Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Serikali ni lazima iwajibike kwa haya

20th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Wabunge kwa siku mbili sasa wamekuwa wakitema moto katika mjadala wa kujadili ripoti tatu za kamati za kudumu za Bunge zenye wajibu wa kusimamia matumizi ya fedha za umma. Hizi ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC).

Hali ya hewa ni kama imechafuka, wabunge kwa ujumla wao bila kujali vyama vyao vya siasa, wameonyesha wazi kukerwa na kuchoshwa na tabia isiyokuwa na mwisho ya matumizi ya ovyo ya fedha za umma; walengwa wakuu katika shutuma za wabunge ni mawaziri na watendaji serikalini.

Ripoti za PAC, POAC na LAAC zinahusu matumizi ya fedha za umma kwa mwaka wa fedha wa 2009/10, na kilio chao kinaonyesha hali ya kutokujali ya watumishi wa umma katika matumizi ya fedha za umma wakati huduma za kijamii zikizidi kudorora na miradi mingi kusimama kutokana na kukosekana kwa fedha, huku kila kona serikalini hali ya kutisha ya ufujaji wa fedha ikishuhudiwa.

Ingawa wabunge wanawaka kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2009/10, hakika hata ripoti ya CAG kwa  mwaka wa fedha wa 2010/11 ambayo ilitolewa wiki uliyopita mjini Dodoma nayo haionyeshi kuwa kuna unafuu wowote wa maana katika uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma.

Wabunge wengi wameonyesha dhahiri kwamba serikalini ama kuna kulindana mno kiasi cha kukosekana uwajibikaji wa maana hasa kwa wale wanaovunja kanuni za utumishi katika matumizi ya fedha za umma, au imeshindwa kazi.

Hali hii iliwafikisha baadhi ya wabunge kutaka kupitishwa kwa azimio la Bunge la kutaka mawaziri wote wajiuzulu kwa kile kinachoelezwa kushindwa kuwajibika kwa mujibu wa nafasi zao.

Kuna wakati hali ilifika mbali zaidi kwa mbunge mmoja kusema kuwa mawaziri wanaongoza kwa wizi wa fedha za umma, na aliahidi kuwasilisha ushahidi wake mbele ya Bunge. Kwa ujumla mjadala huu umeibua hisia kali sana juu ya matumizi ya fedha za umma.

Tunafurahi kwamba wabunge wameamua kusahau tofauti zao za kiitikadi na sasa wanaongea lugha moja ya kibunge, kuisimamia na kuiwajibisha serikali; lakini la pili ambalo ni la muhimu zaidi, wanataka kuwaona mawaziri kila mmoja kwa nafasi yake akiwajibika kwa madudu yanayotokea kwenye wizara yake.

Hali hii ndiyo ilimfanya Waziri wa Viwanda na Biashara kujikuta akisimama bungeni kujitetea na kumtetea Mkurugenzi Mkuu wa TBS juu ya tuhuma za ubadhirifu katika kazi ya ukaguzi wa magari ugaibuni; ni hali hiyo hiyo ilifanya baadhi ya wabunge juzi kuhoji sababu za msingi za kumfanya Waziri wa Fedha kuwa nje ya nchi katika kipindi muhimu na nyeti cha kujadiliwa kwa ripoti tatu za kamati za Bunge ambazo zinamuhusu sana kwa kiwango kikubwa.

Tunafahamu kwa hakika kuwa hali ya uchumi nchini si nzuri, tumeshuhudia mfumuko wa bei ukipaa kila uchao, lakini kibaya zaidi thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani ikizidi kuporomoka kwa kasi kubwa; matukio yote haya yakitiwa nguvu na matumizi ya ovyo serikalini hakika yanaiacha nchi pabaya sana katika mstari wa maendeleo.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010 huu ni mwaka wa pili, zipo ahadi nyingi zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ilani yake ya uchaguzi, kwa bahati mbaya sana inavyoelekea nyingi hazijagushwa kabisa na wenye wajibu wa kuona zinatekalezwa ni mawaziri.

Tunajiuliza hawa mawaziri wanafikiri muda wao wa kukaa madarakani ni mrefu kiasi gani kiasi cha kuwa na raha ya kuendelea kuponda raha wakati mambo mengi ya kimsingi yamesimama?

Kila kona ya nchi utakayopita leo utakuta vilio vya wananchi juu ya kusimama kwa miradi ya maendeleo hasa ile ya barabara, mathalan, wakandarasi wengi wamesitisha kazi zao kwa sababu kwa muda mrefu hawajalipwa fedha zao na serikali.

Hali hii inatokea wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kila mwezi ikivuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali. Kama walivyosema wabunge, sasa ni wakati wa mawaziri kuacha kuchapa usingizi na badala yake wachape kazi, vinginevyo waachie ngazi ili serikali ijipange upya.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles