Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

CHANETA iungwe mkono maandalizi netiboli Afrika

30th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kiko katika maandalizi kabambe ya kuandaa michuano ya netiboli ya Afrika inayotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Mei 8 hadi Mei 12.

Hadi sasa, tayari nchi kadhaa zimeshathibitisha kuwa zitakuja nchini kushiriki katika mashindano hayo. Kenya, Uganda, Burundi, Zambia, Malawi, Botswana na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi hizo ambazo zimeahidi kutuma vikosi vyao kwa nia ya kupigania taji la michuano hiyo yenye heshima ya aina yake barani Afrika.

Licha ya nia nzuri waliyo nayo CHANETA katika kuandaa michuano hiyo, lakini chama hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa katika kutimiza malnego yao. Moja kati ya changamoto hizo ni ya namna ya kupata fedha za kufanikisha malengo yao.

Taarifa zilizowahi kutolewa na CHANETA zinaonyesha kwamba uhaba wa fedha ni tatizo kubwa zaidi. Kwamba, kwamba takribn Sh. milioni 120 zinahitajika kwa ajili ya kufanikisha maandalizi ya michuano hiyo.

Malazi, chakula na usafiri wa ndani kwa wageni ni baadhi ya gharama bila shaka haziwezi kuepukwa na wenyeji.

Kwa kuzingatia ukweli huo, ndipo tunapoona kwamba ipo sababu ya kuwaunga mkono CHANETA kwa hali na mali ili wafanikishe vyema malengo yao na kuwapa nafasi vijana katika kuonyesha vipaji vyao vya netiboli, huku wakijilinganisha na wenzao wa mataifa mengine.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, wake za baadhi ya mabalozi na wadau wengine mbalimbali wa michezo nchini wameshajitokeza na kuonyesha kwa vitendco dhamira yao ya kusaidia maandalizi ya michunao hiyo ya Afrika.

Hata hivyo, wadau wa michezo nchini wanatakiwa kuongeza kasi ya kusaidia maandalizi hayo kwani hadi sasa, taarifa kutoka CHANETA zinaeleza kwamba kiasi kilichopatikana bado hakijafikia malengo.

Wadau waendelee kujitokeza kwa wingi zaidi na kuunga mkono maandalizi ya michuano hiyo ya Afrika kwani ni wazi kwamba ikifanyika kwa ufanisi, sifa njema zitakuwa ni kwa taifa zima na wala siyo kwa CHANETA na viongozi wao pekee.

Kinyume chake, kama michuano hiyo itadorora na kukumbwa na kashfa itokanayo na ukata na maandalizi duni, aibu itakuwa ni kwa taifa zima. Hivyo, ni wajibu wa kila mdau wa michezo kuhakikisha kwamba michuano hiyo inafanyika vizuri na tena kwa weledi wa hali ya juu.

Uzoefu katika maeneo mengine unaonyesha kwamba wanamichezo wengi nchini si wabaguzi. Hujitokeza kwa wingi katika kuziunga mkono klabu za michezo mbalimbali, ikiwemo ya soka. Hawasiti pia kuziunga mkono timu za taifa za soka za wanaume, wanawake na hata vijana wadogo.

Moyo huu wa kizalendo umewahi kujidhihirisha mara kadhaa wakati wa maandalizi ya timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), ambapo wapenzi wa michezo walijitokeza kusaidia fedha, vyakula, maji na hata dawa.

Hali kama hiyo pia imeshaonekana wakati wa kuiandaa timu ya taifa ya soka ya wanawake (Twiga Stars), ambapo kwa mara nyingine, wadau wengi wa michezo nchini, bila kujali jinsia, walijitokeza kwa wingi na kuichangia timu hiyo wakati ikijiandaa kwa mechi mbalimbali za michuano ya kimataifa.

Tunadhani kwamba sasa ni wakati muafaka pia wa kuendeleza mshikamano katika kusaidia maandalizi ya michuano ya Afrika na pia kuisaidia timu yetu ya taifa ya netiboli (Taifa Queens).

Kupitia CHANETA, tunadhani kwamba wadau wote wa michezo, wakiwemo wa makampuni binafsi, taasisi za umma na hata mtu mmoja mmoja, wanapaswa kuunga mkono maandalizi haya kwa kuchangia fedha na vitu vingine mbalimbali vinavyohitajika katika kuendesha michuano hiyo kwa ufanisi.

Shime. Tujitokeze kwa wingi katika kuunga mkono maandalizi ya CHANETA kwa ajili ya michuano ya netiboli ya Afrika ambayo bila shaka itakuwa ni ya kihisotia.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles