Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Watumishi wote wanaosaidia kuteketeza misitu wadhibitiwe

1st August 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Katika ukurasa wa 10 wa gazeti hili jana tuliandika habari iliyobeba kichwa cha habari kisemacho “Meneja wa misitu anyang’anywa muhuri wa kuruhusu uvunaji miti” zikiwa ni habari zilizokariri maamuzi ya Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki nchini, Dk. Felician Kilahama, dhidi ya Meneja wa Misitu Hifadhi wa Wilaya ya Kilindi kutokana na tuhuma kuwa unatumika vibaya.
 
Mkurugenzi huyo alitangaza uamuzi huo juzi alipokuwa katika kikao kifupi cha pamoja kilichowashirikisha Tume ya Kukagua Misitu Wilayani Handeni iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Luteni Mstaafu Chiku Galawa, na kufanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu.
 
Kwa mujibu wa Kilahama, wilaya za Handeni na Kilindi zimethibitika kuwa na uharibifu mkubwa wa misitu; miti mingi ya asili ambayo huchukuwa miaka mingi kustawi imeteketezwa kwa kukatwa na msomeno wa mnyororo (chain saw).

Katika mkutano huo Mkurugenzi huyo aliweka wazi kuwa amegundua makosa mengi yanayofanywa katika usimamizi wa misitu wilayani humo ikiwamo matumizi mabaya ya nyundo yenye muhuri kuhalalisha mbao zisizo halali hivyo aliamrisha meneja huyo anyang’anywe kisha irudishwe mkoani na asipewe tena, huku akimtaka kwenda makao makuu Dar es Salaam kwa hatua zaidi.

Mbali ya kubaini matumizi mabaya ya nyundo hiyo ambayo inachangia kuteketeza misitu, pia akishirikiana na maofisa maliasili wilayani Handeni, walifanikiwa kukamata mbao haramu zaidi ya 436, misomeno ya mnyororo saba na misumeno ya kawaida 32 katika misitu hiyo.
 
Katika mkutano huyo ambao Mkurugenzi huyo alitoa ombi kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuongeza udhibiti wa misitu kama inavyofanya mkoa wa Tanga, ilibainika kuwa uharibu wa misitu katika wilaya ya Handeni ni wa kutisha kwani hata wawekezaji wamekuwa wanatumia kivuli cha uwekezaji kushiriki uhalifu wa kuteketeza misitu.

Ulitolewa mfano wa wawekezaji ambao wameteketeza misitu kwa kata miti kwa visingizio vya kuanzisha mashamba, lakini tangu waikate miti hiyo sasa ni takriban miaka 10 imepita, lakini hakuna shamba lolote limeanza na wahusika wametoweka.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha ndani ya mwezi mmoja tunaandika tahariri kuhusu uharibifu wa misitu Handeni na kumpongeza Mkurugenzi huyu kwa hatua anazochukuwa akishirikiana na utawala wa wilaya hiyo ili kuokoa misitu.

Hatuandiki tahariri hii kwa sababu ya kujifurahisha au kumpendezesha yeyote, tunaandika kwa sababu kuu moja, kwamba uharibifu wowote wa mazingira kwetu ni janga la taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho. Tunatambua kuwa uhai na ustawi wa taifa hili unategemea sana mazingira, hususan misitu.

Haingii akilini kwamba watumishi wa umma waliokabidhiwa dhamana ya kusimami na kulinda rasilimali zetu kama misitu ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuendesha vitendo vya uhalifu kwa kushirikiana na watu wasiokuwa na huruma wala mapenzi mema na utawi wa taifa hili, kwa kuteketeza misitu kwa sababu tu ya kutaka fedha kwa njia zisizokubalika.

Itakumbukwa kwamba tangu Januari mwaka huu NIPASHE imekuwa na kampeni kabambe ya kuokoa msitu kuzunguka mlima Kilimanjaro, na ni katika kufichua ukataji mkubwa wa miti mamlaka husika katika mkoa huo, ziliibuka na kuanza kuchukua hatua za kulinda msitu kuzunguka mlima huo mrefu kuliko wote barani Afrika.

Tunapoandika tahariri hii taarifa za kisayansi zinasema kuwa kiwango cha maji juu ya uso wa dunia kimepungua sana, sababu kubwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu ama kwa kujua au kutokujua, tunachukulia uharibifu huo wa Handeni kama sehemu ya kuchochea kasi ya kuadimika kwa maji katika nchi yetu.

Tunatambua kuwa ipo miti mingi ya asili ambayo huchukua hata karne mmoja kukomaa, lakini bila aibu wala juhudi yoyote ya kuirejesha maofisa wa serikali wenye wajibu wa kulinda na kutunza miti kama hiyo ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kuhalalisha biashara haramu kwa maslahi binafsi huku wakisaidia kuteketezwa kwa maliasili za nchi hii. Watu kama hawa hakika hawana nafasi katika utumishi wa umma ni lazima wawajibike kwa vitendo vyao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment