Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Mmoja afariki vurugu za Mtwara
Mtu mmoja amefariki dunia katika vurugu zinazoendelea Mkoani Mtwara kupinga gesi kusafirishwa, ambapo pia ofisi kadhaa na nyumba moja zimeharibiwa.

Klabu zitoe nafasi kwa yosso waliong`ara Copa Coca Cola

16th July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Copa Coca Cola ilimalizika jana kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam ambapo mashabiki walishuhudia soka la ushindani mkali kutoka kwa wanafainali Mwanza na Morogoro.

Vijana kadhaa wenye vipaji walionekana kuanzia mwanzo wa michuano hiyo hadi jana jioni wakati ilipofikia tamati. Karibu kila nafasi ilipata vijana walioonyesha umahiri mkubwa.

Mashabiki waliobahatika kushuhudia michuano hiyo walikuwa mashahidi wazuri juu ya ukweli wa madai kwamba nchi yetu ina vijana wengi wenye vipaji vya soka; isipokuwa tatizo pekee ni namna ya kubaini vipaji hivyo na kuviendeleza.

Sisi tunadhani kwamba kupitia michuano ya Copa Coca Cola kama iliyomalizika jana, wasaka vipaji wa klabu mbalimbali za soka nchini, hasa za Ligi Kuu ya Bara, walipata nafasi nzuri ya kujionea vipaji vipya na hivyo wakabaki na kazi rahisi ya kuchagua wale wanaoamini kuwa wanaweza kuendelezwa.

Kwa mfano, maafisa wa benchi la ufundi la klabu ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya Bara walionekana kila mara katika michuano hii, wakiwafuatilia vijana wenye vipaji kwa kile kilichoonekana wazi kuwa ni kutaka kuwanasa vijana watakaowajumuisha katika timu yao ya yosso.

Tunadhani kwamba klabu nyingine pia hazikulaza damu. Zilituma wawakilishi wao na kupata vijana wanaoamini kuwa waling’ara, hivyo kuwa na mipango thabiti ya kuwaendeleza kwa manufaa ya baadaye ya timu zao na taifa.

Ni imani yetu kwamba zoezi hilo lilifanyika kwa weledi mkubwa. Kwamba, vijana walioonyesha kuwa wana vipaji vya hali ya juu hawaachwi hivi hivi, bali wanachukuliwa na klabu mbalimbali kwa nia ya kuwaendeleza.

Changamoto pekee kwa kila klabu ni kuhakikisha kwamba yosso wote wanaowapata katika michuano ya Copa Coca Cola hawapotei bure. Badala yake, wanawalea vyema na baadaye kuwapa nafasi zaidi ya kuonyesha umahiri wao kupitia vikosi vyao vya timu B na hatimaye kuwajumuisha katika timu za wakubwa.

Tunawakumbusha viongozi wa klabu mbalimbali kuwa mchezo wa soka hauna njia ya mkato. Ni lazima wakubali kuwekeza kiasi cha kutosha kwa vijana kabla ya kufikiria namna watakavyonufaika nao katika miaka michache ijayo.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba, mchakato huo wa kulea vijana wenye vipaji huhitaji subira.

Kwa mfano, yosso Shomari Kapombe alivumiliwa kwa muda mrefu na wale waliomlea mkoani kwao Morogoro kabla Simba hawajamuona na kumpa nafasi ambapo sasa amekuwa mmoja wa nyota wa kutumainiwa kwa ‘Wana Msimbazi’ na pia kwa Taifa Stars.

Viongozi wa klabu ya Azam walilazimika kuwa na uvumilivu mkubwa katika kuwalea chipukizi wake kadhaa na sasa wanafaidi matunda kupitia kwa baadhi yao, akiwemo Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, anayeng’ara katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na pia Taifa Stars.

Wakati wa fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, wawakilishi wa Afrika, timu ya taifa ya Ghana ‘Black Stars’ walituonyesha pia umuhimu wa kuwekeza katika soka la vijana.

Bado tunakumbuka kuwa soka maridadi la Ghana katiks michuano hiyo liliwapa raha mashabiki wote wa soka barani Afrika baada ya kushinda 2-1 dhidi ya timu ngumu ya Marekani na hatimaye kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, ikiwa ni rekodi ya tatu kwa timu za Afrika kufikia hatua hiyo baada ya Cameroon na Senegal kuwahi kufanya hivyo katika fainali za miaka ya 1990 na 2002.

Wachezaji wengi waliounda kikosi cha Ghana kilichoshiriki Kombe la Dunia walikuwa ni chipukizi wa umri wa wastani wa miaka 20, baadhi yao wakiwa ni Andre Ayew, Jonathan Mensah, Inkoum na yosso wengine ambao pia waliunda kikosi cha timu yao ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 20 kilichotwaa Kombe la FIFA la Dunia la vijana wa umri wao kwa kuwafunga Brazil nchini Misri, Oktoba mwaka 2009.

Kuwepo kwa michuano ya vijana ya Copa Coca Cola na mingine ya aina hiyo kama ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na ya sekondari (UMMISETA) kunatoa fursa nzuri kwa klabu za soka kupata vipaji vipya.

Ni kwa kutambua ukweli huo, ndipo nasi tunaposhauri kuwa vijana wote waliong’ara katika michuano iliyomalizika jana ya Copa Coca Cola wapewe nafasi ya kuendelezwa katika klabu zetu ili waje kuzipa mafanikio klabu hizo na pia timu ya taifa, Taifa Stars.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment