Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Majeruhi waongezeka Yanga

28th June 2012
Print
Comments
Kikosi cha Yanga

Wakati kitendawili cha kocha mpya wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga, kikitarajiwa kuteguliwa kati ya kesho na keshokutwa, timu hiyo imeendelea kuandamwa na tatizo la majeruhi baada ya jana kiungo Nurdin Bakari kuumia mguu huku kipa Yaw Berko akilazimika kusimama kufanya mazoezi mpaka atakapopona.

Juzi beki wake mpya, Kelvin Yondani, pia aliumia kwenye mazoezi ya timu hiyo ambapo kocha msaidizi Fred Minziro alisema kuwa moja ya matatizo anayokumbana nayo ni Uwanja wa Kaunda kukosa ubora na jana walilazimika kuuhama kutokana na kujaa matope na kwenda kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Posta Kijitonyama ambao nao nyasi zake hazijajaa kama inavyotakiwa.

Akizungumza na gazeti hili, Nurdin alisema kuwa ameambiwa apumzike kwa muda wa siku tatu na baada ya hapo atafanyiwa vipimo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kuanza tena mazoezi.

Nurdin alisema kuwa anasikitika kukosa programu za kwanza za mazoezi ambazo ndio humjenga mchezaji kujiandaa na ushindani wa mechi za mashindano.

Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, aliliambia gazeti hili kuwa Nurdin tatizo lake si kubwa lakini Berko haijajulikana atakuwa nje kwa muda gani.

"Nurdin amepewa siku mbili za kuangalia hali yake na Berko bado atapumzika mpaka daktari wa timu hiyo atakapomuangalia tena," Sendeu alisema.

Hata hivyo, Sendeu alishindwa kuthibitisha kama timu hiyo itaenda Zanzibar kushiriki mashindano ya Kombe la Urafiki ambayo wamealikwa.

Kiungo huyo wa Yanga aliumia pia kifundo cha mguu akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) na kumfanya aachwe kwenye safari ya Ivory Coast mapema mwezi huu akiwa ni mchezaji pekee wa Yanga aliyeitwa kwenye timu hiyo.

Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Simba na Azam zote za jijini wanajiandaa na michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu kwa kuzishirikisha timu zaidi ya 12 za ukanda wa CECAFA.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment