Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tanzania yarejesha matumaini netiboli Afrika

11th May 2012
Print
Comments
Nyota wa timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, Mwanaidi Hassan (katikati) akimiliki mpira wakati wa mechi yao ya kuwania ubingwa wa Afrika kwenye Uwanaj wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Taifa Queen ilishinda 37-34.

Timu ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, ilipata ushindi wake wa pili katika mechi tatu baada ya kuifunga Zambia kwa magoli 37-33 katika pambano lililojaa upinzani la kuwania ubingwa wa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Queens ambao walishinda 57-13 dhidi ya Lesotho katika mechi yao ya ufunguzi Jumanne, kabla ya kulala 34-30 dhidi ya Malawi juzi, sasa wamefikisha pointi 4, sawa na Malawi ambao nao wameshinda mechi mbili.

Matokeo hayo yamerejesha matumaini ya Tanzania katika michuano hiyo ya timu sita inayoendeshwa kwa mtindo wa ligi.

Katika mechi nyingine ya jana, Zimbabwe iliifunga Botswana 32-28.

Zambia walikuwa wa kwanza kulisakama lango ya Taifa Queens na kupata magoli ya haraka katika robo ya kwanza ya mchezo huo ambayo ilimalizika wakiwa mbele kwa magoli 8-6.

Wenyeji Taifa Queens walicharuka katika robo ya pili na kwenda mapumziko wakiongoza kwa magoli 20-16.
Taifa Queens ilimaliza robo ya tatu ikiwa mbele kwa magoli 28-26 na ikamaliza vyema robo ya mwisho kwa ushindi wa 37-33.

Mabao ya Taifa Queens yalipachikwa na wafungaji Mwanaid Hassan, Pili Peter, Irene Elias na Mwadawa Twalib wakati ya Zambia yalifungwa na B Nakazone, Lucky Jere na Brenda Mwila na Ebber Sithole.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kocha wa timu hiyo Mary Protas alisema mechi ilikuwa ngumu kwao kutokana na kwamba walihitaji ushindi ili warejeshe matumaini ya ubingwa.

Alisema Zambia ni wapinzani wao wa muda mrefu ambao wamekuwa wakiwafunga mara kwa mara hivyo kuwafunga leo imekuwa faraja kwao.

Nahodha wa Taifa Queens, Lilian Sylidion alisema mchezo huo ulikuwa mgumu lakini walitumia akili ya ziada ya kupunguza mipira mingi ya wapinzani isifike langoni mwao na hatimaye kuibuka na ushindi.

Mfungaji wa Taifa Queens, Mwanaid, alisema mechi yao dhidi ya Zambia ilikuwa ni kama fainali kwao kwani timu hiyo imekuwa ikiwasumbua sana.

"Tumefurahi kuifunga Zambia, kwa sababu wamekuwa wakitufunga kila mara, nina imani kiwango chetu kimeongezeka," alisema Mwanaid.

Mashindano hayo yanaendelea tena leo ambapo Botswana itacheza na Lesotho, Zimbabwe itaivaa Zambia katika mechi za asubuhi wakati jioni Botswana itaikabili Malawi, huku Taifa Queens wakiwakaribisha Zimbabwe.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles