Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tunahitaji kuwa makini zaidi kwenye elimu

15th May 2012
Print
Comments

Katika toleo moja la gazeti la kila siku linalotolewa kwa lugha ya Kiswahili wiki hii, ilichapisha picha moja ya iliyokuwa ya kibanda cha nyasi (sio nyumba), ikiwa na madawati na wanafunzi  ilielezwa na mpiga picha kuwa  ile ilikuwa ni picha ya wanafunzi  darasa la sita  wakiendelea na masomo.

Nina uhakika kabisa kuwa ile shule imeingizwa kama sehemu ya mafanikio ya elimu tangu tupate uhuru. Ni bahati mbaya iliyolifika taifa hili.

Moja ya jambo nililolitaja katika makala ya safu hii hii wiki iliyopita ni kukosekana kwa uwiano kati ya watahiniwa wa shule mbalimbali kutokana na wanafunzi kupitia mifumo tofauti ya ufundishaji na elimu kwa ujumla.

Nilisema kuwa nina wasiwasi kama kweli mitihani ya kwetu- kwa darasa la saba au kwa sekondari,  inapima kile kinachotakiwa kupima, au kinatumika tu kama kigezo cha kuchuja wanafunzi ili wapatikane wanaoweza kuitwa wamefaulu na wanaoruhusiwa kuendelea na masomo.

Sielewi Baraza laMitihani linawezaje kujidai kuwa mitahani hii ni kipimo sahihi kwa wanafunzi wetu kama wanafunzi kama walioko kwenye picha wako sio kwa ajili ya kusoma bali kukutana na mwalimu tu, na mwalimu anafundisha ili mradi, ili mshahara uingie.

Kama tuna wanafunzi ambao hajui lini watakutana na walimu, na ambao hawajawahi kuona vitabu vinavyotumika shuleni kama vitabu vya kiada, na kuwa kuwa na vitabu vya ziada ni ndoto; halafu tuna wanafunzi ambao mazingira yao kielemu ni mazuri na wanapata kila kitu wanacho kihitaji, na hizo shule sio za watu na mashirika binafsi, bali za serikali, unaweza sasa ukatunga mtihani ambao unakuja kusema unalengo la kuleta usawa katika kuwapima na kuwapata wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na masomo ya juu?

Huu kama sio mchezo wa kuigiza usioakisi uhalisia ni kitu gani sasa. Halafu cha ajabu wanafunzi wanaposhindwa kufanya mitihani kwa ufaulu unaotakiwa kwa idadi kubwa sana tunaanza kujiuliza imekuwaje; na tume iundwe kuchunguza.

Lakini kumbe majibu tunayo sisi wenyewe; kuwa hakuna uwekezaji wa kutosha, na ulio sawa kwa shule zote; na kuwa elimu bado innayonekana sio msingi wa maendeleo, na serikali inafurihia kuona tunawezekeza katika wajinga wa miaka ijayo ambao hawatajua kusoma na kuandika.

Kinachoonekana kwa watendaji wetu sio kuwepo kwa shule zenye kila aina ya uwezeshaji ili watoto wasome kwa usawa (baina ya shule zote), bali ili mradi kujenga mahali ambapo watoto wataweza kukutana na kucheza kila siku, mbali na wazazi wao, na wanapoweza kukutana na walimu, hata kama hakuna masomo yanayoendelea.

Halafu eti tunazungumza kuwa tunaweza kushindana katika soko la ajira katika Afrika Mashariki, na kuna yule aliyesema eti kuna siku na sisi tutafikia kiwango cha maendeleo ya Korea Kusini. Na sisi tutengeneze simu kama za Samsung! Kwa elimu ipi, kwa sababu hata ya chuo kikuu bado kuna mengi yanayohitajika kuiboresha na hayapo na hatujui tutayapata lini.

Niwakumbuka hapa marafiki zangu wa shirika la  Haki Elimu wanaolia na kuzorota kwa elimu; kwa kudhani uboreshaji wa miundo mbinu ni sahihi sasa, lakini je, wanajiuliza ni falsafa gani inaongoza elimu yetu?

Kama nchi imeamua kujenga mifumo ya kitabaka kwa kuruhusu shule za wenye vibanda vya nyasi kusoma na kufanya mitihani sawa na wanaosoma kwenye madarasa yenye viyoyozi na kufanyiwa shughuli zote za usafi na walioajiriwa kufanya kazi hizo, ni msingi (philosophical foundation) ya elimu yetu.

Na kipi sasa tuanze kupigania, kuboresha miundombinu, au kuitafakari upya falsafa hii mpya ya kuchanganya mbaya na mbovu ili mradi siku ipite.

Kipi tuanze kujadili, msingi wa elimu au uendeshaji wa elimu. Kama kweli elimu ingekuwa na msingi wa kifalsafa wenye kuzingatia mahitaji yetu anwai, na unaozingatia mabadiliko ya dunia katika fani zote, sidhani kama tungekuwa na aina hii ya utoaji elimu wa mradi kumekucha, na siku ikapita; na kama tunasema kuwa elimu iwe ni msingi wa kujenga usawa miongoni mwa Watanzania, sidhani serikali ingeruhusu kuwa na mfumo wa elimu unaoona kuwa Kiingereza ni lazima kama lugha ya kufundishia; na kuwa hata kama wanafunzi wanasoma kwa mitaala tofauti, “hakuna noma”, na kuwa hata kama wanafunzi wanatofautiana katika ubora wa mazingira ya kusomea, hakuna shida. Nadhani sasa tunajifikisha njia panda na hatutakuja jua tuchukue uelekeo upi.

[email protected], 0766959349

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles