Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wachumba vigeugeu wanavyotishia ndoa!

20th May 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, wakati bado tunasubiri maoni na ushauri kuhusu mada ya wiki iliyopita iliyojadili kisa kilichobeba ujumbe, ‘Mke wangu anachat na wanaume, nakonda sijui nichukue hatua gani!, tuone kisanga kingine.

Huyu ni kijana anayelalamika kusalitiwa na mchumba wake. Ameeleza kisa chake kwa ujumbe kadhaa kupitia simu ya kiganjani. Anaanza hivi;

“Nashindwa nielezeje, nimeishi na mpenzi wangu baada ya kutoka kwao kuja kunitembelea. Alipohitimu elimu ya sekondari mwaka jana nimekaa naye miezi minne kumbe alikuwa na mwanaume mwingine.

Nilikamata ujumbe wa simu(sms) aliyokuwa akimtumia mtu wake ikisema; “mchumba wangu uliniahidi mwaka 2013 tutaoana sasa imekuwaje unasema tuachane nakuomba nisamehe bado nakupenda na nahitaji uwe baba wa watoto sina mwingine anayefaa ni wewe niliyekuchagua nakupenda sana nitakuja bado shangazi anaumwa sana”. Baada ya kugundua kuwa nimefahamu akaanza kuwasiliana na dadake kuwa aende huko Dar akarudie shule.

Mimi pale sikuwa na maneno mengi zaidi ya kumwambia aende amsubiri Yule waliyeahidiana baada ya mwaka mmoja waoane. Naye akanijibu eti hakuwa na nia ya kuishi naye eti ile sms ilikuwa ya uwongo.

Kesho yake akaaga anakwenda Dar kwa dadake huku akiniahidi atarudi tuoane na mimi pale sikuwa na pressure naye kwani baada ya kumkuta na sms ile nilishukuru Mungu kwa kuniepusha na ajali kwani kama ningeishi naye ningepata matatizo mengi.

Lakini sikuwa na ubaya naye. Nikijaribu kumtafuta kwenye simu mara nyingi yuko hewani lakini cha ajabu nilipiga simu ikapokewa na mwanaume usiku saa 6 akidai simu iko kwenye moto mwenye nayo yuko mbali mpaka kesho na kesho yake tena nikampigia kumuuliza akaniambia ni kaka zake wakati siyo kweli kwani kaka zake wako huku Mwanza.

Nilivyopeleleza zaidi akadai ni mwenzake. Kiukweli niliumia sana nikatoa ile sauti ya kutaka kulia lakini alichoniambia alisema kuwa we ulikamata sms ukachukia nikajua umeniacha. Nikamwambia, kumbuka tulikotoka tumesaidiana mambo mengi wakati uko shule. Akaniambia siyo wewe bali wengi wamefanyiwa hivyo, vumilia utapata mwingine.

Niliumia sana ila kaka yake alinipa moyo wa uvumilivu na mpaka sasa sijatuliza akili kusema nimpigie anipe ukweli wa mwisho. Nilimpenda sana kwa sababu ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kuwa na mchumba toka nianze kupenda na hapa nilipo nawaogopa mabinti hata nikimtafuta anaweza kunifanyia hivyo hivyo kama huyu wa kwanza(Naitwa Alphonce Rutta-Mwanza).

Mpenzi msomaji, nadhani kijana Rutta lipo jambo ambalo Mwenyezi Mungu amemuepusha. Yule binti japo alidhani ni chaguo sahihi lakini akaonyeshwa kuwa siyo mwaminifu kwake kwani tayari alikuwa na mahusiano mengine.

Namshauri atulie huku akimtanguliza Mungu kwani mke mwema hutoka kwa Mungu kama maandiko matakatifu yanavyotuambia. Hakuna sababu ya kuhangaika naye tena hasa baada ya kukiri anaye mtu mwingine na pia ujumbe ule wa simu ulidhihirisha wazi kuwa anaye mtu mwingine. Ama kwa hakika maisha yamejaa udanganyifu mwingi na mitego isiyoteguka kirahisi. Na zaidi wachumba vigeugeu ni tishio katika ndoa nyingi zinazotarajiwa kufungwa.

Mpenzi msomaji, kabla sijakamilisha makala haya hebu tusikie maoni ya wasomaji zaidi kuhusu mada ya wiki moja iliyopita ikijadili maoni ya msomaji aliyelalamika kuhusu vituko vya wanaume wa Moshi kule mkoani Kilimanjaro. Bado wamejitokeza wachangiaji zaidi wa mada ile, na yafuatayo ni maoni ya baadhi yao.

Yupo msomaji ambaye ametuma maoni yake kupitia email ya safu hii na inasomeka hivi;

“Kwa kweli kuhusu mada ya wanaume wa Moshi naomba kutoa mchango wangu kidogo. Tatizo kubwa hapa ni watu kutokuwa na malengo chanya na wengine kuwa malengo hasi.

Fikiria unaoa mke wako halafu unakuja jua ya kuwa anataka kukufanya ATM kwa ajili ya ndugu zake ambapo watoto wako hawatakuwa na haki yeyote kule kwa wajomba punde ukipiga nyama chini......Ndugu wa mke kuonekana wa maana sana nyumbani kwako kuliko wako.....hapa mume hutakiwa kuwa na ujasiri wa kusema NO....wengine huruhusu yatima tu na wakati wa ugonjwa...akitaka msaada akae pale kwa babake umfuate kwani kuendekeza hii ni dharau kwa mzazi mtu punde apatapo mazuri.

Wanawake makabila tofauti na Wachagga ndio walalamikaji wazuri kwani wao huja kwa kujua Mangi mtafutaji mzuri ...hivyo ukibana POINT huanza kilio kwani wengi hubweteka na hawataki kufanya kazi ila ni kufuja na kusingizia misiba na safari za kila mara kwao na huko kwenda kuonyesha umaarufu.

Sikatai kusaidia, la hasha, ila kuwe zaidi na REALITY of THE MATTER(ukweli wa jambo).........hapa dada Wingia napenda kusema kuwa hata sisi Wachaga tuna yetu na huaminisha na kuwa mtoto toka nje ya ndoa hujaliwa zaidi na huwa na akili SANA ya mafanikio na hata ile imani ya LAANA za kurithi na husema endapo itatokea basi huyu atakusaidia kuendeleza ukoo na hata kukulea pale itakapo tokea.

Angalia familia kibao za uchaggani utakuta kila moja ina mtoto au watoto wa aina hii.....Wengine hujulikana baada ya mzazi kufa. Lakini kwa akina mama punde itokeapo..........DNA ya Wachagga ni husema huyo mtoto hatakuwa sawa na familia ile...huwa mtukutu kupita kiasi  na hupenda kutoroka nyumbani.

Je nirudi kwenye chimbuko la Penzi la Wachagga......Wengi hawajaandaliwa kuoa au kuolewa........Soma kitabu cha MAISHA YA MCHAGGA DUNIANI NA AHERA .....Utajua mengi sana na miiko yake.

Hakuna mwanamke aliye jasiri kama REBEKA ambaye alimtetea mumewe mpaka dakika ya mwisho hadi Mfalme Daudi alimtamania.

Hii ina maanisha nini? Sijui cha zaidi bali ni kusema ya kuwa tunanakili na kubandika(WE ARE COPYING AND PASTING)  maisha ya Kizungu.

Kibaya zaidi yale ya kusema nimempokea    BWANA......nayo yana yake mabovu ndani ya nyumba........lakini yote tisa na kumi ni kusema ya kuwa FARANGA(pesa) nayo ni imekuwa mbaya ndani ya ndoa nyingi. Naomba niishie hapo. Ni mimi Meku wa Kimarangu”.

Msomaji mwingine anachangia mada ile kupitia ujumbe simu ya kiganjani na kusema; “nashukuru kwa mafunzo kupitia Maisha ndivyo Yalivyo. Mimi naishi Zanzibar, sisi ni wachagga tumefunga ndoa. Lakini mume wangu amenichosha kwa kutokuwa mwaminifu.

Yuko radhi atumie gharama yoyote ili nisafiri niende Moshi apate nafasi ya kusaliti na fuska wa Kitanga. Hapo hapo ni wa kwanza kujifanya ni mwema na kuona wanaume wenzake ni ndio wakosaji bila kujali sisi ni wagonjwa. Nami nimesema namwachia Mungu iko siku huyo kimada wake atasaga meno. Dada Flora narudia kusema wanaume wa Kichagga wengine siyo binadamu ni wauaji hususani Rombo. (Mama Liana Litiku).”

Kwa leo niishie hapa. Zaidi kama unao ushauri, maoni kuhusu kijana wetu Rutta kwenye utangulizi wa makala haya usisite kuwasilisha hapa tujadili kwa pamoja. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa. Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles