’, hali ingekuwaje?

Esther na Lilian wangeadhibiwa vipi na familia, ukoo, jumuiya na taifa kwa jumla? Kwa maana wangeonekana hawana adabu, hawana heshima, watukutuku na wakorofi.

Ama alipotoka NCCR-Mageuzi na kurejea CCM, Esther na Lilian wangehusisha kitendo hicho cha Stephen Wassira na ‘mambo ya wanawake’, hivi sasa wangekuwa katika hali gani? Wangetazamwa vipi na umma?

Sasa inakuwaje mkuki kwa nguruwe, kwa mwanadamu mchungu? Ama ni nani atawasafisha wasichana hao ambao kimsingi hawakuvunja sheria, hawakufanya kosa la jinai, bali kunuifa na uhuru wao ndani ya Tanzania huru?

Poleni sana Esther na Lilian. Wapo wenye akili timamu ndani na nje ya ukoo wenu, wakitambua thamani mliyonayo.

Ninyi ni mfano wa mchanga unaotofautiana na tope la udongo, kwa maana mmetimiza yaliyozigusa nafsi zenu, mtafanikiwa.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255754691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment