Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wafungwa waliogoma wakiona cha moto

15th May 2012
Print
Comments
Kamishna wa Magereza, Augustino Nanyaro

Sakata la mgomo wa wafungwa wa gereza la Lilungu mkoani Mtwara limeingia katika sura mpya baada ya Jeshi la Magereza Nchini kumwagiza Mkuu wa Magereza mkoani humo kukaa na wafungwa hao kujadiliana nao na kama wataendelea kukaidi hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

Kamishna wa Magereza, Augustino Nanyaro, akizungumza katika mahojiano na NIPASHE jana jijini hapa, alisema kutokana na mgomo huo unaowahusisha wafugwa wa kifo hatua za kujadiliana nao zimeanza kuchukuliwa ili kufikia mwafaka.

Hata hivyo, Nanyaro alisema madai ya wafungwa hao ni ya uzushi tu na kwamba baada ya majadiliano hayo kufanyika wafungwa watakaoendelea kugoma hatua za kinidhamu ambazo zimeainishwa kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Tumemwagiza Mkuu wa Magereza Mkoa (RPO) akae na wafungwa waliogoma, wale ambao ni wakorofi wakiendelea na mgomo hata baada ya kujadiliana tutajua hawa siyo wenzetu na itabidi sasa hatua za kinidhamu zichukuliwe,” alisema Nanyaro.

Wafungwa hao wameanza kugoma kula tangu wiki iliyopita ambapo madai yao ni chakula, kupinga manyanyaso ya kipigo kutoka kwa askari magereza pamoja na rufaa zao kuchelewa kusikilizwa na hali ya gereza kuwa mbaya.

Awali jana, NIPASHE ilizungumza na mmoja wa wafungwa waliogoma na kueleza kuwa wameanza kupewa adhabu kali na kwamba wamefungiwa ndani usiku na mchana kuanzia Ijumaa wiki iliyopita.

Mfungwa Abdul Ali Suna mwenye namba 303 aliiambia NIPASHE jana kwamba wamefungiwa ndani kama mbadala wa adhabu yao ya kugoma kula kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa; jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

"Tumepigwa na leo wafungwa wamezimia, hii ni kinyume cha sheria," alisema mfungwa huyo.
Walisema tangu Desemba mwaka jana, wafungwa hawapewi matunda, hawapikiwi nyama wala hawawekewi sukari kwenye uji badala yake wanakunywa uji wa chumvi.

Kadhalika, walisema wamefutiwa huduma ya matibabu na badala yake wamekuwa wakielekezwa kujitibu wenyewe au kujinunulia dawa, jambo ambalo sio sahihi.

Wafungwa hao na namba zao kwenye mabado ni Abdul Ali Sunna (303/2008), Salehe Ramadhani Juma (151/2005), Said Ali Majeje (93/2011), Hussein Said Ntanda (95/2011) na Omary Mussa (104/2011); wote wamehukumiwa kifo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles