


.jpg)
Benki ya CRDB imefanikiwa kuongeza utoaji wa mikopo yake kwa asilimia 27, kufikia Sh. bilioni 1.4 kutoka Sh. bilioni 1.1 mwaka 2010.
Aidha sekta ya Kilimo imeongoza kwa kuchangia asilimia 30 ya mikopo yote iliyotolewa na benki hiyo, huku ikifuatiwa na Biashara na Viwanda kwa asilimia 14.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB nchini, Dk. Charles Kimei, wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa benki hiyo, uliofanyika jijini Arusha.
Dk.Kimei alisema mbali na sekta hizo pia alitaja sekta nyingine zilizochangia ukuaji wa mikopo hiyo kuwa ni mikopo binafsi asilimia 12, utalii, hoteli na migahawa asilimia nane, wakala wa masuala ya kifedha asilimia saba, upangishaji majengo na ujenzi asilimia sita, mawasiliano na uchukuzi kila moja asilimia saba, huduma za kijamii asilimia sita, uzalishaji na usindikaji asilimia tatu na uchimbaji wa madini na kokoto asilimia moja.
Alisema mapato yote yatokanayo na riba ya mikopo yote yalikuwa Sh. bilioni 148, ikiwa juu zaidi ya bilioni 137 katika mwaka 2010, ikiwakilisha asilimia 58 ya jumla ya pato la uendeshaji. Aidha kwa upande wa Amana, Dk Kimei, alisema katika mwaka 2011 amana za wateja zilikua kwa asilimia 19 kufikia Sh bilioni 2.4 kutoka Sh bilioni 2.0 kwa mwaka 2010.
Alisema ukuaji huo umechangiwa na chapa ya Benki , ambayo imeendelea kuboreshwa kwa kampeni za masoko, kuanzishwa na kubuniwa kwa bidhaa na huduma mpya, kukua na kusambaa kwa njia za utoaji huduma.