Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga, Villa leo hapatoshi

17th March 2012
Print
Comments
Timu ya Yanga

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, watashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu kwa kuvaana na Villa Squad kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku wakiwa na matumaini ya kuwakaribia mahasimu wao Simba walio kileleni mwa msimamo.

Kama wakishinda, Yanga wanaokamata nafasi ya tatu kwenye msimamo watawapiku Azam na kupanda hadi katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 43, mbili zaidi ya Azam na pointi moja nyuma ya vinara Simba ambao hata hivyo, watakuwa na nafasi ya kujichimbia zaidi kileleni wakati watakaposhuka ugenini kesho kucheza dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Akizungumzia mechi  yao ya leo, kocha wa Yanga, Kostadin Papic, alisema kuwa kipindi hiki kwake ni cha mapinduzi na wachezaji aliobaki nao wanatakiwa kuonyesha uwezo ili kuipa matokeo mazuri timu yao inayopigana kutetea ubingwa.

Papic alisema kuwa ana kazi ya ziada kwenye kikosi alichobaki nacho na kuongeza kwamba kila mchezaji anatakiwa kuonyesha uwezo wake wote wa kuitumikia klabu hiyo katika wakati huu ambao kila mechi iliyobaki kwao ni ngumu na hivyo wanaichukulia kama fainali.

"Tuko tayari na tutafanya kila linalowezekana ili tushinde, ukweli tuko kwenye wakati mgumu kwa kuwakosa wachezaji watano kikosini," alisema Papic, akiwazungumzia wachezaji wake waliofungiwa kutokana na vurugu zilizotokea Jumamosi iliyopita katika mechi yao dhidi ya Azam ambao ni Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haruna Niyonzima, Nurdin Bakari na Jerry Tegete.

Aliongeza kwamba kilichotokea kwa wachezaji wake hakipaswi kurudiwa tena kwa sababu kinaiweka timu kwenye nafasi mbaya na vilevile kinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya soka nchini.

Habib Kondo, ambaye ni kocha wa Villa Squad, alisema kwamba pamoja na timu yake kukabiliwa na mazingira magumu, lakini leo wanaamini wataonyesha kiwango cha juu ili kupata ushindi na kujiondoa kwenye ukanda wa kuteremka daraja.

Kondo alisisitiza kuwa maamuzi ya haki ndio yatakayosaidia kutoa mshindi anayestahili katika mechi hiyo na nyingine zilizobaki za ligi.

Katika mechi nyingine ya leo, Coastal Union wataikaribisha JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment