Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Papic awaaga wachezaji Yanga

21st April 2012
Print
Comments
Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadian Papic

Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadian Papic amewashukuru wachezaji kwa ushirikiano waliompa tangu alipojiunga na timu hiyo mwanzoni mwa mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Bara msimu huu.

Papic ametoa shukrani hizo ikiwa ni sehemu ya kuwaaga wachezaji hao kwa kuwa anatarajia kuondoka mara baada ya mkataba wake kumalizika Jumanne.

Akizungumza na NIPASHE jana, Papic alisema pamoja na klabu hiyo kuwa na matatizo mengi, alikuwa akipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wachezaji wake katika kipindi chote alipokuwa akiwafundisha.

"Nimemaliza kazi yangu hapa," alisema Papic.

"Nawashukuru sana wachezaji kwa ushirikiano wao... kwa sasa naangalia mambo mengine lakini si kubaki hapa nchini."
Alisema hata kama uongozi wa Yanga utampa mkataba mpya, hayuko tayari kubaki Yanga.

"Lazima ufanye kazi sehemu ukiwa na furaha ma utaona kazi yako inaenda vizuri. Kwa nini nibaki Yanga wakati sina furaha napo?" aliuliza Papic. "Naondoka na sitakuwa tayari kubaki hapa."

Aidha, Papic alisema kuwa lazima Yanga imalize matatizo yake na kufanya maandalizi ya mapema kama inataka kutwaa ubingwa wa Bara msimu ujao.

Alisema timu inapofanya maandalizi mazuri ndipo inapotengeneza nafasi ya kupata matokeo mazuri kwenye michezo mbalimbali.

Papic alisema Yanga inapaswa kukaa chini ya kutafakari walipokosea na kuchukua hatua ya haraka ya kurekebisha makosa hayo.

Yanga ilivuliwa ubingwa wa Bara katikati ya wiki baada ya mchanganyiko wa kipigo cha pili ndani ya siku nne na kutupwa kwa rufaa kumaanisha kuwa haitoweza kuifikia Simba yenye pointi 56 mpaka sasa.

Papic alisema Yanga wakiyaendeleza mambo waliyofanya msimu huu wa ligi kuu ni vigumu kupata ubingwa, na wataendelea kuwashuhudia wapinzani wao wakichukua kombe.

Katika hatua nyingine, Papic alisema kuwa Yanga walipoteza ubingwa wao baada ya kupokonywa pointi tatu za ushindi dhidi ya Coastal Union.

Alisema kitendo cha kupokonywa pointi kilishusha morali ya wachezaji wake na kuwataka viongozi kutorudia makosa waliyoyafanya na kupelekea kupokonywa pointi hizo.

Papic atakuwa kwenye benchi la ufundi la klabu yake kwa mara ya mwisho kesho kwenye mchezo dhidi ya Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Taifa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment