Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Malawi yashindwa kukanusha kuwafukuza Watanzania Ziwa Nyasa

5th August 2012
Print
Comments

Ubalozi wa Malawi jijini Dar es Salaam umegeuka bubu baada ya kushindwa kukanusha ama kuthibitisha madai kuwa imewafukuza Watanzania wanaoishi kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, kwa madai kuwa ziwa hilo ni mali ya taifa hilo kwa asilimia 100.

Jitihada za NIPASHE kutaka kujua msimamo wa Malawi juu ya madai hayo ziligonga mwamba baada ya ofisa wa ubalozi huo kueleza kuwa hana la kusema juu ya taarifa hizo.

Ofisa huyo aliyefahamika kwa jina moja la Andoje licha ya kukataa kuzungumzia mvutano huo pia alililaumu gazeti na kutoa kauli kuwa “ kwani nyie mnapotuuliza hamliamini Bunge lenu?

Licha ya kuelezwa kuwa ni taratibu za uandishi wa habari kusikia maelezo ya pande zote zinazohusika kwenye habari husika alisisitiza kuwa msimamo wa Malawi ni kwamba hawana lolote la kuzungumzia kuhusu mgogoro wa Ziwa Nyasa na kuondoka kwenye meza ya mazungumzo huku akikataa kutaja jina.

Malawi imeanza utafutaji wa gesi na mafuta kwenye ziwa Nyasa na kusababisha mvutano baada ya nchi hiyo inayopakana na mikoa ya Ruvuma na Mbeya kudai kuwa ziwa hilo ni mali yake.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alipoulizwa juu ya hali halisi kwenye maeneo ya ufukweni ziwani Nyasa alisema hadi wakati akitoa taarifa hizi wananchi wako salama na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Aliwaambia wakazi wa maeneo ya mwambao kama Mbamba Bay , Lituhi na Liuli kuwa wasiwe na hofu kwa vile mgogoro huo unashughulikiwa na upo ndani ya uwezo wa serikali .

Jitahada za kuwasiliana na wakuu wa mikoa ya Mbeya na Njombe ambayo nayo inapakana na Ziwa Nyasa hazikufanikiwa. Hata hivyo yapo madai kutoka kwa wananchi wanaoishi mpakani na Malawi kuwa chokochoko za mpaka zilianza muda mrefu hata kabla ya kifo cha Rais Bingu Mutharika aliyefariki Aprili mwaka huu.

Taarifa ya Serikali juu ya mgogoro huo inasubiriwa kutolewa bungeni na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Lakini hata hivyo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye hivi karibuni alikuwa Kaimu wa Shughuli za Serikali bungeni, aliwataka wakazi wa mikoa ya mpakani na Malawi ya Iringa, Mbeya na Ruvuma kuendelea na kazi zao na kusisitiza kuwa Tanzania iko tayari kwa choko choko za Malawi.

Malawi inadaiwa kutoa leseni ya kusaka mafuta na gesi kwa kampuni ya Uingereza kufanya utafiti katika eneo hilo tena ikiingia ndani ya Tanzania .

Mvutano wa mpaka wa Tanzania na Malawi ulianza tangu wakati wa Rais wa kwanza marehemu Dk. Kamuzu Banda na sasa umeingia katika mgogoro mpya kwenye awamu ya Rais Joyce Banda, aliyechukua uongozi Aprili mwaka huu.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment