Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Eti ni kweli wanaume wa Moshi ni wababaishaji wazuri ndani ya ndoa?

6th May 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, katika wiki tatu hivi mfululizo, nilizungumzia namna meseji za simu zinavyozua balaa ndani ya nyumba nyingi.

Baadhi ya wasomaji wa makala hizo walipata fursa ya kutoa ushuhuda kwa yaliyowasibu ndani ya ndoa, yakitokana na meseji zilizojaa utata. Kwa mfano, sikiliza kilio cha msomaji huyu, kisha baadaye nitakumegea msomaji mwingine aliyemjibu.

“Mimi niko Moshi. Nimekamata meseji za mapenzi kwenye simu ya mke wangu. Nikamuuliza akakiri nikampa namba ya aliyemtumia meseji ile akaomba msamaha. Nikamwambia sawa, nimekusamehe.

Nimekaa miezi miwili nimepata nyingine sijui nifanyeje. Watoto bado wadogo, wako watatu naomba ushauri”. Baada ya kuisoma meseji hii ilibidi nimpigie simu kaka huyu nipate undani wa malalamiko yake naye akawa na haya ya kusema;

“ Mimi nina ushahidi na kwa sasa sina imani naye, tena napanga kwenda kupima afya. Bwana anayehangaika naye namfahamu na nitakachoamua ni kwamba nitaondoka na kumwachia nyumba na watoto ingawa watoto wangu nitawapa matunzo. Siwezi kukaa naye amenikwaza sana.

Hata baada ya kumsamehe, nimegundua bado wanaendeleza mahusiano, sitaki tena inatosha”, anamaliza kusema bwana huyu na kukata simu.

Mpenzi msomaji, hebu sasa msikie huyu msomaji mwingine anavyochangia maoni mada hiyo;

“Dada Flora, achana na wanaume wa Moshi, hawana mapenzi ya dhati, akishakuweka ndani, basi, amemaliza kila kitu. Wajeuri, wana dharau acha kabisa.

Niko kwenye ndoa nao kwa miaka 15 sasa nimeshuhudia mengi mtu hawezi kunidanganya. Mada hiyo kuhusu meseji toka msomaji wa Moshi nimeisoma.

Mpaka mwanamke atoke nje ya ndoa siyo mchezo, amechoka hasa. Huyo dada wa watu kachoka mwache ajinafasi kama kampata wa kumliwaza hasa.

“Mimi mwenyewe nafikiria kufanya hayo hayo. Mungu atatunusuru kwani anafahamu mengi kutoka mioyoni mwetu. Lakini ukweli wanaume wa Moshi ni taabu tupu”, anamaliza bibie ujumbe wake huo wa simu ya kiganjani.

Msomaji mwingine anamlalamikia mkewe ambapo ujumbe wake unasomeka hivi; “Maisha Ndivyo Yalivyo, mke wangu hataki kazi yoyote na kila baada ya miezi mitatu ni ugomvi, anakaa kwao na kurudi mwenyewe bila kufanya kesi.

Kazi yake ni kwenda kwa waganga wa jadi kuchunguza mumewe kama ana mwanamke mwingine. Je, huyo ni mke kweli?(Naitwa Tumaini wa Moshi). Huyu ni mwanaume mwingine toka Moshi akilalamika kuhusu mkewe.

Mpenzi msomaji, wiki hii nimesimuliwa kituko hai kinachodhihirisha jinsi baadhi ya wanaume walivyo wasaliti wa ndoa kwa makusudi hasa pale anapopata uchochoro wa kufanya maasi hayo.

Nikiwa napata soda maeneo ya Kariakoo wiki iliyopita nikiwa na wifi yangu, alifika mahali pale kaka mmoja ambaye naye alikuwa anajitafutia mlo wa mchana.

Wifi yangu anamfahamu wakasalimiana. Kidogo akafika bibie mmoja ambaye moja kwa moja alikwenda kuketi na kaka yule. Ndipo wifi yangu akanidokeza kuwa wale ni marafiki, japo siyo wa muda mrefu.

Stori aliyonipa wifi ni kwamba, kijana yule ana mke na watoto wawili. Na yule aliyekuwa ameketi naye ni kimada aliyemuopoa siku za karibuni.

Cha ajabu ni kwamba kimada huyo siyo kwamba alikuwa hamjui kabla. Bali alikuwa anachukuliwa na vijana mbalimbali eneo analofanyia biashara bibie huyo mjasiriamali mwenye duka la vyakula.

Wengine waliokuwa wanamchukua ni marafiki wa kijana aliye naye sasa. Kwa maneno mengine, vijana wenzake katika eneo hilo wanamshangaa alivyoshikamana na bibie wakati akijua ni ‘jamvi la wageni’ yaani kila anayejisikia hujinafasi naye.

Cha kushangaza sasa ni kwamba huyo kijana mkewe amekwenda kwa wakweze kujifungua na sasa anajirusha na kimada huyu nyumbani kwake na siyo ajabu ndani ya chumba cha ndoa.

Hebu fikiria nyumba ina mke na watoto pamoja na ndugu za mume lakini anadiriki kuleta kimada mle ndani kwa kuwa tu mkewe hayupo. Hii ni haki kweli?

Nakubaliana na msomaji wetu hapo juu aliyezungumzia wanaume wa Moshi na kusema acha kabisa hawafai wanalalamika lakini wameficha madhambi mabaya kabisa. Angalia huyu anayeamua kuchafua nyumba yake kwa kuingiza kimada ndani, tena analala hadi asubuhi na kuondoka kwa wakati wake.

Kwa mtaji huu watu wanaponea wapi? Yule mama aliyekwenda kujifungua hana hili wala lile, huku nyuma mumewe anamsaliti kwa kuingiza mwanamke ndani ya boma lake. Huyu baba anampenda mkewe kweli?

Haishangazi ndiyo maana vifo vya wanandoa vinavyotokana na maradhi hatari, ukimwi, vinaongezeka kwa kuwa virusi hivyo vinatolewa nje na kuingizwa ndani kweupee bila huruma wala haya. Upo hapo msomaji wangu? Tufanyeje sasa?

Huu ni mchezo hatari sana kwani ndio unaochipua vifo vingi vya wanandoa, vifo vya watoto ambao walitakiwa kuzaliwa salama lakini wanajikuta wameathirika kwa virusi vya ukimwi na pia nyumba nyingi zinatikisika na familia kufarakana, chanzo kikubwa kikiwa uvunjifu wa uaminifu miongoni mwa wanandoa.

Maneno ndani ya Biblia Takatifu yanasema: Nukuu… “Mwanamke mwenye hekima hujenga nyumba yake, lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe(Biblia Takatifu Kitabu cha Mithali 14: 1 )Kadhalika kwa mwanaume mwenye hekima….”

“Malaya ni shimo refu la kutega watu, mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba. Yeye hunyemelea kama mnyang’anyi, husababisha wanaume wengi kukosa uaminifu(Mithali 23:27-28)”.

Mpenzi msomaji wangu, nimenukuu maneno hayo mazuri ndani ya Biblia yangu nikiamini kuwa hayo ni maneno toka kinywani mwa Mungu mwenyewe. Ameweka bayana kila kitu, lakini ubinadamu huu unatutesa na kuasi njia zake.

Tujiulize, kwanini tunatenda kinyume na yale aliyoagiza kwa maisha mema hapa duniani? Kila mmoja wetu atafakari hilo na kuchukua hatua, hatujachelewa nafasi ya kubadilika bado ipo, ila usikawie kwani muda hausubiri.

Bila shaka msomaji wangu umepata ujumbe kwa maelezo ya hapo juu, sasa nikuachie nawe utafakari na utoe maoni yako hasa tabia hii ya kuvizia mama kaenda kazini, baba anarudi na kumnyatia hausigeli. Au mama kaenda safari ya kikazi baba analala kona na vidosho au kaenda kujifungua, yeye bila hofu, aibu anaingiza kimada ndani ya boma la ndoa. Ni haki hiyo?

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles