Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

JK awataka wamiliki kutoa ajira kwa waandishi mapema

1st April 2012
Print
Comments
Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi (kushoto), wakifurahia jambo wakati wa hafla ya utoaji tuzo za umahiri katika uandishi wa habari Tanzania kwa mwaka 2011.

Rais Jakaya Kikwete amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuacha kuwatumia waandishi kwa kipindi kirefu bila kuwaajiri hali ambayo inawafanya waishi katika mazingira magumu.

Aliyasema juzi jijini Dar es Salaam wakati akisoma hutuba yake katika halfa ya tunzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari Tanzania 2011 (EJAT).

Alisema kitendo hicho huwafanya waandishi kufanya kazi katika mazingira mabaya na hata kujihusisha na tuhuma za rushwa.

Rais Kikwete alisema wakati umefika wa kuwepo na mfumo mzuri wa kusimamia maslahi ya waandishi wa habari ili kuondokana na tatizo hilo.

Alisema kuna waandishi ambao wamefanya kazi kwa kipindi kirefu matokeo yake wanapewa ajira watu ambao hawana taaluma hiyo.

"Utakuta waandishi wenye taaluma nzuri hawaajiriwi ila wale makanjanja wana ajira wakati hawana hata taaluma hiyo ya uandishi sasa wakati umefika wa kuwepo na mfuko wa kusimamia masuala ya uandishi kwani watatakiwa kuzijua haki zao zote wanazotakiwa kupatiwa," alisema Rais.

Hata hivyo, alisema taaluma ya uandishi wa habari inatakiwa kuheshimiwa na kuhakikisha wanapatiwa ajira yao.

Alisema ndio maana unawakuta waandishi wengi wakifika muda wa kuacha uandishi wanabakia kuwa masikini na kujikuta hawana maendeleo yoyote.

Alisema kuna wengine hawana uhakika wa ajira zao na hata maslahi yao hawayafahamu, hivyo kwa taaluma kama hiyo ni muhimu na inatakiwa iangaliwe.

Alisema waandishi wa habari wanatakiwa kuzingatia maadili na kusimamia msingi mkuu wa kanuni za uandishi kwani kutokufanya hivyo ni ukiukwaji wa maadili.

"Kuna gazeti kila likitoa toleo wapo mahakamani andikeni habari za ukweli na sio uwe na chuki na mtu ndio unaamua kumtengeneza katika gazeti lako hayo sio maadili," alisema Rais.

Alisema endapo ukifanya kazi zako kwa nia ya chuki ni sawa na kuua uhuru wa vyombo vya habari.

"Napata tabu kuona waandishi wanavyoandika habari ambayo inawafanya watu waone nchi yao ni ya hovyo na viongozi wake ni ovyo mbona mazuri hayaandikwi kwanini tunashabikia mambo ya wenzetu wakati wao hawapo hivyo," alisema.

Rais Kikwete alisema kwa sasa wanaelekea kwenye mchakato wa katiba mpya, hivyo baada ya siku chache ataunda tume.

Alisema katika jambo hilo vyombo vya habari vinatakiwa kuhakikisha inafanya kazi yake kwa kufuata maadili na sio kusababisha ushabiki usio kuwa na msingi.

Aidha, alisema anategemea jambo hilo litaendeshwa kwa amani katika kuwepo na mijadala mbalimbli ili wananchi waweze kutoa maoni yao juu ya katiba mpya.

Akizungumzia ombi la Jukwaa la wahariri kutaka kukutana naye kwa ajili ya mazungumzo, Rais alisema yupo tayari na kwamba wapange muda.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema waandishi walioteuliwa 69 kati ya 779 waliteuliwa kutoka mikoa mbalimbali kushindanishwa katika zoezi hilo na kwamba majaji tisa walioteuliwa ndio waliofanya kazi hiyo.

Alisema washindi kila nyanja watapata cheti, tunzo na zawadi ikiwemo lap top na digital still camera.

Kajubi alisema mshindi wa jumla ambaye atapata zawadi yoyote pia atapata kitita cha kujiendeleza masomo ambayo ni dola 4,000 za kimarekani ambapo mshindi aliyejinyakulia nafasi hiyo ni mwandishi wa Mwananchi, Neville Meena.

Kwa upande wa mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya Habari alipatiwa, Filli Karashani, ambapo alipatiwa cheti pamoja na Sh milioni 10.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Regnald Mengi alitoa tuzo kwa mwandishi mlemavu wa Mlimani Televisheni, Tuma Dandi, ambaye alishinda kwa kuandika habari za walemavu.

Waandishi mbalimbali walijinyakulia zawadi akiwemo mwandishi wa ITV Televisheni, Imanuel Buhohela, ambaye alishinda kwa kuandika habari ya utawala bora.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment