Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

APRM: Italeta mabadiliko ya utawala bora au geresha

28th March 2012
Print
Comments

Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM- Tanzania), umemkabidhi rais Jakaya Kikwete, ripoti mpya inayoonesha hali ya Utawala Bora nchini kwa mujibu wa maoni ya wananchi na wataalamu mbalimbali.

APRM  ni mpango endelevu uliobuniwa na marais wa Afrika katika kikao chao cha mwaka 2002 ambapo walikubaliana kuweka utaratibu wa kila nchi kuanzisha taasisi hiyo na kisha kuipa jukumu la kufanyakazi ya kujitathmini mara kwa mara katika nyanja za utawala bora. Mkataba huo wa Afrika unaonesha kuwa nchi hutathminiwa kila baada ya miaka minne.

APRM pamoja na malengo yake kuonekana kuwa mazuri lakini kwa upande mwingine inaweza kuonekana kitu kisichokuwa msaada kwa wachambuzi wa mambo kutokana na mambo nitakayoyataja kwenye makala hii.

Kuna sababu nyingi za kutilia shaka ufanisi ama faida za mpango huu kama kweli nchi za Afrika zimedhamiria kweli kujitathmini ama zimeanzisha mpango huo kwa lengo la kuwafurahisha wafadhili.

Mfano fedha za uendeshaji wa mpango huo hutolewa na serikali husika, yaani serikali inawalipa fedha za uendeshaji watu wanaoifanyia tathmini.

 Kwa taasisi iliyofadhiliwa na serikali kutekeleza wajibu huo, Je inaweza kufanyakazi zake kwa uwazi na kutenda haki, mfano je, inaweza kuwa huru kuandika ripoti kwamba kiwango cha utawara bora ni hafifu Tanzanaia? Ili hali kesho yake itakwenda kubembeleza fedha za kuendeshea ofisi.

Hapo lazima kuna mambo ya kufanyia kazi kama kweli serikali za Afrika zinataka mpango huu uwe na maana zaidi, ulete mabadiliko ya kweli katika suala la demokrasia ama iwekwe wazi kwamba mpango huo umeanzishwa kwa ajili ya kuongeza ajira.

Kuna jambo lingine linaloshangaza  katika mpango huu, mfano APRM Tanzania ikishafanya tathmini  na kuandaa ripoti yake inalazimika kuiwasilisha ripoti hiyo serikalini ili ifanyiwe mapitio na kisha warudishiwe na ndipo wanaweza kuipeleka Makao Makuu Afrika Kusini.

Sasa hatua hiyo inamaanisha kwamba kama katika ripoti hiyo serikali imekosolewa katika mambo mengi ni dhahiri itayarekebisha na kuyaondoa kabisa, kwa lugha nyepesi ni kwamba serikali itaipamba ripoti hiyo ili itakaposomwa Afrika Kusini Tanzania ipigiwe makofi na kushangiliwa.

Hapo kwa mtazamo wangu haijakaa sawa, ni vyema na haki APRM Tanzania ikishaanda ripoti yake iwasilishwe kama ilivyo Afrika Kusini ili wahusika wasutwe, wasemwe wajirekebishe la sivyo mpango huo hautakuwa tofauti na michezo tunayoangalia kila siku kwenye luninga.

Barani Afrika ndiko kwenye migogoro isiyoisha kiuongozi, uroho wa madaraka na marais kujaribu kung'ang'ania madaraka hata muda wao wa kikatiba unapomalizika.

Mapinduzi ya kijeshi nayo yamekuwa maisha ya kawaida barani Afrika, ni nadra sana kusikia mapinduzi ya kijeshi nchi za Ulaya na Marekani.

Ung’ang’anizi wa madaraka na vurugu za kisiasa zimekuwa zikitokea zaidi kwa nchi za Afrika kutokana na mazoea ya viongozi kutaka kusalia madarakani hata kwa kumwaga damu ya maelfu ya raia wake.

Swali, ripoti hiyo ya utawala bora inaweza kuwa na mchango wowote katika kuwajenga waafrika hasa viongozi walioko madarakani kuheshimu sanduku la kura na mihula iliyowekwa kikatiba.

Kuheshimu Katiba za nchi zao kwa kuhakikisha wanaondoka madarakani mara wanapomaliza mihula yao, ipo mifano mingi ya marais waliochakachua Katiba ili wasalie madarakani.

Katika baadhi ya nchi yakatokea machafuko makubwa na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha, wengine wakibaki wakiwa walemavu na wengine kulazimika kuzikimbia nchi zao.

Hayo yamekuwa ni maisha ya kawaida kabisa kwa nchi nyingi za Afrika kwani wengi wanaoingia madarakani wakishindwa wanatengeneza namna ya kusalia madarakani.

Ipo mifano mingi, Ivory Coast, ambapo aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo alijaribu kung'ang'ania Ikulu licha ya Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) ya nchi hiyo kumtangaza mpinzani wake mkuu, Alassane Ouattara kuwa mshindi halali.

Omar Bongo wa Gabon alikaa madarakani tangu Novemba mwaka 1967 hadi alipofariki dunia na nafasi yake kurithiwa na mwanaue wa kiume, Ali Ben Bongo.

Muammar Gaddafi naye alikaa Ikulu ya Tripoli tangu achukue madaraka mwanzoni mwa miaka ya 1969 hadi alipouwawa baada ya maandamano ya wananchi yaliyodumu kwa mwaka mzima.

Yoweri Museven, amekaa madarakani tangu mwaka 1986 hadi leo hii na amebadili Katiba kuondoa ukomo wa urais hali inayoweza kumfanya awe rais wa maisha.

Robert Mugabe, aliingia madarakani mwaka 1980 hadi leo hii na umri wake wa miaka 88 anasema bado ananguvu za kuwatumikia wazimbabwe na ameomba muhula mwingine.

Ben Ali wa Tunisia, naye ni miongozi  mwa viongozi waliokuwa madarakani kwa muda mrefu tangu mwaka 1987 na aling'olewa mwanzoni mwa mwaka 2011 kwa maandamano ya wananchi.

Rais wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos, aliingia madarakani mwaka 1976 baada ya miaka minne ya vita kali kati ya chama UNITA na waasi ambayo ilikoma mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa kundi hilo Jonas Savimbi.

Rais wa Cameroon, Paul Biya, 76 aliingia madarakani 1982 akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake, Ahmadou Ahidjo, na mwaka 2004 alifanikiwa kuchaguliwa tena kushinka madaraka kwa kipindi cha miaka saba.

Rais Denis Sassou Nguesso wa Afrika ya Kati, huyu aliingia madarakani mwaka 1979 lakini wakati wa mfumo wa vyama vingi vinaingia nchini mwake alipoteza urais mwaka 1992 dhidi ya mpinzani wake Pascal Lissouba.

 Alifanikiwa kurudi madarakani mwaka 1997 baada ya vita dhidi ya utawala wa Lissouba na mwaka 2004 alifanikiwa kuchaguliwa kidemokrasia kuongoza tena taifa kwa kipindi cha miaka saba.

Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea, aliingia madarakani mwaka 1979 .

 

Hosni Mubarak, aliyeingia madarakani mwaka 1981 naye ni mfano wa viongozi wa madikteta ambaye alitaka kujigeuza rais wa maisha ya Misri na  ambaye alishindwa kusoma alama za nyakati na kung'olewa kwa maandamano ya umma. 

 

Abdulaye Wade, wa Senegal anamiaka 85 na amekaa madarakani mihula miwili tangu mwaka 2000 lakini amefanya ujanja ujanja kutaka aendelee muhula wa tatu hali iliyozua mtafaruku mkubwa katika taifa hilo linalosifika kwa utulivu kwa miongo kadhaa.

Hata hivyo, pamoja na ujanja ujanja wake, ameangushwa katika uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika wiki iliyopita.

Ali Abdulah Saleh wa Yemen, yeye alikimbia nchi Februari mwaka huu baada ya maandamano ya mwaka mzima ya kutaka mabadiliko ya uongozi.

Baada ya kujifanya kaziba masikio na kudharau sauti ya umma hatimaye alifungasha virago na kwenda zake Marekani baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu.

Hiyo ni mifano michache, wako marais wengi wa aina hiyo.

Hivi karibuni serikali ilialika jopo la wataalamu wa masuala ya utawala bora (CRM) kutoka makao makuu ya Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), kuitembelea Tanzania Machi 2, hadi 23, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mtendaji wa APRM, Rehema Twalib, jopo hilo lilijumuisha wataalamu wa fani anuai kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ambapo walikuja kwa ajili ya kufanya mashauriano na wadau mbalimbali wa masuala ya utawala bora.

Jopo lilitakutana na viongozi wa serikali, wabunge, wawakilishi wa vyama vya kiraia, vyombo vya habari, wasomi wa vyuo vikuu, vyama vya wafanyakazi, asasi za kijamii zilizoko vijijini na wabia wa maendeleo, kwa lengo la kushauriana juu ya changamoto za utawala bora na kutoa mapendekezo hatua zipi zinaweza kuchukuliwa.

Ilisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 kati ya 54 za Afrika zinazoshiriki katika mchakato wa APRM ambapo ilisaini makubaliano ya kujiunga Julai 23 mwaka 2004, na Bunge kuridhia kushiriki mchakato huu katika kikao chake cha Februari mosi, 2005.

Iliongeza kuwa hadi sasa Tanzania imekamilisha mchakato wa kujitathmini wa ndani ya nchi ambapo ripoti ya ndani ya nchi na mpango kazi wake vilivyokuwa vimekamilishwa mwaka 2009 vilihuishwa mwaka jana.

Mchakato wa APRM hurudiwa kila baada ya miaka minne ili kuzipa nchi za Afrika fursa endelevu ya kutatua kero za utawala bora.

Ripoti za APRM kutoka kila nchi mwanachama mbali ya kuwasilishwa mbele ya wakuu wa nchi zinazoshiriki mpango huo kwa ajili ya kupeana uzoezi na kushauriana pia huandaliwa mpangokazi wa kitaifa wa miaka mitatu mitatu kwa ajili ya Serikali husika kufanyiakazi changamoto zilizobainishwa. Kwa mujibu wa mkataba, utafiti huu hurudiwa kila baada ya miaka minne.

Katibu Mtendaji wa Mpango huo, Rehema Twalib anasema wameamua kutenganisha ripoti ya mpango huo katia ya Tanzania Bara na Zanzibar, baada ya kupokea maoni mengi kutoka Zanzibar kwamba ripoti yao kwa upande wa Zanzibar itenganishwe.

Alieleza kwamba baada ya ripoti hiyo kukamilika, Rais wa Jamhuri ya Muungano ataiwasilisha katika mkutano utakaowashirikisha viongozi wa nchi Barani Afrika ili ripoti za nchi mbali mbali ziweze kujadiliwa na baadaye nchi hizo kuchukua hatua za utekelezaji wake.

Hivi karibuni timu ya wataalamu kutoka makao makuu ya APRM walikuwa nchini kwa wiki tatu kuhakiki ripoti ya ndani ya nchi kuhusu utawala bora iliyokuwa imeandaliwa na wataalamu wa APRM Tanzanaia.

Akiagana na wataalamu hao, Rais Kikwete akaahidi kutekeleza mapendekezo yatakayotolewa na  mpango huo kwa maslahi ya nchi.

 

Akasema serikali inayasaubiri kwa hamu mapendekezo ya watalamu hao ili serikali nayo iwapatie majibu ya nini imefanya katika utawala bora. 

 

Wataalamu hao kwa muda waliokuwa nchini wamekutana na wadau mbalimbali kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles