Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Machinga Complex yatangaza mikakati kuinusuru na ufisadi

10th June 2012
Print
Comments

Baada ya Bodi ya kituo cha biashara cha Machinga Complex, kuibua ufisadi ndani ya kituo, menejiment ya kitega uchumi hicho, imetangaza mikakati ya kukinusuru ikiwa ni pamoja na kukikodisha kibiashara kwa wafanyabiashara wakubwa pamoja na ofisi mbalimbali.

Meneja wa Machinga Complex, Nyamusukuru Masondore, alisema katika mahojiano na NIPASHE jijini Dares Salaam, alipoulizwa hatua zinazochukuliwa kukiwezesha kitega uchumi hicho kufanya biashara baada ya kudorora kwa kipindi kirefu.

Ili kukusanya mapato, kujiendesha na kulipa mkopo wa ujenzi menejimenti itaanza kukodisha Machinga Complex, kwa wafanyabiashara wakubwa, ofisi mbalimbali wakati wowote kabla ya kumalizika mwaka huu.

Aliongeza kuwa wamachinga ambao ndiyo walengwa wataendelea kupewa nafasi wakati kundi la wenye mahitaji maalumu wakiwemo walemavu watabakia eneo la chini ya majengo hayo ili wafanye biashara zao.

Masondore alisema wapangaji wa mitaji mikubwa watapewa nafasi kwenye ghorofa za juu namba nne na tano za majengo hayo yaliyoko mtaa wa Shaurimoyo na watakuwa wakilipa kodi kwa bei ya soko.

Hawa kwa mujibu wa Masondera watauza bidhaa mbalimbali kwa bei ya jumla na reja reja ili kuwapa walaji uwigo mpana wa mahitaji kituoni hapo pia Wamachinga kupata sehemu ya kununulia bidhaa zao kwa bei nafuu.

Alisema wahandisi wanapima maeneo ya kukodishwa kibiashara kwa wawekezaji wakubwa na kitakachofuata ni kutangaza kuuza nafasi zitakazoainishwa kwa wateja wa mitaji mikubwa.

Ili kukabiliana na wafanyabiashara waliofunga vizimba na kuondoka manejimenti imetoa notisi kuanzia mwezi uliopita kuwataka waliofunga vizimba kulipa kodi na kuendelea na biashara na wasipofanya hivyo menejimenti itavunja vizimba na kuvikodisha kwa wateja wapya.

Masondore alisema kadhalika menejimenti itaanza kuweka matangazo na kukitangaza kwa dhati kituo ambacho tangu kujengwa hakijatangazwa kikamilifu ili kuvutia wawekezaji na wateja.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, mwaka 2005 ilikopa mkopo wa Sh bilioni 12 kutoka Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kujenga kituo hicho kilichokamilika mwaka 2010 na uendeshaji ukaanza kwa kupangisha wamachinga.

Lengo la awali lilikuwa kukodisha wateja 10,000 ambao wangelipa kodi ya sh.30,000 kwa mwezi lakini ilipatikana idadi pungufu ya wapangaji kiasi cha 4,206 hivyo kukwamisha malengo.

Masondore alifahamisha kuwa kuwapandishia gharama za kodi, kukosekana wapangaji na baadhi ya Wamachinga kutelekeza vizimba vya biashara kulisababisha biashara kudorora na kuibuka mvutano baina ya wamachinga na kituo, hivyo ni wakati wa kurejesha imani kwa wadau.

Alipoulizwa kuhusu mapendekezo ya kuvunja masoko ya Mchikichini na Ilala kwa madai kuwa yanachukua wateja Machinga Complex , alisema manejimenti inaangalia ushindani na kuboresha kituo na siyo kubomoa masoko jirani. “Kama soko lipo kisheria sina tatizo nalo, liendelee.”

Wamachinga wanaouza bidhaa kituoni hapo walitoa maoni yao kwa kuishauri manejimenti mpya kuwa na uadilifu katika kukodisha vizimba badala ya kuwapa jamaa za vigogo wa jiji na serikali.

Nicholous Magova mwenye kizimba E329 na Gudila Mushi walihimiza kuanza kujaza vizimba vya chini kisha vya juu badala ya kupangisha kiholela kama ilivyo sasa.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment