



Licha ya kumaliza dakika 120 wakiwa 10 uwanjani, mabingwa watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Yanga walionyesha soka la uhakika wakati walipowabwaga UPR ya Rwanda kwa bao 1-0 katika mechi yao na nusu fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Yanga sasa watacheza fainali dhidi ya Azam FC, ambayo iliwafunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali iliyochezwa uwanjani hapo mapema jana mchana.
Goli pekee la mshambuliaji Hamis Kiiza 'Diego' katika dakika ya 100 kufuatia krosi ya kiungo Haruna Niyonzima liliwapeleka Yanga katika fainali ya pili mfululizo baada ya kurejeshwa katika michuano hiyo kufuatia kusamehemewa adhabu yao ya kifungo cha miaka mitatu wakiwa tayari wametumikia miaka miwili.
Azam walitanguliwa kwa goli la mapema katika dakika ya 35 kupitia kwa Alfred Mfongang, lakini mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ alifunga goli lake la tano katika michuano hiyo na winga aliyeingia akitokea benchi Mrisho Ngassa alifunga la ushindi katika dakika ya 88.
Ngassa, ambaye anaonekana kukosa furaha katika kikosi hicho kutokana na kukaa benchi baada ya nafasi yake kutwaliwa na Kipre Tchetche wa Ivory Coast, alichochea tena uvumi kwamba anataka kurejea Jangwani baada ya kupigwa picha akiibusu jezi ya Yanga aliyokuwa ameivaa.
Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alipoulizwa na mtangazaji Thomas Mlambo wa kituo cha televisheni cha Supersport cha Afrika Kusini sababu za kutomuanzisha Ngassa, alisema: “Najua ni mchezaji mzuri, ninamuhitaji, lakini nataka ajitume zaidi.”
Yanga walimaliza wakiwa 10 baada ya beki wa kulia Godfrey Taita, kupewa kadi ya pili ya njano kwa kuchelewesha mpira wakati wenyeji wakiongoza kwa bao 1-0.
Kocha wa APR, Ernie Brandts, ambaye alishuhudia timu yake ikifungwa mechi ya pili na Yanga ndani ya wiki moja baada ya kulala 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C Ijumaa iliyopita, alimlalamikia mwamuzi wa mechi hiyo akisema: “Hii ni Afrika. Mchezaji analala uwanjani kwa dakika sita lakini mwisho wa mechi zinaongezwa tatu.”
Malalamiko ya Brandts yalifuatia kujiangusha mfululizo kwa kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’, akidai kuumia katika dakika za kuelekea mwisho wa mechi.
“Goli limepatikana baada refa kuruhusu mechi iendelee wakati kulikuwa na faulo. Hii ni Afrika. Hii ni Afrika,” alilalamika Brandts.
Hata hivyo, akijibu tuhuma hizo, kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, alisema kama Brandts anadai kwamba kulikuwa na faulo kabla ya Yanga kurusha haraka mpira na kufunga goli, basi wachezaji wawili wa APR walipaswa kutolewa kwa kadi nyekundu katika tukio hilo.
“Mchezaji wangu katolewa kwa kadi nyekundu nyepesi wakati wachezaji wa APR wamecheza rafu nyingi, wamemuimiza beki wangu wa kulia (Juma Abdul aliyetoka dakika ya 27) na hawakufanywa kitu. Kama makosa refa alifanya na aliyafanya kwa pande zote.
“Timu yangu imecheza vizuri baada ya kipindi cha kwanza, ambapo haikucheza vizuri, ni vizuri kumpongeza mshindi,” alisema Saintfiet, ambaye amekabidhiwa timu hiyo katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja sasa.
Kikosi cha mechi ya Yanga kilikuwa: Ali Mustapha 'Barthez', Juma Abdul/ Shamte Ali (dk.27)/ Rashid Gumbo (dk.86), Godfrey Taita, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Oscar Joshua, Athuman Idd 'Chuji', Stephano Mwasika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuz na Hamis Kiiza 'Diego'.
Kikosi cha Azam kilikuwa:
Deogratias Munishi, Ibrahim Shikala, Erasto Nyoni, Said Moradi, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tchetche/Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Ibrahim Mwaipopo and Ramadhani Chombo.