Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mwenyekiti Chadema achinjwa hadi kufa

29th April 2012
Print
Comments

Mwenyekiti wa Chadema, Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha, Msafiri Mbwambo, (32) mkazi wa Lake Tatu, ameuawa kinyama kwa kuchinjwa shingoni kuanzia upande wa nyuma lakini wakiacha koromeo na mwili wake kutelekezwa makaburini.

Tukio hilo lililitokea majira ya saa 3:00 usiku eneo la Mukidoma, huko Usa River, ambapo wauaji hao wasiofahamika wanadaiwa kuwa walitumia panga kumchinja na kisha kutokomea.

Haijafahamika iwapo tukio hilo ni kisiasa au la lakini Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alitibitisha kutokea kwa mauaji hayo.

Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Arumeru, Totinan Ndonde, alisema jana jioni kwa njia ya simu kuwa hawezi kuhusianisha mauaji hao kwa asilimia 100 kuwa ni ya kisiasa. Hata hivyo, alisema wakiangalia historia ya kampeni za uchaguzi mdogo kuanzia Igunga na huo wa hapo uliofanyika hivi karibuni hapo Arumeru, kuna uwezekano wa kuhusisha mauaji hayo na masuala ya siasa. Hakufafanua zaidi.

Chanzo kingine cha habari kimedai kuwa kulikuwa na ugomvi wa ubadhirifu wa mradi wa maji ambapo marehemu aliahidi kuwataja waliokula fedha hizo.

“Inawezekana wauaji wameamua kumuondoa duniani kwa hofu ya kutajwa kwenye ubadhirifu huo,” kilisema chanzo hicho. Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ya tukio hilo marehemu Mbwambo alikuwa na wenzake kwenye eneo la sterehe huku yeye akiwa hanywi chochote, lakini ghafla alipigiwa simu na watu hao, wakidai kuwa kulikuwa na wanachama wa chama kimoja cha siasa wanataka kurudisha kadi zao cha chama na kujiunga na Chadema.

Habari zilisema kuwa marehemu Mbwambo, alichukua pikipiki na kuwafuata watu hao, lakini, hata hivyo, hakurudi hadi mwili wake ulipokutwa umetelekezwa kandokando ya barabara eneo la makaburi, huku pikipiki na vitu vingine alivyokuwa navyo vikiwa vimebaki eneo hilo bila kuchukuliwa na wauaji hao.

Hata hivyo, chanzo cha tukio hilo hakijajulikana ila taarifa za awali zinahusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa kwani kabla ya hapo baada ya uchaguzi kumalizika katika Jimbo la Arumeru Mashariki malumbano ya masuala ya kisiasa na kukamiana yalikuwa bado yakiendelea eneo hilo.

Kamanda Andengenye alisema polisi bado wanafanya uchunguzi kuhusiana na tukio na kwamba hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo. Alisema mwili wa merehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.

Hili ni tukio la pili la mauaji ya kutisha yaliyoliyotokea wilayani humo hivi karibuni, ambapo tukio wiki iliyopita watu wanne walikutwa wamekufanya kwa kunyongwa na maiti zao kutupwa eneo la Chekereni, wilayani humo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles