Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kanisa lililochimbwa kusaka dhahabu kuendelea kutumika

28th April 2012
Print
Comments

Kanisa la Kiinjili la Kilutheli (KKKT) Usharika wa Brandt wilayani hapa mkoani Mbeya ambalo limechimbwa karibu na madhabahu kwa ajili ya kusaka dhahabu litaendelea kutumiwa kama kawaida kwa ibada baada ya shimo hilo kufukiwa.

Shimo hilo lenye urefu wa zaidi ya futi 10 limefukiwa baada ya uongozi wa Dayosisi ya Kusini kutangaza kusitisha zoezi la kuendelea kuchimba dhahabu ndani ya kanisa hilo baada ya baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ihahi kupinga zoezi hilo.

Mchungaji wa kanisa hilo, Emmanuel Lunda, akizungumza na NIPASHE Jumamosi jana mjini hapa, alisema baada ya Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele, kutangaza kusitishwa kwa zoezi hilo wameamua kufukia shimo hilo.

Lunda alisema watakarabati vizuri kulirejesha kanisa katika hali yake ya awali na kwamba ukarabati huo utafanywa haraka ili ibada ya Jumapili ya wiki hii iweze kufanyika ndani ya kanisa hilo.

Awali Mchungaji wa Kanisa hilo alieleza kuwa uchimbaji wa madini hayo uliokuwa ukifanywa ndani ya kanisa hilo karibu na madhabahu ulilenga kutafuta dhahabu zinazodaiwa ziliwekwa na Wamisionari wa Kijerumani waliolijenga miaka ya 1908.

Alisema dhahabu hizo kama zingepatikana zingeuzwa na fedha ambazo zingepatikana zingetumika kujenga kanisa jipya la kisasa na nyumba ya mchungaji, ya  Mwinjilisiti wa mtaa na kuweka huduma ya umeme.

Alisema tetesi za kuwepo dhahabu ndani ya kanisa hilo zilikuwa zikienezwa na baadhi ya wakazi wa kjijiji cha Ihahi ambapo Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulent Ng’umbi naye alidokezwa suala hilo ambaye naye aliwaeleza viongozi wa Dayosisi ya Kusini na hivyo kuamuriwa kufanyike utafiti wa madini hayo kwa kuchimba ndani ya kanisa.

Alisema mwanzoni mwa mwezi Aprili, mwaka huu uongozi wa Dayosisi, Jimbo na Usharika baada ya majadiliano ya suala hilo, waliitwa wataalam wa madini ambao walipima ndani ya kanisa kwa kutumia vifaa maalumu vya madini mara tatu kwa nyakati tofauti na kugundua kuwa kulikuwa na madini ndani ya kanisa hilo.

Mchungaji Lunda alisema mara ya tatu wataalam hao walipofika katika kanisa hilo kwa ajili ya kupima madini hayo waliambatana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kusini, Mwamisole, Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulenti Ng’umbi, Mchungaji wa Jimbo la Chunya, Mbilinyi na Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mbedule ambapo iliamuliwa kuwa uchimbaji ufanyike.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles