


Baadhi ya makatibu wakuu na wakuu wa taasisi zilizoguswa na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2009/10 na za kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Mashirika ya Umma (POAC) na ya Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma na kushindwa kuwajibika, wameelezea hatma yao baada ya mawaziri wa wizara zao kufutwa kazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, na NIPASHE viongozi hao kutoka Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii na Shirika la Umeme (Tanesco) wamejiweka kando na udhaifu uliobaishwa katika ripoti ya CAG, kwa hali hiyo kutokuwa tayari kujiuzulu nyadhifa zao.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijja, alisema hawezi kujiuzulu kwa sababu ya waziri wake, Mustafa Mkulo, kuwajibishwa kutokana na ripoti ya CAG kuonyesha ubadhirifu katika wizara hiyo na kwamba, anasubiri hatima yake kuamuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema anasubiri maamuzi ya Rais Kikwete kwa kuwa alishazungumzia suala hilo.
Rais Kikwete akitangaza baraza jipya Ijumaa iliyopita Kikului jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wakati sasa umefika kama wizara au taasisi ya umma inayojitegemea au shirika la umma infanya madudu kiasi cha kumfanya waziri wake kuwajibika kisiasa, hatua sasa zitafuta kwa makatibu wakuu, wakurugenzi na maofisa watendaji wa taasisi hiyo ili kuongeza wigo wa uwajibikaji.
“Rais alishazungumza, tusubiri maamuzi,” alisema Khijja alipotakiwa na NIPASHE jana kueleza sababu za kutochukua hatua ya kuachia ngazi kwa hiari yake kutokana na waziri wake kuwajibishwa kwa makosa yaliyotendwa na wasaidizi na watendaji wa wizara yake.
Khijja alisema yeye si mwanasiasa, bali ni mwajiriwa wa Utumishi (Ofisi ya Rais-Utumishi), hivyo hawezi kuwajibika kwa misingi ya kisiasa.
“Unaniuliza kama mwanasiasa. Mimi nimeajiriwa na Utumishi. Utumishi wana taratibu zao. Nimeambiwa taratibu zote za ajira. Kama unaona nastahili kuwajibika waambie Utumishi,” alisema Khijja.
Alimtaka mwandishi kusoma vitabu vya utendaji ili apate ufahamu wa utendaji kazi wa makatibu wakuu wa wizara.
Alisema kama angekuwa na makosa yanayostahili kuwajibika, asingesita, badala yake angefanya hivyo mara moja tena siku nyingi bila kusubiri kuwajibishwa.
“Naweza kutoka hata kama (aliyekuwa Waziri wa Fedha), Mustafa Mkulo angekuwapo,” alisema Khijja.
Alisema hakuna mwenye uhakika iwapo makosa yaliyomwajibisha Mkulo yalitendwa naye kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
“Una uhakika?” alihoji Khijja alipotakiwa na NIPASHE kueleza maoni yake juu ya waziri wake kuwajibishwa kwa kosa lililotendwa na watendaji wa wizara yake.
KATIBU MKUU WIZARA VIWANDA NA BIASHARA
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo, alisema hana sababu ya kujiuzulu kwa kuwa ripoti zote za utendaji wa wizara yake hazina matatizo yoyote.
Alisema kama kuna kuwajibika kwa makosa ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), basi anayestahili kuwajibika ni TBS yenyewe.
MKURUGENZI MKUU WA TBS
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, hakupatikana jana kuzungumzia msimamo wake kuhusiana na suala la kuwajibika na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi muda wote jana ilikuwa imezimwa.
KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, awali alipotafutwa kwa simu, mara zote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Dakika chache baadaye, katibu mkuu huyo alipiga simu katika chumba cha habari cha NIPASHE na kutaka kumjua aliyekuwa akimtafuta na anachomtafutia.
Alipojibiwa kuwa ni mwandishi wa NIPASHE, kabla mwandishi hajakamilisha sentesi iliyotaja kuwajibishwa kwa aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Ezekiel Maige, Tarishi alimtaka mwandishi atumie simu yake kumpigia kwa maelezo kwamba simu aliyokuwa akiitumia muda huo ilikuwa ya mkononi.
Mwandishi alimpigia Tarishi, lakini hadi tunakwenda mitamboni, simu yake iliishia kuita tu bila kupokelewa kabisa.
KATIBU MKUU WIZARA YA UCHUKUZI
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Omar Chambo, alipotafutwa, alisema hawezi kuzungumza kwa maelezo kwamba, muda huo alikuwa na mkutano na mawaziri.
“Naomba kidogo, nina mkutano hapa na mawaziri,” alisema Chambo kisha akakata simu.
WILLIAM MHANDO WA TANESCO
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, alisema kuwa kuna watu wanampiga vita na kutaka aondoke katika nafasi yake na kwamba ikiwa Rais Kikwete atataka kumuondoa yeye yupo tayari kuondoka.
Mhando aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Tanesco kwa miaka mitano imekuwa ikipata hati safi za mahesabu na hivyo hakuna sababu ya watu kumshutumu kutokana na utendaji wake.
“Mimi niseme tu kitu kimoja kwamba kuna watu hawanitaki niwepo pale ndiyo maana haya yote yanatokea licha ya kujitahidi kuueleza umma kuhusu hali ya shirika lao na upatikanaji wa umeme,” alisema.
Alisema ripoti ya CAG haijawahi kumtaja kuhusika na kashfa yoyote tangu aingie Tanesco miaka miwili iliyopita na kwamba juhudi za kulisukuma mbele shirika zinafanywa usiku na mchana.
“Mimi wakati mwingine nafanya kazi usiku na mchana na sipati usingizi, lakini kama mwajiri wangu ataona sifai katika nafasi hii mimi niko tayari kuondoka,” alisema Mhando.
Mhando alikanusha madai kwamba Tanesco ilifanya manunuzi makubwa kinyume cha utaratibu yanayofikia Sh. bilioni 600 kama ilivyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari.
Aliweka wazi kuwa manunuzi yaliyofanyika na ambayo CAG anayajua ni Sh. bilioni 258.
Aidha, Mhando alisema gharama za ujenzi wa lango la bwawa la Mtera ambazo zilizua utata Tanesco ilikuwa imetenga Sh. milioni 65 kwa ajili ya kazi hiyo, lakini POAC iliona kiasi hicho ni kidogo na kutaka kiongezwe.
Alifafanua kuwa POAC iliishauri Tanesco kuongeza kiasi hicho cha fedha ambapo kiliongezwa na kufikia Sh. bilioni 1.8 ambazo hata hivyo, hadi sasa bado zipo na kwamba hazijatumika.
“Hizi fedha zinazozungumziwa zipo wazi na namna zilivyopatikana, inajulikana na baada ya kupatikana tunazo wala hatujazitumia,” alisema.
Kuhusu kuondolewa kwa jenereta nyumbani kwake kama ilivyoagizwa na POAC Machi mwaka huu, Mhando alisema suala hilo limekataliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.
“Suala hili lipo kwenye mkataba wangu wa ajira ambapo mimi kama mkurugenzi mtendaji ninatakiwa kuwekewa jenereta sasa kitu kama hiki unawezaje kukiondoa?” alihoji Mhando.
Akizungumzia matumizi mabaya ya manunuzi yanayolalamikiwa kwa Tanesco, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, ambaye jana alifanya kikao na Mhando, alisema ripoti ya CAG haijalitia hatiani shirika hilo.
Zitto alisema alinukuliwa vibaya na ukweli ni kwamba Tanesco haina ubadhirifu na imekuwa na hati safi ya mahesabu kwa miaka mitano mfululizo.
Katika mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyofanya Rais Kikwete aliwaacha mawaziri sita na manaibu mawaziri wawili.
Walioachwa ni Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na naibu wake, Athuman Mfutakamba; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Afya, Dk. Hadji Mponda na naibu wake, Dk. Lucy Nkya pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami.
Katika mabadiliko hayo makubwa kuwahi kufanywa na Rais Kikwete yakikaribiana na yale ya Februari mwaka 2008 ambayo yalifanywa baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu, pia aliwapangua mawaziri wanane wa zamani kwa kuwapangia wizara nyingine, kuteua mawaziri saba wapya, manaibu sita kubadilishwa wizara pamoja na kuteua manaibu mawaziri 10 wapya.