Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ligi 9-Bora yazidi kushika kasi Morogoro

6th April 2012
Print
Comments

Timu ya JKT Mlale ya Ruvuma ilionyesha kiwango kizuri na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tabora huku Rhino ya Tabora ikiibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Transit Camp ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa fainali za 9-Bora ya Ligi Daraja la kwanza zinazoendelea kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Katika mechi ya kwanza iliyoanza saa 8:00 mchana, mshambuliaji Igogo Maganga aliifungia Mlale bao la kuongoza katika dakika ya 5 kwa shuti kali. Mlale waliendelea kulishambulia lango la Polisi na dakika tano baadaye wakafunga bao la pili kabla Polisi kufunga goli la kufutia machozi.

Rhino waliofungwa bao 1-0 katika mechi yao iliyopita dhidi ya Polisi Tabora, jana walijirekebisha na kushinda kwa idadi hiyo hiyo ya magoli dhidi ya Transit Camp katika mechi yao ya pili iliyochezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Amri Sambiga ndiye aliyewafungia Rhino bao la ushindi katika dakika ya 16 baada ya kupata krosi safi kutoka kwa Venance Genda na kuunganisha wavuni kwa kichwa.

Timu nne zitakazomaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Jumamosi zitapanda daraja na kucheza ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Mechi mbili huchezwa kila siku na hadi sasa, ligi hiyo imekuwa ngumu kutabirika kwani imekuwa na matokeo tofauti ambapo timu kadhaa zilizoshinda zimejikuta pia zikiangukia pua katika mechi zao zilizofuata.

Timu pekee ya kiraia katika michuano hiyo, Mbeya City ilianza kwa ushindi wa kishindo wa 3-0 dhidi ya Trans Camp ya Dar katika mechi yao ya ufunguzi, lakini mambo yaliwageukia katika mechi iliyofuata baada ya kuchapwa 2-0 na majirani zao Prisons ya Mbeya.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment