Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Anayetuhumiwa kubaka mtoto afariki ghafla

28th April 2012
Print
Comments
  Kesi ilikuwa ianze jana akaanguka chooni

Mtuhumiwa anayedaiwa kuwa na virusi vya Ukimwi aliyekuwa akikabiliwa na  kesi ya ubakaji wa mtoto wa miaka 11 ambaye kesi yake ilikuwa ianze kusilizwa jana kwa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka chooni.

Mtuhumiwa huyo Abdallah Makonta (50) maarufu kama Mpemba, alikuwa anakabiliwa na shitaka hilo lililoripotiwa polisi Oktoba, mwaka jana.

NIPASHE iliyokuwa katika utafiti wa masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), ambayo pia ilikuwa inafuatilia suala hilo ilipigiwa simu na walezi wa mtoto huyo na kujulishwa kuhusu kifo cha mtuhumiwa huyo.

Taarifa hizo pia zilizithibitishwa na Afisa Ustawi Jamii wa Wilaya ya Same, Johnson Mndeme, ambaye kesi hiyo ilianzia mikononi mwake.

“Ni kweli amefariki dunia jana (juzi) na hivi sasa watu wamekusanyika nyumbani kwake kushuhudia tukio hilo,” alisema Mndeme.

Juhudi za kumpata msemaji wa polisi juu ya tukio hilo, hazikuzaa matunda baada ya kutafutwa kwenye simu ya mkononi bila mafanikio.

Matukio ya ubakaji na watoto wa shule kukatishwa masomo kwa kupewa mimba ni kati ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro ambapo matukio 68 yameripotiwa polisi hadi kufikia Machi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Same, kesi 59 zilikuwa zimeripotiwa katika kituo hicho kuanzia Januari hadi Desemba, 2011.

Uchunguzi wa NIPASHE Jumamosi umebaini kuwa kesi hizo nyingi ni za watoto walio chini ya umri wa miaka 18, ambao hubakwa na wengine kukatishwa masomo kutokana na kupewa mimba.

Kesi 23 kati ya hizo ni za watoto kubakwa ambapo 15 zimefikishwa mahakamani na kuanza kusikilizwa.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, kesi tisa ziliripotiwa kituoni hapo na zote zimefikishwa mahakamani.

Afisa wa polisi wa kituo hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa polisi, alisema matukio ya aina hiyo yapo mengi lakini kutokana na baadhi ya wazazi kutoripoti polisi kwa kuyamalizia nyumbani, matukio mengine yanabaki mikononi mwa wananchi wenyewe.

“Matukio haya ni mengi sana, lakini watu wa huku hupenda kumaliza mambo yao nyumbani, wanalipana fidia wenyewe na mtu anaridhika,” alisema ofisa hiyo.

Alisema kuwa baadhi ya wazazi hulipwa Sh. 50,000 na watu waliobaka watoto wao na kukubali yaishe,” alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya wazazi pia huwatumia watoto wao wa kike kama mtaji kwa  kuwatuma kwenda kwa wanaume ili wawawekee mtego halafu wakiwakamata wanawalipisha faini.

Kwa mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Same,  Mndeme, baadhi ya wenyeji wa wilaya hiyo hawapendi kesi zao kuziripoti polisi mpaka mtu awe ameuamia sana na kuhitaji msaada wa polisi.

Alisema baadhi ya kesi zinazofika kwenye ofisi yake ni ya mtuhumiwa huyo aliyefariki dunia ambayo ilishafikishwa kwenye ngazi ya mahakama.

Mndeme alisema baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo kwenye ofisi yake alifuatilia na kulifikisha polisi ambapo mtoto alipewa fomu PF3/ RB/83/2001 kutoka Kituo cha Polisi  Same, kuonyesha amepata majeraha.

Kwa mujibu wa Mndeme, mtoto alipelekwa kupimwa hospitali ili kujua hali yake kiafya, lakini alikutwa hana maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Hata hivyo, alisema ataenda kupimwa tena mwezi Juni, ili kuthibitisha kama hajapata maambukizi.

Alisema mtuhumiwa wa tukio hilo alikamatwa na kesi hiyo ilishaanza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same.

Akitoa takwimu za kesi za ukatili wa kijinsia zilizofikishwa katika ofisi yake, alisema kwa mwaka 2009, alipokea kesi 16, mwaka 2010, kesi nne na mwaka jana alipokea kesi moja.

Mndeme alisema, ushirikiano kati ya polisi na ustawi wa jamii unasaidia kuibua matatizo hayo, hata hivyo anasema kama jamii ingekuwa inatoa ushirikiano wa kutosha watu wanaofanya ukatili huo wangeibuliwa kwa wingi na kuchukuliwa hatua.

Awali mlezi wa mtoto aliyebakwa, alimwambia Mwandishi wa habari hizi kuwa mtuhumiwa aliwahi kwenda nyumbani kwa kwake na kutaka kumhonga pesa ili kesi hiyo aifute.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles