


Wiki iliyopita nilijadili katika safu hii kauli ya Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, aliyoitoa bungeni kuwataka watu wote, wakiwamo wazazi na walezi, kuhakikisha vijana wanazingatia na kufuata misingi ya mila na desturi za Kitanzania.
Dk. Mukangara alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maryam Salum Msabaha, bungeni, mjini Dodoma, Novemba 10, mwaka jana.
Mbunge huyo katika swali lake alitaka kujua hatua iliyochukuliwa na serikali kusimamia utamaduni na maadili ya Kitanzania kwa kuwadhibiti wanaume wanaovaa mavazi ya kike kinyume cha utamaduni wa Watanzania.
Katika majibu yake, Dk. Mukangara alisema kwa vile suala la uvaaji wa mavazi linakuwa ni maamuzi ya mtu binafsi, Watanzania wanapaswa kuvaa mavazi ya heshima yanayozingatia maadili ya Kitanzania.
Awali, Dk. Mukangara alilithibitishia Bunge kuwapo na baadhi ya vitendo vinavyofanywa nchini na wanaume au wanawake kinyume cha maadili ya taifa.
Nilieleza kuwa pamoja na maelezo hayo ya Dk. Mukangara, kuna unafiki mkubwa katika kuhimiza maadili ya taifa.
Hiyo ni kwa sababu ustawi wa jumla wa maadili ya taifa hauwezi kupatikana mahali ambapo jitihada njema za wazazi, walezi na viongozi wa dini hazipati ushirikiano au msaada wa dola.
Ukweli huo unathibitishwa na kasi ya mmomonyoko wa maadili inayozidi kuongezeka nchini siku hadi siku.
Kufuatia hoja hiyo, baadhi ya wasomaji wapenzi walinipigia simu na wengine kuniandikia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) kutoa maoni yao kuhusiana na mada hiyo.
Mmoja wa wasomaji aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mrisho, mkazi wa jijini Dar es Salaam, alinipigia simu. Pamoja na kupongeza uchambuzi mzuri wa mada hiyo, aliilaumu serikali kwa kutoweka bayana maadili ya taifa. Akadai hali hiyo imewafanya wananchi wengi kutojua ni yapi maadili ya taifa.
Ningependa niungane na msomaji huyo kutaka ufafanuzi huo kutoka kwa serikali ili kukata kiu ya wananchi.
Wakati tukisubiri ufafanuzi huo, itakumbukwa katika makala yangu ya wiki iliyopita, nilieleza japo kwa uchache namna mwelekeo wa serikali ya Tanzania unavyofanana sawia na ule wa nchi za Magharibi kiutendaji.
Lakini hali sio hiyo peke yake. Bali serikali imekwenda mbali zaidi. Imeufungulia milango utamaduni wa Magharibi ambao umemeza utamaduni mzuri wa taifa.
Utamaduni huo wa kigeni umechangia na unazidi kuchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maadili hasa ya kizazi kipya.
Kwa mfano, kitendo cha kuruhusiwa miziki ya wanengua uchi, mitindo ya mavazi yasiyo ya heshima, mashindano ya urembo, elimu ya jinsia kwa watoto wadogo, biashara ya kondomu, kumeporomosha maadili kwa kasi ya mshale.
Mengine yaliyoporomosha maadili kwa kasi hiyo, ni kuruhusiwa vitabu na majarida yenye picha za ngono, filamu za ngono, utalii wa kihuni, ufunguaji wa mabaa, makasino, kumbi za starehe za usiku, dawa za urembo na kadhalika, Ingawa utamaduni wa asili una dosari zake, bado una nafuu kubwa sana kuliko ule wa kizungu.
Maadili ya “vijana wa zamani” yalikuwa mazuri mno kuliko ya vijana wa leo. Hata miziki ya asili ilikuwa bora kuliko ndombolo, ikibindankoi na kwasakwasa.
Miziki kama ile ya akina Marijan Rajabu na Mbaraka Mwinshehe ililenga kuadilisha jamii.
Kwa kiasi kikubwa nyimbo zao ziliwajenga kimaadili vijana wa zamani. Walikuwa na heshima, uungwana na nidhamu ambayo vijana wa leo nathubutu kusema hawana.
Halikadhalika, utaratibu wa jadi wa kutoa elimu ya jinsia japo ulikuwa na kasoro zake, lakini ulikuwa na nafuu kubwa kuliko elimu ya sasa ya jinsia.
Elimu ya jinsia ya sasa inawataka wazazi, walimu na watoaji wa ushauri nasaha kuwafundisha watoto namna ya kujamiiana kwa njia salama.
Matokeo yake limeibuka wimbi la ufuska. Watoto wa umri mdogo kabisa ‘wanachemka’ na ngono.
Wengi wamekufa kwa kujaribu kutoa mimba, wameambukizwa ukimwi na wamekatisha masomo. Pia wameua vizazi na wengine kuteseka na mzigo wa malezi kama si kutupa watoto kwenye mashimo ya vyoo.
Japo zamani kulikuwa na matukio kama haya, lakini si kwa kiwango cha sasa. Ndio maana nasema serikali inastahili lawama kwa kuufungulia milango utamaduni wa Magharibi. Tujirekebishe sasa.
Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. Barua pepe: muhibu72@yahoo.co.uk