



Leo wananchi wenye sifa ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha, watamchagua Mbunge wao.
Pamoja na uchaguzi huo, tunatambua kuwepo uchaguzi mwingine wa madiwani unaofanyika kwenye kata mbalimbali hapa nchini, ingawa macho na masikio ya Watanzania wengi, yameelekezwa Arumeru Mashariki.
Tumeshuhudia kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki zikiwashirikisha viongozi waandamizi wa kisiasa nchini. Vyombo vya habari ‘vilivyohamia’ huko vimekuwa chachu ya kuufahamisha umma kuhusu matukio mbalimbali yaliyotokea katika hatua zote.
Vyombo hivyo vilianza kutoa taarifa tangu hatua za mchakato wa kuwapata wagombea kupitia vyama vya siasa, kutangazwa na vyama husika na hatimaye kuanza na kufungwa kwa kampeni zao.
Kupitia vyombo vya habari, umma wa ndani na nje ya nchi umejua kila tukio lililo jema na lisilo la kiustaarabu, lililotokea Arumeru Mashariki. Pamoja na kasoro kadhaa zikiwemo za kujeruhi na kujeruhiwa, uchaguzi huo unafanyika leo.
Tunatambua kwamba yapo mambo ya kujifunza kutokana na chaguzi ndogo ukiwemo wa Arumeru Mashariki unaofanyika leo. Kama taifa tunapaswa kuelekeza jitihada zaidi katika kuendeleza yaliyo mema na kuachana na mambo maovu na yasiyokuwa ya kimaadili.
Kwa hali hiyo, tunaziasa pande zinazojumuisha wadau wote katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki na kwingine kunapofanyika chaguzi ndogo za udiwani, kuhakikisha vurugu zinaepukwa, ili kufikia ukomo wa kuwapata wawakilishi wa wananchi kukiwa na amani na utulivu.
Haitakuwa na maana kwa nchi ikiwa tumepita hatua zote za uchaguzi kwa salama, japo kumekuwepo matukio machache ya uvunjifu wa amani, lakini ifike hatua, kufanyika kwa uchaguzi huo kuibue tafrani zinazoweza kuzuilika.
Si jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama peke yao kuhakikisha vurugu zinaepukwa katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, bali ni jukumu letu sote.Vyombo hivi vinatekeleza wajibu huo ikiwa kunakuwa na dalili ama kutokea kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.
Ni jambo linaloeleweka kwamba kabla kuvunjika kwa amani hakujatokea, vipo viashiria vyake vinavyofanywa na watu ambao kwa namna yoyote, ni wadau katika uchaguzi huo.
Kwa hali hiyo tunawasihi wadau wote kama vile vyama vya siasa, wagombea, msimamizi wa uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vya habari, kuhakikisha kuwa kilichobaki ni uamuzi wa wapiga kura wa Arumeru Mashariki.
Wapiga kura hao ndio wenye dhamana pana ya kuhakikisha mgombea aliye chaguo lao, anatangazwa mshindi. Hapo watajitokeza hadharani, wakipiga muziki, wakipeperusha nembo za chama husika, wakimnyanyua juu mshindi, wakisherehekea.
Itakapotokea hali hiyo, furaha haitakuwa kwa wakazi wa Arumeru pekee, furaha haitakuwa kwa mkoa wa Arusha pekee, furaha haitakuwa kwa viongozi, wanachama na washirika wa chama anachotoka mshindi, bali kwa Watanzania kwa ujumla.
Kwa maana uchaguzi unapomalizika pasipo vurugu, ndugu, jamaa na marafiki waliopo jimboni humo wataendelea na shughuli zao kama kawaida. Watazalisha bidhaa, watatoa huduma, watahudumia na kukuza uchumi wa kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Haijajulikana ni nani ataibuka mshindi kwa maana kura zitaendelea kupigwa hadi jioni ya leo, kisha zitahesabiwa ili kila mgombea wa kila chama kujua kiasi cha 'fungu' lake.
Msisitizo wetu hapa ni kwamba kila mdau atekeleze wajibu wake kwa misingi ya haki na usawa, huku ukweli ukitawala na kuepuka ulaghai ama ghilba zinazoweza kusababisha vurugu.
Kwa upande mwingine, vyama vya siasa na wagombea wao viwe tayari kuyapokea matokeo kwa njia ya amani na utulivu. Kwa maana faida iliyo kuu katika mfumo wa chaguzi hapa nchini, ni kuwepo mlango wa kutafuta haki mahakamani.
Inawezekana mmoja ama wagombea zaidi wasiridhishwe na matokeo. Wanaweza kuwa na ushahidi wa kwa nini hawaridhiki. Hapo ndipo wengine (kutokana na uzoefu) huanza kuwachochea wananchi.
Wakati tukisisitiza haki na ukweli kutawala utangazaji matokeo yaliyo halali, inawapasa wadau kuepuka uchochezi ikiwa hawataridhishwa na matokeo hayo.
Kuwachochea wananchi kufanya vurugu ni kuchochea uvunjifu wa amani, badala yake subira inatakiwa itawale ili kama kuna haja ya kuchukua hatua zaidi za kisheria, iwe hivyo.
Tunautakiwa kila heri uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki, tunazitakia heri chaguzi ndogo za udiwani zinazofanyika leo.