


Mwanafunzi Chuo Kikuu ajinyonga
Watu wanaodaiwa kuwa majambazi wamemuua kwa risasi askari polisi mkoani Kigoma na kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 4:30 usiku katika mtaa wa Kichangani kata ya Mwanga Kaskazini mjini Kigoma baada ya askari huyo D1645-S/SGT.George (45) kuingia katika duka la kuuza dawa za binadamu.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Francis Mwakabana, alisema jana kuwa muda mfupi baada ya marehemu kuingia dukani na kumkuta muuzaji, ghafla waliingia watu wawili na kumwamrisha kuwa yuko chini ya ulinzi kisha kumpiga risasi na kutoweka bila kuchukua kitu chochote.
Mwakabana alisema kuwa baada ya watu hao kuingia ndani ya duka, muuzaji alihisi wanahitaji fedha, lakini hawakuzidai badala yake walimpiga risasi askari huyo na kuvunja kioo cha duka na baadaye kutoweka.
“Baada ya kupata taarifa tulikwenda eneo la tukio, lakini kwa kuwa walitumia miguu na kwa kuwa duka haliko karibu na barabara, walikimbia tukashindwa kuwapata,” alisema Mwakabana na kuongeza kuwa walimchukua marehemu na kumpeleka katika Hosputali ya Mkoa wa Kigoma Maweni, lakini alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Alisema hadi sasa uchunguzi unaendelea na kwamba Jeshi la Polisi linamshikilia muuza duka hilo, Rehema Gwimo (30) kwa ajili ya mahojiano.
“Inawezekana alikuwa na visa na watu hao na pengine ndiyo sababu hawakuchukua kitu chochote,” alisema Mwakabana.
MASHUHUDA WASIMULIA
Shuhuda Meja Bryton (22) alisema: “Nilikuwa dukani kwangu majira ya saa nne usiku katika mtaa wa Kichangani nilivamiwa na majambazi hao ghafla nikapigwa ngumi kwenye shavu upande wa kushoto, wakanikamata na kuniingiza dukani kwangu wakanilaza chini kifudifudi wakapekua dukani na kuchukua Sh. 100,000 pamoja na simu aina ya Nokia yenye thamani ya Sh. 60,000.”
Alisema baada ya kuchukua vitu hivyo walimkanyaga mgongoni kisha kuingia duka la dawa na kumuua polisi.
Shuhuda mwingine, Sofia Alfani (19) alisema: “Nilikuwa ndani naangalia TV katika nyumba hiyo yenye duka la dawa, nilisikia mlio wa risasi nikachungulia dirishani nikaona watu watatu mmoja akiwa na rungu kubwa wakiwa wanatembea haraka haraka wakatokomea kusikojulikana.”
“Baada ya muda nilimsikia muuza duka anapiga kelele za kuomba msaada akisema wamemuua polisi,” alisema Sofia.
Alisema kuwa baada ya muuza duka, Rehema Gwimo, kupiga kelele walitoka nje na kumkuta polisi akiwa chini damu zinamtoka puani, mdomoni na masikioni wakati huo anakoroma na polisi walifika wakamchukua na kumpeleka hospitali ya Mkoa Maweni.
Marehemu alitarajiwa kuzikwa jana nyunbani kwake katika eneo la Nguruka, wilayani Kigoma.
MFANYABIASHARA APIGWA RISASI, APORWA
Mfanyabiashara wa Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, Daniel Gisiri (38), amejeruhiwa kwa risasi na kisha kuporwa gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado TX namba za usajili T. 517 DZT lenye thamani ya Sh. milioni 42 pamoja na vitu mbalimbali, zikiwamo fedha taslimu vyenye thamani ya Sh. 341,100,000.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Ernest Mangu, mfanyabiashara huyo alipigwa risasi kwenye shavu lake juu ya shingo upande wa kulia na watu wawili anaowafahamu ambao ni marafiki zake.
Alisema mfanyabiashara huyo alikumbana na mkasa huo Mei 21, mwaka huu, majira ya saa 4 usiku, katika eneo la Kongowe, wilayani humo.
Alivitaja vitu vingine alivyoporwa aliporwa kuwa ni simu mbili za mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya Sh. 800,000 na Nokia yenye thamani ya Sh. 650,000.
Vingine ni fedha taslimu Sh. 250,000,000 na Dola za Marekani 30,000 pamoja na nyaraka mbalimbali za kiofisi, ambavyo vyote alisema jumla thamani yake ni Sh. 341,100,000.
Kamanda Mangu alisema siku hiyo majira ya jioni, mfanyabiashara huyo akiwa maeneo ya nyumbani kwake, alipigiwa simu na mmoja wa marafiki zake hao.
Alisema marafiki zake hao walimweleza kuwa kuna Mzungu anataka kufanya mkataba naye wa kibiashara eneo la Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Kamanda Mangu alisema kwa kuwa alimwamini sana rafiki yake huyo, aliamua kufunga safari kwenda Mlimani City.
Lakini alisema baada ya kufika huko, hakumkuta huyo Mzungu na badala yake aliwakuta jamaa zake ambao walimwambia kuwa Mzungu yuko kwenye kikao na ameahidi kuwa wakutane naye Mei 22, 2012 saa 9:00 alasiri hapo hapo Mlimani City.
Alisema baada ya hapo mfanyabiashara huyo aliamua kurudi nyumbani kwake na marafiki zake wawili walimuomba lifti ya kurudi Kibaha, ambapo aliwabeba kwenye gari lake.
Kamanda Mangu alisema baada ya kufika eneo la Maili Moja, Kibaha aliomba awashushe pale, lakini walimuomba awapeleke mpaka Kongowe kwani usafiri ulikuwa wa shida na hapakuwa na daladala.
Alisema alikubali kuwapeleka hadi walipofika Kongowe ndipo walipomgeuka na kumtaka ashuke kwenye gari ili wao waondoke nalo.
Kamanda Mangu alisema alijaribu kupambana nao, lakini walipoona anataka kuwazidi, mmoja wao alitoa bastola na kumpiga risasi na kutokwa na damu nyingi na hivyo kumtupa chini na kutoweka kusikojulikana.
Alisema mfanyabiashara huyo amelazwa katika Hospitali Teule ya Tumbi kwa matibabu na kwamba, uchunguzi zaidi unaendelea.
MWANAFUNZI TUMAINI AJINYONGA
Mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam, Hamis Yahaya (20), amejinyonga kwa kutumia kamba ya traki suti katika chumba chake alichokuwa akiishi katika Hosteli ya Evening Star iliyopo eneo la Makumbusho.
Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya wanafunzi, Shaidi Yona, alisema kuwa marehemu alikuwa wanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho.
“Kifo cha Yahaya kimetusikitisha Chuo kizima kwani juzi alikuwa maeneo ya kampasi akiwa mzima, lakini leo nashangaa kupewa taarifa kuwa amefariki dunia,” alisema Yona.
Rafiki wa marehemu, John Luthani, alisema kuwa kifo cha rafiki yake huyo kimemshtua sana kwani juzi (Jumatano) alikuwa naye akiwa mzima.
“Ninachojua hakuna mtu aliyegombana naye, lakini kama alikuwa na ugomvi na mtu mwingine asiyemfahamu rafiki hilo sifahamu ila najua kuwa hakuwa na ugomvi na mtu yeyote,”alisema.
“Yahaya hakuwa mkorofi na kama angekuwa mgomvi usingeuona umati huu wa wanafunzi ambao wamekuja kuuaga mwili wake, hivyo kwetu ni pigo,” aliongeza.
Baba mdogo wa marehemu, Said Gwila, alisema kuwa ameshangazwa na kifo hicho kwani kimetokea ghafla na chanzo chake hakijafahamika, lakini alikuwa aishirikiana na wanafunzi wenzake vizuri.
“Kwa kweli nimeupokea msiba huu kwa simanzi, sifahamu kwa nini alichukua uamuzi huu wa kujinyonga na bila ya kuacha ujumbe wowote,” alisema Gwila.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo, aliiambia NIPASHE kuwa polisi walipata taarifa za tukio hilo kutoka kwa baba mlezi wa marehemu, Lukas Suka (46), mkazi wa Sinza Vatican saa 5:00 juzi usiku.
Kamanda alisema askari walifika eneo la tukio na kukuta Yahaya amejinyonga kwa kutumia kamba ya traki suti ambayo aliifunga kwenye feni na hakuacha ujumbe wowote ulioonyesha sababu za kifo chake.
Mtalimbo alisema maiti ilihifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
Maiti iliangwa jana saa 9:00 alasiri katika Hospitali ya Mwananyamala na baadaye kusafirishwa kwenda Ifakara, mkoani Morogoro kwa mazishi leo.
Imeandikwa na Joctan Ngelly (Kigoma) na Muhibu Said, Leonce Zimbandu (Dar).