Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tunaunga mkono juhudi za kufufua reli

2nd August 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Miongoni mwa nyenzo rahisi na za uhakika katika sekta ya usafirisjhaji ni reli. Kwa njia hii ni rahisi zaidi kusafirisha mizigo mikubwa na mzito kwa haraka na ufanisi zaidi, hali ambayo huchangia kwa kasi zaidi kukuza uchumi katika taifa lolote lile duniani.

Nchi zote zilizopiga hatua ya maana katika maendeleo, zimejikita sana katika kusimamia na kuelekeza nguvu zote katika usafiri wa reli kwa kuwa ndiyo ukombozi wa kweli katika usafirishaji.

Tanzania tumejaliwa kuwa na reli kuu mbili, ile ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Reli ya Kati. Kwa sasa itakuwa ni kujidanganya kusema kuwa zinatoa huduma kwa kiwango kilichotarajiwa ndiyo maana shughuli kuu ya usafirishaji wa mizigo na abiria imehamia barabarani.

Ukiitazama Reli ya Kati inatia huruma; mabehewa yamechakaa, vichwa vya treni (injini) ndiyo usiombe kabisa, lakini kikubwa zaidi hata njia yenyewe (reli) nayo iko hoi.

Hali imesababisha huduma zitolewazo na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuwa duni sana kiasi cha kushindwa kabisa kuvutia wateja wa maana.

Siku hizi nchi hii imekuwa ni soko kubwa la malori ya mizigo, siyo kwa sababu mizigo imeongezeka sana, la hasha, ila kwa sababu barabara imebakia kuwa njia pekee ya kusafisha mizigo na abiria.

Tangu juhudi za kubinafsisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuwa TRL zishindwe kuleta tija yapata miaka mitano hivi iliyopita, taifa hili limejaa malumbano ya nani kafanya hiki au kile kiasi cha kufikisha shirika hilo hapo lilipo leo.

Bila kumung’unya maneno, waliofikisha TRL hapo lilipo leo ni sisi Watanzania; ni sisi ambao tulipata fursa ya kuajiriwa ndani ya shirika hili, badala ya kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii, tulishiriki kwa njia moja au nyingine katika kulihujumu. Kwa maana hiyo Watanzania wanapaswa kujilaumu na kujilaani wenyewe kwa kuua TRL.

Hata hivyo, pamoja na majuto haya, tunafarijika sasa kusikia kwamba zipo juhudi za kweli kabisa za kubadili hali ya mambo. Akiwasilisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Uchukuzi bungeni jana, Waziri wake, Dk. Harrison Mwakyembe, aliweka bayana mikakati ya kufufua Kampuni hiyo.

Pamoja na mambo mengine alisema katika mwaka wa fedha wa 2012/13 serikali imetenga Sh. bilioni 104 kwa ajili ya kufufua kampuni hiyo.

Aliainisha kazi zitakazofanyika kuwa ni pamoja na kujenga upya njia ya reli, kufufua injini na mabehewa ya mizigo na abiria, kulipa madeni makubwa iliyokuwa inadaiwa kampuni hiyo ili kujijenga upya na kwa kasi na morali mpya.

Katika hotuba hiyo waziri huyo alisema watakarabati injini nane, kutoa malipo ya awali kwa injini mpya 13, mabehewa mapya 22, kukarabati ya mzigo 125 na kununua mapya 274, sambamba na kufufua reli katika jiji la Dar es Salaam.

Waziri huyo alisema kwa  Dar es Salaam  Sh. bilioni 4.75 zimekwisha kupatikana kwa ajili ya kufufua njia ya reli, injini tatu na mabehewa 14 ili kusaidia usafiri kwa jiji hilo na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.

Kwa macho na tathmini ya aina yoyote malengo na mipango hii ni vitu vikubwa, ni kujitoa kwa nguvu zaidi kurejesha huduma ya usafiri wa treni katika heshima inayostahili kwa ajili ya kusaidia uchumi wan chi hii. Tunapongeza hatua hizi na kumtia moyo waziri wake na wizara nzima kwa ujumla kusimamia kazi hii kwa ufanisi mkubwa.

Tunasema bila kujibidiisha kujenga miundombinu yetu, hakika hakuna Mgeni kutoka kokote atakayekuja kusaidia kazi hii, kwa maana hii tunaunga mkono juhudi hizi za kuthubutu, tunawatia shime wote wenye wajibu wa moja kwa moja katika kufanikisha kazi hii wafanye biadii ili kufikia malengo tarajiwa.

Hata hivyo tungependa kutoa angalizo kwamba katika utekelezaji wa miradi mikubwa kama hii, walaghai wenye mioyo ya kifisadi hawakosekani, ni kwa maana hiyo tunawataka wote wenye dhima ya usimamizi kuwa macho kuhakikisha kwamba malengo haya yanafanikiwa na hivyo kuleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini. Kila la heri Wizara ya Uchukuzi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment