Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mfumo dume bado ni pingu ya jamii

24th April 2012
Print
Comments

Hivi karibuni niliunganishwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook na rafiki yangu mmoja ili niwe mmoja wa washirika wa kubadilishana mawazo. Mimi ni mshirika mkubwa sana na hata kama siandiki husoma sana mawazo ya waingizaji, na kwa vile nafanya utafiti sasa kuhusu facebook na jinsia kwa ajili ya muswada ninaouandika.

Siku moja niliingiza picha ya mwanaume anaendesha kibaiskeli kikiwa na mtoto ndani, siku nyingine nikaweka picha ya jikoni , na siku ya tatu nikaingiza maelezo ya wanaume kuitwa majina kwa ubini wa majina ya kike; na mwisho niliingiza picha ya kuazima ya baba amebeba mtoto huku akiosha vyombo jikoni.

Lengo langu ni kutaka kuona je kama kukiwa na mabadiliko ambayo yanawasaidia sana wanawake katika kufanya kazi nyumbani (wapumzike), wawe na hadhi ya juu zaidi, na waweze kushiriki katika mambo ya kijamii nje ya nyumbani, wanaume na wanawake wenyewe wanajisikiaje. Michango ya waheshimiwa, wanawake na wanaume, ilinifurahisha sana kuhusiana na maingizo hayo.

Kwanza niliona kuwa wanaume wengi hawakuonekana kuchangia, na kwa kweli hapakuwa na wachangiaji wa kutosha sana. Sababu ya kuwa na wachangiaji wachache ni kuwa, kwa nadharia yangu, ni kuwa niliweka maingizo na mapendekezo ambayo maudhui yake wengi hawana mazoea nayo.

Kuwa mwanaume amebeba mtoto mgongoni, na anapika au kuosha vyombo; au mtu akajiita Charles Mwajuma; ni jambo geni na mmoja alisema –“kiama kitakuwa kimefika.” Na kuna mwingine alisema Mungu amepanga hivyo, kuwa, kwa tafsiri yangu, mwanaume awe na hadhi fulani ya juu.

Inapokuwa watu wanaokusudiwa na harakati za ukombozi wa kijinsia kuamini kuwa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni kutokana na majaaliwa ya mwenyezi Mungu, na sio kutokana na ujenzi wa kijamii katika kutufanya tutambue kuwa sisi kama wanawake tuna hadhi fulani, au wale kama wanaume wana hadhi fulani, basi harakati hizo zina mlima mkubwa wa kupanda. Tena mlima mrefu hasa.

Na wengi wa wale walioingia katika kikundi nilikoweka maingizo yangu ni wanaume na wanawake ambao wamepata elimu, na ninafahamu wameingia katika mafunzo ya mambo ya jinsia. Kwa sababu nawafahamu.

Lakini mafunzo hayo hayajawaingia, je sisi akina yahe ambao hatujapata mafunzo kabisa ya kutuamsha kijinsia tunawezaje kujenga utambuzi mpya kuhusu jinsia na haki za mke na mume katika jamii.

Nilidhani wasomi wangekuwa watu wa msitari wa mbele kutambua kuwa mwanamke au mwanaume hatokani na zao la maumbile, kuumbwa, hata kama tunalazimisha vipi na kwa msingi wowote ule; mwanamke na mwanaume ni zao la matunzo kijamii ambayo yameandamana na mafundisho na kuiga kutoka kwenye jamii juu ya nini maana ya kuwa mwanamke au kuwa mwanaume.

Wewe ni wewe sio kwa sababu ya maumbile ya asili au uumbaji, ni kutokana na ulivyokuzwa katika jamii yako, katika familia yako, na katika mifumo ya elimu na kupitia taarifa za vyombo vya habari na kadhalika. Tunaweza kulazimisha kuwa Mungu alituumba hivyo lakini mbona kuna tofauti kubwa za tabia za binadamu katika mwenendo wao.

Kwa mfano sisi tunasema Mungu anataka kila mtoto awe na baba yake na mama yake pamoja.

Lakini kuna makabila hapa duniani ambako msichana anakuambia anataka mtoto na wewe na akishapata mimba anaondoka. Anakwambia kazi yako imekwisha. Anaondoka na mimba yake na mtoto hawi tena wa kwako. Hili ni swala la kijinsia, na halifanani na huku kwetu kabisa. Nalo liliumbwa na Mungu? Yupi?

Mfumo wa malezi ni kitu muhimu sana katika kujenga taswira binafsi ya kijinsia.

Kama malezi hayalengi katika kujenga usawa, inapokuja kwenye elimu, imani, na vyombo vya habari ambavyo kazi zao zimekuwa kusimamia mifumo ya kimfumo dume, basi uwezekano wa harakati zetu kuleta mabadiliko ni mdogo, tena mdogo sana.

Nilishawahi kusema kuwa ingawa juhudi za kuleta mabadiliko katika mifumo mikubwa ya kijamii na kitaifa-marco structures-ni sehemu ya harakati, lakini kujenga na kuhinikiza harakati katika jamii na mtu mmoja mmoja- micro structures, ni muhimu zaidi kwa sababu mifumo ya kitaifa inaundwa na fikra kutoka kwa mtu mmoja mmoja. Ni lazima kubadilisha mbinu za harakati zetu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles