


Dira ya Mabadiliko, ambayo kwa kifupi “V4C”, ni kauli mbiu iliyoasisiwa na Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 2008 ikiwa ni nyenzo mahsusi wa kukiongoza chama hicho katika kufikia malengo yake ya kisiasa nchini.
Iliiweka rasmi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kuinadi katika kampeni zake za uchaguzi huo, uliofanyika katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais nchini kote.
Septemba 16, mwaka huu, CUF ilifanya matembezi ya hisani na kuchangisha zaidi ya Sh. milioni 129 kutoka kwa wananchi, huku Sh. milioni 325 zikitajwa kama ahadi.
Matembezi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alichangia Sh. 110,000.
Michango hiyo ililenga kufanikisha operesheni ya CUF iliyozinduliwa na uongozi wa chama hicho taifa, jijini Dar es Salaam, Septemba, mwaka huu, ijulikanayo kama “Mchakamchaka wa Dira ya Mabadiliko (V4C) nchini hadi mwaka 2015”.
CUF ilianza zoezi hilo kwa maandamano ya amani, yaliyoanzia makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam. Yaliongozwa na Profesa Lipumba.
Maandamano hayo yalianza saa 4:30 asubuhi.Yalipita katika Barabara za Uhuru, Kariakoo, Morogoro na kuhitimishwa kwenye viwanja vya Jangwani majira ya saa 5:33 asubuhi.
Hatua ya CUF kuchangisha fedha kwa ajili ya Mchakamchaka V4C mpaka 2015 ilifananishwa na kile kilichofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Chadema iliwahi kuchangisha wafuasi wake fedha kwa ajili ya mikutano yao ya Vuguvugu la Mabadiliko linaloitwa kwa kifupi “M4C”.
Operesheni Mchakamchaka V4C mpaka 2015 ya inayoendeshwa na CUF, inalenga kutekeleza shughuli mbalimbali za CUF, ikiwamo ufunguzi wa matawi.
Pia kupokea wanachama wapya, viongozi kuhutubia mikutano ya hadhara mijini na vijijini kueleza sera za chama hicho.
Vilevile, kuandaa na kufanya mikutano ya ndani kwa lengo la kujadili na kupanga mikakati ya kuimarisha nguvu za chama na kufikia malengo yake ya kisiasa ya kushika hatamu za dola.
Pamoja na mambo mengine, uzinduzi wa operesheni hiyo ulikumbana na changamoto.
Changamoto mojawapo ni kejeli iliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kejeli hiyo ilitolewa na Chadema kupitia Mkurugenzi wake wa Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, katika mkutano na waandishi aliouitisha jijini Dar es Salaam, Septemba 17, mwaka huu.
Mtemelwa katika mkutano na wanahabari alidai kuwa CUF haina uwezo wa kuendesha Operesheni ya Dira ya Mabadiliko (V4C) nchini kote.
Hata hivyo, kauli hiyo ya kejeli hiyo ya Chadema ilipuuzwa na CUF baada ya kuacha kuijibu, badala yake iliendelea kuandaa operesheni hiyo.
Utekelezaji wa operesheni ya ‘Mchakamchaka V4C mpaka 2015’, ulianzia mkoani Arusha mwanzoni mwa mwezi huu.
Viongozi wakuu wa CUF ngazi ya taifa, akiwamo Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba, na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, walihutubia mikutano mbalimbali ya hadhara.
Mbali na Profesa Lipumba na Maalim Seif, viongozi wengine waliohudhuria na kuhutubia katika mikutano hiyo, ni Makamu Mwenyekiti, Machano Khamis Ali, na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Julius Mtatiro.
Katika mkutano wa hadhara wa operesheni hiyo, uliofanyika katika viwanja vya Levolosi, jijini Arusha, Profesa Lipumba, alihutubia na kusema Tanzania inahitaji kuwa na viongozi wenye dira watakaoweza kuzitumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, zikiwamo jiografia yake, bahari na madini, ambazo alisema bado hazijatumika vizuri kuwanufaisha Watanzania wanaoendelea kuishi katika hali ngumu ya kiuchumi.
“Tunahitaji viongozi wenye dira watakaoweza kuzisimamia rasilimali za Watanzania kwa maslahi ya Watanzania wenyewe”, alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Watanzania tumeshindwa kuzitumia rasilimali tulizonazo kwa maendeleo yetu. Tunayo mazao mengi ya mboga mboga. Tunayo madini mengi, bandari na kadhalika, ambazo zote hizi zikitumika vizuri, tunaweza kujikwamua kiuchumi.”
Alisema Watanzania wanahitaji kujipanga kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na maendeleo ya teknolojia.
Profesa Lipumba alisema iwapo kutakuwa na mipango imara, kila Mtanzania anaweza kunufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi.
Alitaja utajiri mwingine unaoizunguka Tanzania kuwa ni pamoja na vivutio vya utalii, ikiwamo milima mikubwa, kama vile Kilimanjaro na Meru, visiwa vya Zanzibar pamoja na rasilimali za mafuta na gesi.
Mkutano huo ulihutubiwa na Maalim Seif, ambaye aliwakebehi wanaobeza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar.
Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), alisema maridhiano hayo yalikuwa ni maamuzi ya Wazanzibari wenyewe, hivyo haifai kuyabeza.
Alisema maridhiano hayo yaliyosababisha kuundwa kwa SUK, yameifanya Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
“CUF ina malengo ya kuwaunganisha Watanzania wote na ni chemchem ya amani, siyo kama vingine hivi vyenye sera za kuripua mabomu na siasa za kibaguzi,” alisema Maalim Seif na kuongeza:
“Siasa si lelemama wala si vurugu, bali viongozi wa kisiasa wanatakiwa washindane kwa hoja siyo kuwabagua wananchi kwa misingi ya udini na ukabila, na wajue kuwa hili linavuruga umoja wa kitaifa.”
Aliwashukuru wananchi wa Arusha kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo, na kusema kuanzia sasa CUF itajikita katika mkoa huo kuhakikisha kuwa inawakomboa wananchi wa eneo hilo.
“Nasema hakuna mtu wala chama chenye hatimiliki ya mkoa huu, bali mkoa huu ni wa wananchi wote wa Arusha. Na kuanzia sasa tutajikita kisiasa katika mkoa huu hadi kieleweke,” alisema Maalim Seif.
Aliwataka wananchi wa Arusha kuwa makini na propaganda zinazoenezwa dhidi ya CUF kuwa ni chama cha Kiislamu na Waarabu.
Alisema propaganda hizo zina lengo la kuwagawa Watanzania badala ya kuwaunganisha.
Katibu wa CUF Wilaya ya Arusha, Hassan Zakaria Zani, alisema wananchi wa Arusha wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na siasa za vurugu.
Katika mkutano huo, Profesa Lipumba alimkabidha kadi ya CUF aliyekuwa Diwani wa Chadema Kata ya Ererai, mkoani Arusha, John Bayo.
Bayo aliihama Chadema pamoja na wanachama wengine kutoka chama hicho na wengine kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Profesa Lipumba pia alikabidhi kadi kwa wanachama wapya walioamua kujiunga na CUF.
Changamoto nyingine, ambayo operesheni hiyo ilikumbana nayo, ni mkutano na msafara wa viongozi wa CUF kurushiwa na baadhi ya watu, waliosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema.
Tuhuma hizo zilikanushwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ambaye alikaririwa akisema kuwa wafuasi wa chama chake hawakuhusika na kuwashambulia CUF kwa mawe, mkoani Arusha.
‘Mchakamchaka V4C mpaka 2015 iliendelea mkoani Kagera mwezi huu, ikiongozwa na Profesa Lipumba, akiandamana na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali wa chama hicho.
Walitembelea katika vijiji kadhaa na miji ya wilaya zote za mkoa huo, ambako kote huko walipata fursa ya kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Operesheni hiyo iliendelea Jumapili wiki iliyopita, katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Maalim Seif, ambaye alisema tatizo la ajira kwa vijana linashindwa kupatiwa ufumbuzi kutokana na kutokuwapo kwa sera na mipango thabiti ya kusaidia kundi hilo.
Katika mkutano huo, uliofanyika eneo la Buguruni Sheli, jijini Dar es Salaam, zaidi ya wanachama 20, ambao walijiondoa CUF na kujiunga na chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) walirejea CUF.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili wiki iliyopita, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema operesheni hiyo inatarajiwa kuendelea mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki hii.