


Taifa lipo katika hali tete, nuru ya thamani ya amani inatoweka, haki na usawa vinapotea, ni vurugu tupu!
Umma unapaza sauti ukilia, unapaza sauti ukipendekeza njia mbadala za kuifanya Tanzania iwe mahali pazuri pa kuishi, wenye dhamana ya kutufikisha hapo, hawaisikii sauti hiyo.
Uovu umelelewa katika ngazi tofauti, maovu yanafanywa na watekelezaji na walio watetezi wa uovu, wale ambao mustakabali chanya wa nchi na watu wake si sehemu ya matamanio yao, wanaangaliwa, wanaachwa wanatamba!
Kwa muda mrefu sasa, kimekuwepo kilio cha kuuawa kwa raia wasiokuwa na hatia. Wakishambuliwa na vyombo vya dola hususani askari polisi.
Wakijeruhiwa na askari wa idara nyingine, ili mradi kukidhi matakwa ya kikundi cha watu wachache na si kwa maslahi ya nchi na watu wake.
Kilio cha umma kimekuwa kuwaomba watawala, wafanikishe kupunguza matukio yenye nia ovu, yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, zaidi yakifanywa na askari polisi.
Lakini kwa kile kinachotafsiriwa kama ‘kiburi cha madaraka’, mwangwi wa kilio hicho ni kama unapitia sikio la kushoto, ukatokoea lile la kulia. Hakuna kinachofanyika!
Tatizo la kijamii halipo katika mauaji ya raia yanayofanywa na askari polisi, yakiwemo ya hivi karibuni, yakimhusisha aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa kituo cha runinga cha Channel 10, David Mwangosi. Mwenyezi azidi kumpumzisha kwa amani-AMINA!
Yapo matukio yanayohusiaana na rushwa na aina nyingine za ufisadi, yakifanyika kwa mtazamo kwamba yanaiathiri jamii ya watu wenye hali duni kiuchumi.
Kwamba kutokana na kushamiri kwa rushwa na ufisadi, raia wa kawaida wanakosa huduma bora za jamii. Ni kweli, hali ipo hivyo.
Lakini hivi sasa ambapo watawala kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanashiriki chaguzi za ndani, athari zinazotokana na rushwa na ufisadi zimeibuka katikakati yao.
Kuanzia mwanachama wa ngazi ya chini hadi waliowahi kuwa viongozi waandamizi serikali, wameathirika kutokana rushwa na ufisadi.
Wameathirika kwa maana uovu huo umepindisha uamuzi sahihi wa wanachama wao, kuwapigia kura na kuwachagua waendelee kukiongoza ama kushiriki vikao muhimu vya maamuzi ndani ya CCM.
Kwa maana rahisi, athari za rushwa na ufisadi zimetoka katika taswira ya kuamuathiri raia wa kawaida, na kuwafikia ‘wakubwa’. Sasa wanalalamika.
Mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Tluway Sumaye, ambaye ‘piga ua galagaza’, hataonekana katika vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM.
Ameshapaza sauti akilalamikia rushwa na ufisadi mwingine, kwamba vimejikita katika umbo la mtandao ulioenea nchi nzima, ukilenga kuwaingiza madarakani wasiostahili kuliongoza taifa hili.
Hata tukiangalia sakata la sauti ya wanyonge dhidi ya mauaji yanayofanywa na askari polisi kwa upande mmoja na majambazi kwa upande mwingine, hali ipo kama hivyo.
Kwamba tathmini mbalimbali zimeonyesha udhaifu katika mpangilio wa ulinzi wa watu na mali zao.
Haki ya watu kuishi imekuwa ikiondolewa kwa njia ya mauaji. Machozi yametiririka kwenye nyuso za wapendwa ndugu waliouawa, mwishoni yakakauka.
Salaam za pole zikatolewa kwa nyakati tofauti, miili ya waliouawa ikalazwa makaburini, japo si kwa mapenzi ya Mungu, bali uzembe wa kibinadamu.
Wakati jeshi la polisi likielekezewa kidole, Taifa linakumbwa na simanzi baada ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) mkoani Mwanza, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Barlow, kuuawa. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi-AMINA!
Binafsi niliwahi kukutana na Barlow wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Tarime mwaka 2008, baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Chacha Zakayo Wangwe.
Kama walivyo askari polisi wengine, Barlow akiwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, alifanya kazi kubwa kuhakikisha amani na usalama vinadumu, hata uchaguzi huo ukamalizika pasipo madhara makubwa kwa binadamu.
Inapofikia hatua ya RPC anauawa ‘kirahisi’ kama inavyoripotiwa kwa Barlow, lazima kama taifa lijiulize, tunaelekea wapi? Kwa maana si tukio la kawaida.
Lakini kama nilivyoeleza awali, Tanzania inakabiliwa na ‘ka-ugonjwa’ kwa watu kufikiri kwamba uovu unawafika raia wa kawaida, haupenyi katikati ya walio wakuu. Ni upotofu.
Imeshaonekana, Waziri Mkuu mstaafu analalamikia rushwa kwa kadri ilivyomuathiri. Wapo ‘vigogo’ wanaolalamika hivyo.
Kamanda wa Polisi anayetekeleza jukumu la kuwalinda raia na mali zao, anauawa ‘kirahisi’. Tuone ni mambo ya kawaida? Haiwezekani. Kuna tatizo.
Kuna tatizo linalolelewa, licha ya athari zake kujulikana dhahiri, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa, sehemu ya matokeo yake ndio hayo.
Kuijenga jamii inayoyaona matukio kama rushwa, ufisadi na mauaji ni mambo ya kawaida, yanaweza kutokea mahali popote, wakati wowote na kwa yeyote, ni hatari kubwa.
Ni hatari inayolifanya taifa lisijue sekunde moja ijayo, kuna jambo gani litatokea, na nani atakayelitekeleza.
Lakini kama wenye dhamana ya utawala wakiweka mfumo unaikinga jamii dhidi ya uovu na watenda maovu hayo, ni dhahiri kwamba kizazi cha Tanzania kitaifurahia haki, kitapata amani na kuiona ardhi ya Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi.
Kuyadharau matukio ovu kwa namna yoyote, kutoguswa na matokeo yake, ni sawa na mkulima wa mahindi anayemcehekea nyani, kwani mwisho wake anaambulia kuvuna mabua.
Tusifike huko!
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia namba +2755754691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com