


.jpg)
Kutekwa na kisha kupigwa vibaya kiasi cha kuumizwa hadi kuwa mahututi kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, kumeibua taharuki kubwa nchini na sasa kila mahali kuna hali ya hofu na hasira huku viongozi wakuu wa serikali wakikutana kujadili hali ya usalama nchini.
Katika taharuki hiyo, makundi mbalimbali na mwananchi mmoja mmoja wamelaani vikali unyama huo wakieleza kwamba inahitajika tume huru kuchunguza tukio zima na kuweka ripoti yake hadharani.
Kadhalika, Jumuiya ya Madaktari imekataa kamati iliyoundwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Kova akizungumza na waandishi wa habari juzi alisema Jeshi la Polisi limeunda jopo hilo itakayoongozwa na Mkuu wa Upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam, ACP Salim Msangi, kwa ajili ya kuchunguza tukio.
Hata hivyo, akizungumza na waandhi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage, alisema hawaitambuwi kamati hiyo kutokana na mazingira ya tukio hilo ambayo yana utata na kuzua maswali mengi kama polisi walihusika au la.
“Kulingana na mazingira yalivyo ya tukio hili la kutekwa na kujeruhiwa Dk. Ulimboka Polisi hawawezi kuaminika kufanya uchunguzi huo,” alisema Chitage.
Alisema vitisho vinavyotolewa na Serikali kwa madaktari havitaweza kumaliza na kutatua mgogoro uliopo baina yao, bali njia pekee ni kutekeleza madai wanayoyataka.
HALI YA DK. STEPHEN ULIMBOKA
Habari kutoka Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) zinasema kuwa Dk. Ulimboka anaendeela vizuri na kwa sasa anaweza kuwatambua watu wanaofika kumuona hospitalini hapo na hata kuweza kuongea tofauti na awali.
Kiongozi wa jopo la madaktari wanaomtibu Dk. Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba, alisema hali yake inaendelea kuimarika ukilinganisha na hali aliyokuwa nayo juzi.
Alisema Dk. Ulimboka alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake haswa kichwani kwenye ubongo wake, kifuani, mikononi, ambapo aling’olewa meno mawili ya mbele pamoja na kucha.
Aidha ulinzi mkali umewekwa na madaktari katika wodi alikolazwa Dk.Ulimboka ambapo haruhusiwi kuingia mtu yeyote.
DK. ULIMBOKA AZUNGUMZA
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Namala Nkopi, aliwaonyesha waandishi wa habari picha za video aliyomrekodi Dk. Ulimboka ambayo alionekana akisema anaendelea vizuri.
“Najisikia maumivu sana, naomba niendelee kuwa kwenye mapumziko, kwa yeyote anayetaka kuniona kwa sasa jambo hilo lisifanyike,” alisema Dk. Ulimboka.
HUDUMA MOI HOI
Kusitishwa kwa huduma MOI kumezua malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Zuhura Yusuph mkazi wa Arusha ambaye ameteguka nyonga aliliambia NIPASHE kuwa tangu juzi hajapata huduma yoyote.
Naye Felista Ngulimi, mkazi wa Shinyanga, alisema kuwa alifika jana ambayo ilikuwa ni siku yake ya kuonana na daktari, lakini hakufanikiwa kuonana naye, na kwamba amefikia nyumba ya kulala wageni na hana pesa ya kukidhi mahitaji yake muhimu.
MUHIMBILI HAKUNA DAKTARI
Kitengo cha dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambacho kilikuwa kikifanyakazi tangu kuanza kwa mgomo jana hakukiwa na daktari yeyote wala mgonjwa aliyepokelewa na wagonjwa waliolazwa wodini hawakupa huduma za matibabu.
Uchunguzi wa NIPASHE ulibaini kwamba hakuna daktari kutoka wizarani ambaye aliletwa Muhimbili kama alivyokuwa ameahidi Waziri Mkuu bungeni jana asubuhi.
PINDA: UTATA MTUPU
Akijibu maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jana asubuhi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema mazingira ya tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka, bado yana utata mwingi na hivyo ameagiza uchunguzi wa tukio hilo ufanyike haraka.
Alitoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe.
Mbowe alitaka kujua kama kauli ya Pinda juzi bungeni kuwa liwalo na liwe lilikuwa na maana gani hasa kwa sababu imeibua hofu kwa wananchi, kwani muda mfupi baada ya kauli hiyo habari za tukio la Dk. Ulimboka kutekwa, kupigwa na kuondolewa kucha zilizagaa na kuleta hofu na kuhoij serikali inatoa kauli gani kuhusiana tukio hilo.
Akijibu, Pinda alisema jambo hilo linaweza kupata tafsiri tofauti lakini kilichokuwa kikimsumbua kichwani ni kuwa jambo hilo lilikuwa Mahakama Kuu.
“Na kwamba kutoa kauli wakati jambo liko mahakamani ni dhahiri ningeonekana mtovu wa taratibu zetu za kikatiba, ndiyo maana nikafika mahali kuwa katika mazingira yaliyopo nikaoneka nikawa mtovu kwa kutaka kuelezea kinachoendelea ni nini,” alisema na kuongeza:
“Ndio maana nikasema najua watanilaamu viongozi wa mhimili mwingine lakini nafikiria natakiwa kusema kitu fulani sasa hilo lilitafsiriwa vingine na hapa niliona dada yangu Halima (Mbunge wa Kawe-Chadema, Halima Mdee) alijaribu kuliunganisha na hili la Ulimboka," alisema na kuongeza:
“Na wakati nilipokuwa nasema hata sikuwa na taarifa hizo (za kutekwa kwa Dk. Ulimboka), nilichokuwa nikisema kilikuwa kikihusiana na mgomo wa madaktari.”
Pinda alisema juzi aliahidi kuwa serikali ingelitoa kutoa kauli bungeni, lakini juzi usiku alishauriana na vyombo vingine vya dola na kuonekana kuwa hawawezi kulieleza jambo hilo mbele ya Bunge wakati kesi iliyopo mahakamani imeahirishwa hadi mwezi ujao.
Hata hivyo, alisema kutolewa kwa kauli linategemea Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakavyopendekeza.
Kuhusu la Dk. Ulimboka, alisema amesikitishwa na jambo hilo na kwamba utaratibu wa kumaliza mgogoro huo ulikuwa ukiendelea vizuri.
Alisema taarifa aliyopelekewa ina mazingira ambayo bado yanahitaji uchunguzi wa haraka ili ukweli kuhusiana na mazingira ya tukio hilo uweze kujulikana.
“Mazingira yake kwa kweli kidogo yana utata mwingi na yanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina. Kila mmoja anahisia zake wengine wanafikiria hiki, wengine wanafikiria ni serikali, hayo yote hatuwezi tukakaa bungeni tukayasemasema, mimi kwa upande wangu kama itakuwa ni serikali tutakuwa ni watu wa ajabu sana,” alisema.
Alisema Dk. Ulimboka wamekuwa naye na wameshirikiana katika suala hilo na kila mmoja anajua kuwa mgogoro huo umepelekwa mahakamani.
Alisema suala hilo linampa tabu na kuwa kama ni serikali wamefanya hivyo ili iweje. Alisema njia rahisi ni kusubiri uchunguzi ufanyike.
Katika swali lake la nyongeza Mbowe, alisema kuna taarifa kuwa madaktari katika Hospitali za Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Hospitali ya Rufaa ya KCMC na maeneo mengine mengi wameanza mgomo rasmi kwa kutokwenda kazini jana.
Alihoji kama serikali inasubiri kutoa tamko mara baada ya kesi iliyoko mahakamani kumalizika, ni hatua gani za ziada zinazochukuliwa kutafuta ufumbuzi wa muda wa tatizo hilo ili kunusuru madhara yanayotokana na mgomo huo.
Pinda alisema serikali imezungumza na vyombo mbalimbali ili kuona mazingira waliyonayo ili kunusuru maisha ya wagonjwa.
Alisema wamewaomba Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na hospitali nyingine zilizochini ya Jeshi kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za matibabu.
“Tumeona pia ni vizuri tuwaite na madaktari wengine ambao wamestaafu na waliopo wizarani, watafutiwe njia ya kurudi ili waweze kutoa huduma hiyo.
Kwa maana ya hatua tumeona hilo tuendelee nalo, lakini hatujachoka pia kuzungumza kama tutapata fursa ya kuzungumza na madaktari,” alisema.
MLATA: MGOMO UNAFADHILIWA
Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalum (CCM), Martha Mlata, alisema kuna taarifa kuwa mgomo wa madaktari unasababishwa na vikundi vya watu wanaowapa fedha madaktari ili wagome.
Alisema lengo ikiwa ni kufanya nchi isitawalike na kuhoji iwapo serikali iko tayari kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Akijibu Pinda alisema hata yeye amesikia taarifa hizo na tayari ameshaviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kulifuatilia na kama kuna ukweli serikali itafuatilia na kuchukua hatua.
LISSU: PINDA JIUZULU
Kuhusu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, (Chadema) Tundu Lissu alihoji kwa nini asijiuzulu kwa kushindwa kushughulikia mgomo wa madaktari wakati Februari mwaka huu alisema hautatokea tena.
Akijibu, Pinda alisema siyo kila jambo mtu utajiuzulu au kuwajibika, na haoni kwa suala hilo anastahili kuchukua hatua hiyo.
“I have done my best (nimefanya jitihada za kutosha), kumaliza hili la mgomo, tukubali lina changamoto nyingi na limeingiliana," alisma.
Hata hivyo, Lissu aliuliza swali la nyongeza na kumtaka Pinda kama amejaribu kwa kadri ya uwezo wake lakini ameshindwa, kwa nini hajiuzulu?, Spika Anne Makinda alisema swali hilo lisijibiwe kwa sababu limerudiwa, hata hivyo Pinda alimjibu Lissu kwa kusema: "No Lissu nakuheshimu sana lakini hiyo siyo best approach.”
BARAZA LA USALAMA LAKUTANA
Haya yakijiri Dodoma Pinda alitoboa bungeni kuwa alikuwa na Rais Jakaka Kikwete lakini ameondoka Dodoma kurejea Dar es Salaam, kwa ajili ya kukutana na Baraza la Usalama wa Taifa.
Pinda alisema hayo wakati wa kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa papo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kutokana na kuweko kila dalili kuwa hali ya usalama imedorora nchini.
Mbunge huyo alisema Serikali ya awamu ya nne iliposhika madaraka kwa kasi kubwa ilipambana na wimbi la ujambazi lilokithiri nchini.
Alisema hata hivyo hivi sasa wimbi hili limeanza tena na linatoa taswira ya hofu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.
Alitoa mfano wa matukio ya kuvamiwa kwa watalii na majambazi katika mbuga za Serengeti, biashara ya usafirishaji wa binadamu lililotokea Kongwa ambapo wahamiaji 43 walipoteza maisha na tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka.
Alitaka kufahamu serikali inachukua hatua gani ili kuwaondolea hofu wananchi.
Pinda alisema Baraza la Usalama litakutana kwa ajili ya kujadili na kuamua hatua za kuchukua ili kupambana na matokeo ya uhalifu yaliyojitokeza hivi karibuni, pia alisema matukio ambayo yanaitia hofu hata serikali.
“Tulikuwa na Rais (Jakaya Kikwete), ambaye ameshaondoka kwenda Dar es Salaam, kwa sababu ya kwenda kuzungumza jambo hili, nadhani Baraza la Usalama wa Taifa, watalijadili na kutoa maelekezo ya hatua gani za kuchukuliwa katika kipindi kifupi,” alisema.
TUME HAKI ZA BINADAMU WALAANI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imeeleza kusikitishwa na kitendo cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka na imeleeani tukio hilo.
Taarifa ya Mwenyekiti Tume hiyo, Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Manento, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kinyama kwani kinakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Kifungu cha 12(2) kinachoitaka jamii kutambua na kuthamini utu wa mtu na pia kifungu cha 5 cha Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
“Tume inatoa wito kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliofanya kitendo hicho cha kinyama, sababu za kufanya kitendo hicho na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wananchi, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamelaani tukio hilo na kuita serikali ifanye uchunguzi haraka.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kitendo hicho ni cha kulaaniwa na kuiomba serikali kufuatilia ili kubaini wahusika.
“Tunalaani kitendo hicho, tunaomba serikali ifuatilie ili kubaini waliohusika na sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema serikali inatakiwa kufuatilia suala hilo kwa haraka zaidi kwa sababu eneo alilotekwa Dk. Ulimboka ni asasi ya serikali, sehemu ya Usalama wa Taifa.
“Tunalaani vikali kitendo hicho na tunasikitika sana, serikali ichunguze tukio hilo kwa sababu limetokea wakati ina mgogoro na madaktari,” alisema.
Aliongeza: “Sehemu ile aliyotekwa Dk. Ulimboka nia asasi ya serikali, sehemu ya usalama wa taifa, hivyo endapo italifumbia macho suala hili ni lazima kutakuwa na utata.”
CHADEMA WATAKA TUME HURU
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaka iundwe tume huru itakayochunguza ukatili aliofanyiwa Dk. Ulimboka.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema kuna matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakiundiwa tume ya uchunguzi, lakini hakuna majibu yoyote ambayo yametolewa kwa sababu serikali haiwezi kujichunguza yenyewe.
"Tunataka tume huru itakayoshirikisha wadau mbalimbali kama vile wanasheria, madakatari na mashirika binafsi ili itoe majibu ya uchunguzi," alisisitiza.
Aidha, Kigaila alimtaka Rais Kikwete aeleze mambo waliyokubaliana katika kikao chao na madaktari katika mgomo wa Februari.
Pia alimtaka Rais Kikwete aeleze sababu za kushindwa kutekeleza makubaliano hayo hadi kufikia hatua ya mgomo kujirudia katika kipindi cha miezi minne tu.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Dodoma; Ninael Masaki, Elizabeth Zaya, Samson Fridolin na Gwamaka Alipipi, Dar.