Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Manispaa Kinondoni haikutumia busara `bomoabomoa` Hananasif!

7th October 2012
Print
Comments

Ijumaa wiki hii ilikuwa ni siku chungu kwa kaya zaidi ya 100 zilizokuwa zikiishi katika Mtaa wa Mkunguni ‘B’, eneo la Hananasif, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Hiyo ni baada ya kaya hizo kupoteza makazi katika mazingira yaliyomsikitisha na kumhuzunisha kila mwenye japo chembe ya huruma kwa binadamu mwenzake.

Kaya hizo zilikumbwa na masaibu hayo baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kubomolewa na watu waliodaiwa kutumwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufanya hivyo.

Mbali na nyumba zao kubomolewa, pia mali mbalimbali za wananchi hao zenye thamani ya mamilioni ya shilingi ziliharibiwa na nyingine kuporwa katika ‘operesheni’ hiyo.

‘Bomoabomoa’ hiyo ni mwendelezo wa operesheni ya kuondoa nyumba zilizojengwa katika maeneo yasiyostahili. Kwamba, zinadaiwa kujengwa katika makazi holela na kwenye ardhi oevu.

Jijini Dar es Salaam, operesheni hiyo ilianza Julai 11, mwaka huu, ambapo kati ya nyumba 27, nyumba 15 zikiwa zimekamilika ujenzi, nane uzio na nyingine katika hatua za awali za ujenzi, zilizokuwa kando ya mito ya Mbezi Beach, Mndumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko, zote zilibomolewa.

Nyumba zilizobomolewa Hananasif, ni miongoni mwa nyumba zilizowahi kuainishwa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, Julai, mwaka huu, kwamba, ziko kando ya mto Msimbazi. Hivyo, zingeingia katika mpango wa kubomolewa.

Nyumba nyingine zilizoko kando ya mto huo, kuanzia eneo la Gongo la Mboto, Kigogo, Msimbazi na Jangwani, nazo pia zilitajwa na DC Rugimbana kuwa ni katika orodha ya nyumba zitakazokumbwa na ‘bomoabomoa’ hiyo.

Rugimbana alikaririwa akisema tathmini imeshafanyika na wakazi wa maeneo watapewa viwanja katika eneo la Mabwepande, lakini hawatalipwa fidia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Fotunatus Fwema, nyumba 5,000 ndizo zitakazobomolewa katika manispaa yake.

Aidha, Mei 25, mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Gaudence Nyamwihura, alikieleza kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba, zaidi ya nyumba 2,000 zilizojengwa kando kando ya mto huo, zingebomolewa.

Nyamwihura alisema nyumba hizo zingebomolewa ili kupisha upanuzi wa mto huo. Lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi hawakumbwi tena na mafuriko.

Kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Terezya Huvisa, naye pia alikaririwa akisema serikali ingetekeleza mpango wake wa kubomoa nyumba 10 zilizojengwa katika maeneo yasiyostahili wilayani humo.

Huvisa alisema nyumba hizo ni zile zilizojengwa katika maeneo ya kandokando ya mito iliyopo maeneo ya Mbezi Beach na Kawe, ambazo alisema zinasababisha maji kutuama.

Pamoja na nia nzuri iliyonayo serikali katika ‘bomoabomoa hiyo, kuna upungufu mkubwa unaoikabili operesheni hiyo kiasi cha kuifanya ionekane kuwa ni ya kiharamia!

Kutokutumika kwa busara katika utekelezaji wake, ndiyo msingi unaofanya operesheni hiyo ionekane hivyo.

Watu waliotumwa na manispaa kubomoa nyumba hizo, wametekeleza operesheni hiyo kihuni.

Wamiliki wa nyumba hawakupewa taarifa lini operesheni itafanyika. Pili, viongozi; kama vile wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani, ambao ndiyo watu walio karibu zaidi na wananchi hakupewa taarifa.

Ile nidhamu ya kutambua kwamba, jambo lolote linalohusu jamii hata kama imekosea, mawasiliano lazima yafanyike, haikuwapo kabisa.

Badala yake, kinachofanywa na watu hao, ambao hawavai hata sare ili kuwatambulisha, huvamia eneo mithili ya majambazi na kuanza kubomoa nyumba.

Uthibitisho wa hilo ni kauli iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Hananasif, Abbas Tarimba, muda mfupi, baada ya wakazi wa Hananasif kuvamiwa na watu hao na kubomolewa nyumba zao.

Tarimba, mbali ya kuwapa pole waliofikwa na masaibu hayo, alikaririwa akisema ni jambo la kusikitisha watu hao kubomolewa nyumba zao.

Alisema hakutarajia kama manispaa ingeweza kufanya hivyo kwa sababu kama viongozi na wawakilishi wa wananchi hawakufahamishwa wala kuonyeshwa mahali, ambako wananchi waliobomolewa wangekwenda kuishi.

Hawajali kama athari ya ‘bomoabomoa’ inakwenda mbali zaidi. Hawajali kama athari hizo zinaweza kuwapata wasiohusika zinazotokana na utekelezaji wa operesheni hiyo kihuni.

Hawajali kama ndani ya nyumba inayobomolewa na nyumba nyingine ya jirani isiyohusika kunaweza kuwa na vichanga, vikongwe na wagonjwa ukiachilia mbali mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zinazoweza kuwamo.

Hawajali kama kunaweza kukawa na nyumba jirani ya nyumba zinazobomolewa, kama vile shule, ambako kuna watoto wanaendelea na masomo.

Hawajali vumbi linaloruka na kusambaa kutokana na nyumba kubomolewa linaweza kusababisha vichanga, wazee, vikongwe na watoto kuumia.

Kwa jumla, hawajali kama kwa kuendesha kwao operesheni kihuni kunaweza kuleta madhara makubwa kiafya kwa watu niliowagusia hapo juu.

Pia hawajali kama kunaweza kuleta pia madhara ya kiuchumi kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao.

Kwa hakika, inasikitisha na kuhuzunisha! Inasikitisha kwa sababu utaratibu unaotumika kubomoa nyumba hizo hauongozwi japo na busara tu ya kuzaliwa.

Kubwa linalosikitisha ni kitendo cha askari polisi kumkamata na kumfunga pingu mmoja wa watu waliobomolewa nyumba yake, Bakari Issa, baada ya kulalamika kuwa ameibiwa vitu vyake na wabomoaji.

Kwa ufupi, utaratibu wa ‘bomoabomoa’ hiyo una matatizo! Hauna tofauti na mtu anayetaka kumchinja kuku ili apate nyama, lakini haangalii kama kuku yule ana vifaranga! Ni busara tu hapo ndiyo inayohitajika.

Ni kweli watu walishapewa viwanja. Lakini ndiyo uwaondoe kwa kuwavamia?

Jiweke wewe leo. Kwamba, umerudi nyumbani kutoka katika shughuli zako za kujitafutia riziki, halafu unakuta watoto wako wapo nje. Utajihisi vipi?

Kama hoja ni kwamba, viwanja vimeshatolewa kwa watakaobomolewa, bado kuna maswali.

Mosi, je, huduma muhimu za kijamii zimewekwa katika maeneo viliko viwanja hivyo? Pili, je, viwanja hivyo vimepimwa?

Tatu, inafahamika kuwa katika kuhama kuna usumbufu. Je, wanaohamishwa kutoka Hananasif kwenda Mabwepande wamewezeshwa kiasi gani kuhama?

Maswali hayo yakitafakariwa, yafaa utaratibu ukafanyika katika kuwahamisha waliojenga katika makazi holela.

Kwani wengi wao wamefika hapo kutokana na uzembe uliofanywa na baadhi ya maofisa ardhi, watendaji wa manispaa na halmashauri za miji.

Itolewe elimu endelevu kuhusu uendelezaji wa makazi ili wananchi wajue madhara ya kuishi katika makazi holela. Kwani kuna watu wamezaliwa mabondeni. Hawajui ubaya wa kuishi mabondeni.

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment