



Siku mbili baada ya aliyekuwa mwenyekiti Yanga, Lloyd Nchunga, kujiuzulu wanachama wa klabu hiyo wanakusudia kuiomba serikali kuchunguza mahesabu ya kipindi chote cha utawala ulioanguka.
Akizungumza na Waandishi wa habari klabuni jana, katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga Ibrahim Akilimali alisema wajumbe wake na vijana wa klabu hiyo watawasilisha barua Wizara ya Michezo kuomba mkaguzi wa mahesabu kwenda kufanya kazi hiyo klabuni hapo.
Uchunguzi wa mahesabu ya fedha serikalini ni jukumu la Mdibiti na Mkaguzi Mkuu, CAG, ambaye ripoti yake ya mwaka jana ilipelekea kufumuliwa kwa Baraza la Mawaziri na Rais JK hivi karibuni.
Akilimalia alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuwa na mashaka ya kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha na mali za klabu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuingia madarakani kwa uongozi wa Nchunga.
"Ndugu zangu pamoja na kuwa Nchunga amejiuzulu, kazi bado inaendelea," alisema Akilimali ambaye alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Nchunga anang'oka.
"Tunaandaa barua ambayo tutawasilisha Wizarani Jumatatu kuomba itume mkaguzi wa kuja kufanya ukaguzi hapa klabuni kwetu ili tujiridhishe kuwa hakuna ubadhirifu wowote wa mali na fedha za klabu yetu." Akilimali alisema kuwa suala la ubadhirifu ni sababu mojawapo kubwa iliyofanya baraza lake pamoja na vijana wa klabu hiyo kumlazimisha Nchunga kujiuzulu uenyekiti wa klabu hiyo.
Wakati huo huo, katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga Ibrahim Akilimali alisema kuwa wanachama wa klabu hiyo wamepokea kwa furaha taarifa ya kujiuzulu kwa Nchunga na kuwataka kuanza tena kulipia ada za uanachama wakati wakisubiri taratibu nyingine zinazoendelea.
"Kuna mambo tuliyasitisha wakati Nchunga alipokuwa ameng'angania madaraka, jambo moja wapo ni pamoja na uilipaji wa ada za uanachama," alisema na kueleza zaidi, "sasa nawaomba wanachama wenzangu turudi kwenye msatari, tuendelee kulipa ada kwa sababu tayari Nchunga ametoka madarakani."
Naye Mwenyekiti wa vijana wa klabu hiyo, Bakili Makele, alisema baada ya Nchunga kujiuzulu na kuiacha timu mikononi mwa wazee na vijana, wataikabidhi timu hiyo kwa wadhamini wa klabu hiyo ambao ni mama Fatma Karume wa Zanzibar na Francis Kifukwe.
"Kwa kipindi hiki tunachosubiri maelekezo ya TFF, timu yetu itakuwa kwenye mikono salama ya wadhamini wetu wa klabu hii, wao wataiongoza timu yetu kufanya usajili pamoja na kushiriki vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Kagame," alisema Makele.
Yanga ni bingwa mtetezi wa Kombe la Kagame la klabu bingwa za Afrika Mashariki na Kati linalotarajiwa kuanza jijini Dar es Salaam mwezi ujao. Aidha, Makele alisema pamoja na Nchunga kuondoka madarakani kwa kutangaza kujizulu, wanachama wanataka kupata taarifa ya benki ya kipindi cha miaka miwili.