Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wizara ya Habari inahitaji tiba

8th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Leo katika gazeri hili ukurasa wa tatu tumeandika habari inayotokana na tamko wa wahariri wa vyombo vya  habari nchini juu ya mwenendo wa kiutendaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambao unaonyesha kuwako kwa masuguano wa dhahiri kabisa baina ya Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo na Katibu Mkuu wake.

Huu ni msuguano ambao kwa hakika unakwaza utekelezaji wa shughuli za kikazi za wizara hii yenye wajibu wa kusimamia tasnia ya habari.

Kulingana na tamko la wahariri waliokutana mjini Morogoro kati ya Juni 3 – 5, mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Mashauriano kati yao na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambao ulishirikisha wahariri kutoka vyombo vya serikali, binafsi na vile vinavyomilikiwa na vyama au taasisi za kidini, pamoja na mambo mengine ulijadili hali na mwenendo wa vyombo vya habari hapa nchini kwa sasa na kwa siku zijazo.

Katika mkutano huo zilijadiliwa mada mbalimbali ambazo kwa ujumla wake zililenga kufanya kazi ya uandishi wa habari kutekelezwa kwa kuzingatia maadili, wajibu na weledi wa kitaaluma.

Pia mada hizo zililenga kuimarisha, weledi wa kitaaluma, uwajibikaji utendaji wa kazi, na uhuru wa vyombo vya habari na zaidi kujenga mfumo wa usimamizi wa maadili ndani ya vyombo vya habari.

Mbali ya hayo, wahariri na wadau wengine wa habari waliohudhuria mkutano huo walijadili kuhusu Mchakato wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Vyombo vya Habari nchini ambao umekuwa ukisuasua kwa takriban miaka 10 sasa.

Ifahamike kwamba, mkutano huu ulikuwa na uzito wa pekee hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba, wahariri ndio wasimamizi na watoa uamuzi wa mwisho katika vyumba vya habari kuhusu masuala yote yanayohusu habari.

Ingawa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, aliombwa kuwa mgeni rasmi na kuthibitisha kuwa angehudhuria kubariki mkutano huo ambao kimsingi unalenga kurahisisha utendaji wa wizara yake, alibadili nia nyakati za majeruhi na kumwelekeza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Seth Kamuhanda, kumwakilisha.

Naye akathibitisha kushiriki, lakini baadaye akabadili nia pia.

Viongozi hao wawili mbali ya kutumiwa rasimu ya hotuba ambayo ilipaswa kusomwa kwanza na waziri ambaye ndiye alipaswa kuwa mgeni rasmi, kabla ya yeye mwenyewe (waziri) kutoa taarifa kwamba angewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara, hawakutokea katika mkutano huo wala kutuma mwakilishi mwingine yoyote, huku wakitoa udhuru kwamba walikuwa na kazi nyingine.

Kimsingi hatua ya viongozi hao kushindwa kufika katika mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kushindwa kwao kutuma mwakilishi mwingine kutoka wizarani, siyo tu iliwashtua wahariri, bali iliwasononesha na kuwashangaza, lakini pia ikithubutisha hisia ambazo zimekuwako kwa muda sasa kwamba kuna mgogoro wa kimahusiano ya kazi kati ya viongozi hawa wawili wa wizara.

Sisi tukiwa sehemu ya tasnia ya habari nchini, tukiwa na kiu na haja ya kweli ya kuona utendaji uliotukuka katika sekta hii, tunaungana na kauli ya wahariri waliokutana Morogoro kwa kuelekeza malalamiko na kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye bosi wa viongozi hawa kwamba atupe macho wizarani hapo ili kurekebisha mambo kabla hayajawa mabaya zaidi.

Tunakumbuka Rais Kikwete alikwisha kusema utaratibu wa katibu mkuu kumtegea waziri wake ili aanguke naye abakie hautavumiliwa, ndiyo maana hata Mei 4, mwaka huu alipokuwa akitangaza mabadiliko makubwa ya baraza lake la mawaziri, alisema wazi kuwa kuanzia sasa uwajibikaji kwa madudu ya wizara hayatamkumba waziri peke yake tu, bali hata watendaji wakuu wa wizara na taasisi za serikali zinazojitegemea.

Tunahisi na kwa kweli hisia zetu zina ushahidi kwamba katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuna tatizo kubwa ambalo linahitaji macho ya haraka ya Rais, vinginevyo sekta ya habari nchini itaingia katika mgogoro usiokuwa na lazima na serikali ambayo malengo yake mapana ni kuisaidia ikue na kuleta ufanisi zaidi nchini.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment