Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ligi ya Muungano yarudi kiaina

27th July 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilisaini mkataba wa miaka mitatu na benki ya ABC kwa ajili ya udhamini wa mashindano mapya yatakayoshirikisha klabu nane bora za Tanzania Bara na Zanzibar na kufanyika kwenye viwanja mbalimbali nchini. 

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa mashindano hayo yana lengo la kuziandaa timu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu na yatazishirikisha timu tatu zilizofanya vizuri kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Bara na nyingine tatu kutoka Ligi Kuu ya Zanzibar.

Osiah alizitaja timu nyingine mbili kuwa ni, moja iliyofanya vizuri zaidi katika Ligi Daraja la Kwanza na kupanda katika ligi ya Bara na nyingine itakayokamilisha idadi ya klabu nane ni iliyoongoza pia kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza la Zanzibar.

Alisema kwamba timu hizo zitapangwa kwenye makundi mawili yenye timu nne kila moja na mbili kutoka kila kundi zitatinga hatua ya nusu fainali. Bingwa wa michuano hiyo tu ndiye atakayetwaa zawadi.

Alieleza kuwa kuwa hadi sasa, TFF imeshaziandikia barua klabu za Simba, Azam na Yanga kuhusiana na mashindano hayo na wanaamini watatoa ushirikiano kwa sababu wanataka kuona timu zinaonyesha ushindani kuanzia mwanzo wa ligi na si wakati wa mzunguko wa pili.

Mkuu wa kitengo cha fedha wa benki ya ABC, Mwalimu Zubery, alisema kwamba wamejiandaa kudhamini michuano hiyo kwa sababu wanataka kuona mchezo wa soka nchini unapata maendeleo.

Aliongeza kuwa ni imani yao kwamba wakiwekeza katika mashindano ndipo Tanzania itatoa wachezaji wenye uwezo na kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa watakayoshiriki.

Alieleza kwamba maamuzi ya kuweka vituo vinne vya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar ni kuwapa nafasi mashabiki wa mchezo huo kuziona timu zao zikichuana na hatimaye itakayoibuka bingwa kujinyakulia kitita cha zawadi ambacho kitatangazwa Agosti 2 mwaka huu.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment