


Shirikisho la Wenye Mahoteli (HAT), limepata fedha kutoka asasi ya Uboreshaji wa Mazingira ya Kibiashara Kitengo cha ushawishi ( (Best-AC) kufanya utafiti wa miezi miwili kuhusu athari za kisheria na uchumi kwa utoaji wa leseni za utalii hapa nchini.
“Ni muhimu kutazama upya namna ya utoaji leseni ili kuwawezesha wajasiriamali wengine washiriki kikamilifu katika kuboresha sekta ya utalii nchini," alisema Mwenyekiti Shirikisho la wenye Mahoteli, Damasi Mfugale.
Alisema ada za leseni ni kubwa mno kwa wananchi wengi wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika kukuza sekta hiyo.
Leseni za utalii Tanzania hutolewa na Bodi ya Leseni za Utalii (TTLB) ambayo zamani ilikuwa inajulikana kama wakala wa utoaji leseni za utalii Tanzania (Tala).
Ili kufanikisha kazi hiyo, HAT imewateua washauri wawili, mwanasheria na mchumi ili kuangalia mambo mbalimbali ikiwamo ya ulinganifu na yanayofanyika katika nchi za Kenya, Uganda, Botswana na Mauritius kuhusiana na masuala ya leseni na kuangalia ni kwa namna gani muundo wa leseni wa sasa unaisaidia Tanzania.
Mwanaharakati na mshauri wa masuala ya sheria ya makampuni, Dk. Eve Hawa Sinare, ataangalia masuala ya kisheria, historia yake, mantiki yake na inavyojitosheleza.
Atakayeshughulikia masuala ya uchumi ni Malcolm Toland.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa HAT , Lidwien Appels, alisema suala la utoaji leseni la TTLB linahitaji kuangaliwa kwa makini na watoa maamuzi na hivyo kuwapo na haja ya kufanya utafiti kujua athari zake kisheria na kiuchumi.