Tuesday Jun 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mhadhiri UDSM kizimbani akidaiwa kutusi

21st July 2012
Print
Comments

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini Singida akikabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba.

Dk. Mkumbo ambaye pia ni Mshauri wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika shitaka hilo ameunganishwa  na Afisa wa Sera na Utafiti wa Chadema, Mwita  Mwikwabe (37), aliyesomewa shitaka hilo, Julai16, mwaka huu.

Awali Mwanasheria wa serikali, Maria Mudulugu, alidai kuwa Julai 14, mwaka huu saa 10 jioni, mshitakiwa huyo alitoa lugha ya matusi kwa Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi (CCM), kuwa ni malaya, mzinzi na ni ‘the comedy” huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ruth Masamu, Mwanasheria huyo alidai kuwa mshtakiwa alitoa lugha hiyo kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika kwenye viwanja vya kituo cha mabasi, kijiji cha Nguvumali, kata ya Ndago, jimbo la Iramba Magharibi.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo amekana na yupo nje kwa dhamana ya sh. 800,000 kila mmoja kwa mashahidi wawili hadi Julai 30, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Katika hatua nyingine, wakazi wawili wa kijiji cha Nguvumali, kata ya Ndago, Paulo Nashokigwa Shumu (27) na Emanuel Shila (24), wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi ya mjini hapa wakikabiliwa na tuhuma za kushiriki kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Yohana Mpinga (30).

Mwanasheria huyo wa serikali alidai kuwa Julai14, mwaka huu saa 10 alasiri katika kijiji cha Nguvumali, kata ya Ndago, washtakiwa wote kwa pamoja wakitumia fimbo na mawe, walimpiga Yohana na kumsababishia kifo.

Pamoja na kusomewa shitaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Washtakiwa hao ambao ni vijana wadogo wameunganishwa na washtakiwa wengine 12 waliosomewa shitaka lao la mauaji Julai 16, mwaka huu hadi Julai 30, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment