Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba wajifua kuzoea baridi kali Setif

5th April 2012
Print
Comments
Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Simba

Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Simba, jana mchana waliwasili mjini Setif nchini Algeria na mara moja wakaanza mazoezi kwa nia ya kuzoea hali ya baridi kali kabla ya mechi yao ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya wenyeji ES Setif itakayochezwa kesho nchini humo.

Simba ilianza mazoezi juzi ikiwa jijini Algiers baada ya kukataa kusafiri kwa basi kuelekea Setif kufuatia kanuni za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwalazimisha wenyeji kuwasafirisha kwa ndege kuelekea katika eneo lenye umbali unaofikia kilomita 200.

Jana jioni, wachezaji Simba walifanya mazoezi pia kwenye Uwanja wa Mei 8, 1945, ambao ndio utakaotumika kwa mechi yao itakayochezwa kuanzia saa 12:00 jioni, sawa na saa 2:00 usiku ya Tanzania.

Katika kuhakikisha kwamba wanajiweka kwenye mazingira ya usalama na kukwepa hujuma kutoka kwa wenyeji, viongozi wa Simba walioondoka nchini jana asubuhi walibeba vyakula mbalimbali kwa ajili ya msafara wao, ikiwa ni pamoja na mchele, maharage na maji ya kunywa.

Vyakula hivyo vilisafirishwa jana kuelekea Algeria na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'.

Ikiwa Setif, Simba imefikia katika hoteli ya Zidane iliyopo katikati ya mji na kuna taarifa kuwa hoteli hiyo ni miongoni mwa vitega uchumi vya mwanasoka bora wa zamani wa dunia, Zinedine Zidane ‘Zizzou’, ambaye ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria.

Kwa mujibu wa CAF, mechi ya Simba dhidi ya Setif itachezeshwa na waamuzi kutoka Tunisia huku kamisaa wa akiwa ni raia wa Gabon.

Simba iliyoshinda 2-0 katika mechi yao ya kwanza, itafuzu kwa raundi inayofuata ikiwa itapata sare au kufungwa kwa tofauti ya bao moja.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles