Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Al Ahly Shandy watua na Waghana, Wanigeria

27th April 2012
Print
Comments
Nahodha wa timu ya Al Ahly Shandy, Malik Issack akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jana kwa ajli ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili.

Timu ya soka ya Al Ahly Shandy kutoka Sudan iliwasili nchini jana mchana tayari kwa mechi yao ya awali ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya wenyeji wao Simba itakayofanyika kuanzia saa 10:00 jioni Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, anatarajiwa kuwa mgeni. Sumaye pia aliongoza mashabiki kuishangilia timu hiyo katika mechi ya kwanza dhidi ya ES Setif ya Algeria ambapo Simba ilishinda 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Kikosi cha Al Ahly Shandy kimewasili kikiwa na wachezaji 20, watano wakiwa ni wa kigeni ambapo watatu wanatoka Nigeria, mmoja Ghana na mwingine kutoka nchini Mali.

Wachezaji wawili wanachezea timu ya taifa ya Sudan. Baadhi yao waliwahi kuchezea klabu kongwe za Sudan za El Mereikh na El Hilal.

Kocha wa Al Ahly Shandy, Kouk Mohamed aliwaambia wana habari baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana kuwa wamekuja kusaka ushindi na kwamba wenyeji wao wategemee mechi ngumu sana lakini ameisifu Simba kuwa timu nzuri yenye sifa kubwa nchini kwao.

Nahodha wa timu hiyo, Malick Isaack alisema wanajua kuwa Simba iko nyumbani hivyo itakuwa na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini wamekuja kushindana ingawa ukweli utabaki pale pale kwamba soka lina mambo matatu, kushinda, kushindwa ama sare.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa wageni wao Al Ahly Shandy wamefikia kwenye hoteli ya Durban na jana jioni walitarajiwa kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa Karume.

Kamwaga alisema kuwa kufika kwa wageni hao ni ishara kuwa timu zote mbili ziko tayari kwa mechi hiyo ya keshokutwa na Simba ambao ni wenyeji wamejipanga kupata matokeo mazuri ili waweze kujiwekeza mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa.

"Wachezaji, viongozi na kila anayeipenda Simba tumejiandaa kuipa sapoti timu ili tuweze kufanya vizuri katika mechi ya Jumapili, hata mawazo ya mechi ya watani ya kufunga ligi kwa sasa hatuna kichwani," Kamwaga alisema.

Aliongeza kuwa waamuzi wa mechi hiyo ni kutoka Swaziland ambao ni  Nhleko Simanga Pritchard atakayesimama katikati na wasaidizi wake, Mbingo Petros Mzikayifani na Sibandze Thulani pamoja na Fakudze Mbongiseni Elliot atakayekuwa wa akiba watawasili jijini leo jioni.

Pia alisema kwamba kamisaa wa mchezo huo kutoka Rwanda, Kayijuga Gaspard, naye atawasili leo mchana akitokea jijini Kigali.

Tiketi za mchezo huo ambazo kiingilio cha chini ni Sh. 5,000 zitaanza kuuzwa leo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam huku klabu hiyo ikiwataka mashabiki na wanachama kujitokeza kwa wingi kuipa hamasa timu yao ili ifanye vizuri na hatimaye kuwa na kazi nyepesi kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika katika mji wa Shandy ambao ni kilomita 150 kutoka Khartoum, Sudan.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles