Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tume ya Mabadiliko ya Katiba iwafikie wengi

11th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Rais Jakaya Kikwete, wiki iliyopita, alitangaza Tume ya Mabadiliko ya Katiba huku akimteua Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba, kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo.

Aidha, Rais Kikwete, alimkumbuka mshindani wake wa kisiasa katika kura za maoni mwaka 2005, Dk. Salim Ahmed Salim.

Dk. Salim, Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya na Rais Kikwete, walifikia kilele cha kupigiwa kura za kuwania urais mwaka 2005 ambapo Kikwete, ambaye ndiye Rais wa sasa, alishinda.

Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo.

Tume hiyo pia ina Katibu, Naibu Katibu na wajumbe 30 ambapo Tanzania Bara na Zanzibar zina wajumbe 15 kila upande.

Akitangaza majina hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete, alisema wajumbe hao ni sehemu ya majina zaidi ya 550 ambayo yalitumwa na wadau mbalimbali kumshauri awape nafasi hiyo, hivyo ikamrahisishia yeye kufanya uteuzi huo.

Aidha, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kabla ya kupitisha na kutangaza majina hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alishauriana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Pia Rais Kikwete alisema katika uongozi wa sekretarieti ya tume hiyo, Katibu aliteuliwa kuwa Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu ni Casmir Sumba Kyuki.

Mbali na Dk. Salim, wajumbe kutoka Tanzania Bara ni pamoja na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu na Mkuu wa Idara ya Sheria wa NCCR-Mageuzi, Dk. Sengodo Mvungi.

Wengine ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, Riziki Mngwali, Richard Lyimo, John Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Jesca Mkuchu, Profesa Palamagamba Kabudi na Humphrey Polepole.

Wengine ni Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir na  Mwantumu Malale.

Rais Kikwete aliwataja wajumbe kutoka Zanzibar (pamoja na Dk. Salim) kuwa ni Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said na Ussi Khamis Haji.

Wengine ni Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohamed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.

Akizungumza kabla ya kutangaza majina hayo, Rais Kikwete alisema mchakato huo utafanyika kwa awamu na hatua tofauti ndani ya miezi 18, ambapo kukamilika kwake kunatarajiwa kuwa mwaka 2014.

“Huu ni mchakato utakaotufanya tuwe na Katiba inayofanana na Taifa, itakayoliongoza na kulilea taifa kwa miaka mingi ijayo huku tukiwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano,” alisema.

Alizitaja hatua zitakazopitiwa kabla ya kuwepo Katiba mpya ni maoni ya Watanzania kuhusu Katiba na maudhui yake, kuwepo Bunge Maalum la Katiba litakalojadili muswada wa Katiba na makubaliano ya mwisho kuwasilishwa kwa umma.

Kimsingi, kama walivyo Watanzania wengi, tuna imani kubwa na wajumbe wa tume hii wengi wao wakiwa ni watu wanaoheshimika mno mbele ya jamii, watu makini, wasomi na wenye uzoefu wa kutosha katika masuala ya kisheria, kiuchumi, kisiasa, kijamii na wengine wanaharakati wa haki za binadamu.

Kwa mfano, Mwenyekiti wake, Jaji Warioba, mbali ya kuwa mwanasheria aliyebobea, pia ni mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Waziri Mkuu na za kisiasa kama vile ubunge na pia aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rushwa.

Kwa upande wake, Jaji Ramadhani, amebobea katika taaluma ya sheria na aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Hali kadhalika, wajumbe wa tume hiyo, wengi wao wanaheshimika sana nchini kutokana na kuwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika awamu mbalimbali za uongozi serikalini.

Mathalani, Dk. Salim, aliwahi kuwa mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wakati huo, na pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vile vile, Mkurungenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ni miongoni mwa watu wanaoheshimika mno hapa nchini kutokana na mchango wake wa kuliongoza taifa.

Hata hivyo, tunachopenda kukisema leo katika tahariri hii, si kueleza nani ni nani katika Tume, bali ni kuwaomba na kuwasihi wajumbe wa tume hiyo kuwa wafanye kila liwezekano kuhakikisha kwamba wanawafikia Watanzania wengi zaidi popote pale walipo ili kupata maoni yao.

Tunafahamu kwamba nchi yetu ni kubwa kijiografia na inakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara, jambo ambalo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa wajumbe wa tume hiyo washindwe kuyafikia maeneo mengine ya nchi kwa kazi hii nyeti.

Lakini pamoja na tatizo hilo, bado tunaamini kwamba tume hiyo itajipanga vema ama kwa kuigawa nchi katika kanda au vyovyote vile itakavyoona inafaa ilimradi kuhakikisha kwamba inakabiliana na vikwazo hivyo kwa maslahi ya Taifa letu.

Kwa hakika, haitakuwa imewatendea haki Watanzania iwapo baada ya kukabidhi ripoti yake kwa Rais, litokee kundi fulani ama kikundi na kudai kwamba eti halikupata fursa ya kuchangia maoni ya Katiba mpya.

Hata hivyo, pia tungewasihi Watanzania wafahamu kwamba waliokabidhiwa kazi hiyo siyo malaika bali ni binadamu wenzetu, ambao kwa namna moja ama nyingine, wanaweza kupitiwa ama kutoona kila kitu.

Inapotokea hali hiyo, basi tunawaomba Watanzania wenzetu wawe na uelewa na kuvuta subira badala ya kuwalalamikia wajumbe wa Tume kwani miezi 18 iliyopewa tume hiyo kukamilisha kazi hii, kihalisia na kwa nchi kubwa kama Tanzania, si muda mrefu.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles